JE UNAJUA THAMANI YA UNACHOKITAKA? (HADITHI)-1

Hello habari ndugu mfuatiliaji wetu wa makala zetu na habari zetu katika BLOG yetu (www.jocheinc.blogspot.com) na katika APPLICATION yetu inayojulikana kwa jina la JocheApp (unayoweza ipata katika Playstore ya Simu yako kwa kuidownload bure kabisa). Tunashukuru kwa kutuunga mkono.

Leo tunaswali ambalo tunapenda kukuuliza wewe msomaji nalo ni JE UNAJUA THAMANI YA UNACHOKITAKA? 

Tunaanza na hadithi moja ya zamani kidogo ambayo wasimuliaji wengi wa hadithi walipenda kuisimulia hata Hayati Baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere aliwahi isimulia mahali fulani. Nayo ni kama ifuatavyo:-

Hapo zama zale palikuwa na nchi moja ya mbali sana ambapo ilisadikika kwamba kulikuwa kuna msichana mmoja mrembo sana ambaye hajawahi kutokea katika nyakati hizo na alikuwa anakaa mlimani juu kabisa ya kilele. Wanaume wengi walihamasika kutaka kumpata huyo msichana ili aweze kuwa mke wao.
Basi watu wengi wakawa wanafunga safari kuelekea kwenye huo mlima na walipofika hapo chini ya mlima walikuwa wanakutana na bibi mmoja kizee anawauliza kwa masikitiko na sauti ya upole “mnaenda wapi wajukuu zangu?” Basi vijana wakawa wanamwambia bibi tunaenda huko juu kumfata msichana mrembo, yule Bibi akawa anawapa masharti ya kuzingatia ili waweze kufika katika kilele cha Mlima huo wa Ajabu anapoishi msichana huyo mrembo.

Akawa anawaambia, “ unapoanza kupanda mlima huu wa ajabu kuelekea kule kileleni alipo mrembo utasikia sauti nyingi sana zinazosema HUYOOO HUYOOOOOO, MKAMATEEE MCHINJEEE, HUYOOO MUUENI, lakini usigeuke nyuma we songa mbele tu na kadri unavyokaribia juu ndivyo zitakavyokuwa zinaongezeka kuwa kali na sauti kuwa kubwa sana.. Na endapo ukigeuka nyuma tu utageuka kuwa jiwe”. Basi vijana wengi walijitahidi kupanda mlima lakini zile sauti zilivyoanza kupamba moto waligeuka na kuwa mawe... Mlima ule ukawa na mawe mengi sana sana kutokana na wengi kushindwa kutimiza masharti.


Basi siku moja katika kijiji cha Mzoke habari hizi za huyu Msichana Mrembo na Mlima wa Ajabu zikafika na kuenea kwa wanakijiji, wazazi wengi waliwakaza vijana wao wa kiume wasiende huko maana hakuna aliyewahi kwenda akarejea salama. Basi kulikuwa na Kijana mmoja ambaye alikuwa ni yatima wazazi wake waliuawa na wanyama wakali wakati yuko mdogo walipoenda kulima katika mashamba ya kijiji yaliyopo huko msituni. Jina lake aliitwa Joe, aliposikia habari hizi akaingia na shauku kubwa sana akanuia moyoni mwake kuwa atakwenda katika mlima huu wa ajabu nae akajaribu bahati yake ya kumpata Msichana Mrembo aliye katika Mlima wa Ajabu. Basi siku iliyofuata kijana Joe akaenda nyumbani kwa rafiki yake wa tangu utotoni ambapo ndipo alipolelewa mpaka akawa mkubwa, alipofika kwa rafiki yake huyo akamshirikisha dhumuni la safari hiyo ya asubuhi, mwisho akashauriana na rafiki yake aliyeitwa Mwilo na kufikia muafaka ya kwamba watoroke kesho usiku, Basi ilipofika siku ya siku waliyoipanga wakaondoka vijana hawa wawili usiku wa kiza kizito ili wasiweze kuonekana na wanakijiji. Safari yao ilikuwa ndefu sana maana ni umbali mkubwa wakapita misitu minene kwa muda wa siku Tatu Mchana na Usiku. Mara ghafla kwa mbali wakauona ulipo mlima ule wa Ajabu wakasogea mpaka karibu kabisa.

Joe na rafiki yake kipenzi Mwilo wakafurahi sana kuona wamefika katika mlima huo wa Ajabu, kiu yao ya kufika kileleni alipo Msichana Mrembo iliongezeka na wakapata nguvu maana safari yao imeanza kuzaa matunda.

Ghafla Mwilo akamuuliza Joe, “rafiki yangu Joe tumetoka pamoja mpaka hapa na tunaenda kuupanda mlima lakini kule juu yupo Msichana Mrembo tena mmoja lakini sisi tuko wawili je nani kati yetu atamchukua?”. Lilikuwa swali zito sana kwa Joe wakajadilia na mwisho wakaafikiana kuwa Mwilo ndio amchukue msichana yule pindi watakapofika kileleni.

Nini kitaendelea? Je Mwilo na Joe watafanikiwa kufika Kileleni? Ni nini mwisho wa patano lao?

Karibu tena katika Sehemu ya Pili ya Swali Letu na Hadithi hii Fupi..
________________________________
Mwandishi: Joseph Geotham Mrema
Joche Inspirational and Motivational Inc
www.jocheinc.blogspot.com

Contact: +255712851687 (Call&Whatsapp)
Email: josephgeotham4@gmail.com

Follow us
Fb: Joseph Geotham Mrema
Instagram: joseph_geotham_mrema
Tweeter: Joseph Geotham Mrema
Youtube: Joseph Geotham Mrema
Fb Page: Joche Talks

————————————————

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...