JE UNAJUA THAMANI YA UNACHOKITAKA? (HADITHI)-2
Hello habari ndugu mfuatiliaji wetu wa makala zetu na habari zetu katika BLOG yetu (www.jocheinc.blogspot.com) na katika APPLICATION yetu inayojulikana kwa jina la JocheApp (unayoweza ipata katika Playstore ya Simu yako kwa kuidownload bure kabisa). Tunashukuru kwa kutuunga mkono.
Leo tunaswali ambalo tunaendelea kukuuliza wewe msomaji nalo ni JE UNAJUA THAMANI YA UNACHOKITAKA?
____________________________________
Ghafla Mwilo akamuuliza Joe, “rafiki yangu Joe tumetoka pamoja mpaka hapa na tunaenda kuupanda mlima lakini kule juu yupo Msichana Mrembo tena mmoja lakini sisi tuko wawili je nani kati yetu atamchukua?”. Lilikuwa swali zito sana kwa Joe wakajadilia na mwisho wakaafikiana kuwa Mwilo ndio amchukue msichana yule pindi watakapofika kileleni.
Hapo ndipo tulipoishia sehemu ya kwanza. Sasa tuendelee sehemu ya pili ndugu msomaji wetu wa Makala zetu katika Blog yako pendwa na vijana ya (www.jocheinc.blogspot.com).
Basi hawa marafiki wawili Joe na Mwilo wakaukaribia ule mlima, wakati wanaanza kuweka hatua ya kwanza kwenye kilima kile ghafla ikasikika sauti hafifu yenye mawimbi na iliyochoka toka katika kichaka kilicho karibu na njia ile ya kupanda kuelekea mlimani ikiuliza ,”mnaenda wapi wajukuu zangu?”. Vijana wale wawili wakapata hofu kubwa sana maana toka wameingia katika msitu ule hawakukutana mtu yoyote na hawakudhani kama wataweza kukutana na mtu. Basi wakajibu kwa pamoja huku wakiwa na hofu kuu , “tunaenda kumchukua mrembo wa kule juu kileleni”.
Walivyojibu vile wakaona mtu anatoka katika kichaka kile, oooh lahaula alikuwa ni yule bibi kizee akawatazama vijana wale wadogo. Akawaone huruma akawaambia ,”wajukuu zangu huko mnapotaka kwenda ni hatari, vijana wengi wameenda hawajarudi, akawaonyesha mlimani mnaona hayo mawe mengi yanayouzunguka mlima ni vijana wenzenu waliotaka kupanda kilima hiki lakini wakashindwa kutimiza masharti”.
Looh! Vijana wale walipotazama mlima wakaona mlima umejaa mawe mengi sana na hata njia imesongwa songwa na mawe kila kona. Wakamuuliza bibi ,”mbona mawe mengine ni makubwa na mengine ni madogo?”. Bibi yule akawajibu,” Wajukuu zangu hapa hupita watu wa kila umbo wapo wakubwa ndio hayo mawe makubwa na wengine wadogo ndio hao wadogo”. Joe na Mwilo wakaingiwa na hofu iliyo kuu.
Mwilo akamvuta Joe pembeni akamwambia ,”mwenzangu safari tuishie hapa naogopa kuwa jiwe mimi mwenzio, wazazi wangu wananitegemea”. Joe akamtazama rafiki yake kwa huruma sana akamwambia kwa sauti ya unyonge lakini yenye ujasiri mkubwa ndani yake ,”Mwilo rafiki yangu wewe ni ndugu yangu, Kwanini kukata tamaa kwa kuangalia walioshindwa wakati hata hujajua masharti au jambo lililowafanya wakawa mawe?”. Mwilo akashtuka akasema ,”ni kweli usemalo rafiki yangu, hebu twende tukamuulize bibi atuambie nini cha kufanya bila shaka atakuwa anajua”. Basi vijana wale wawili wakarejea kwa bibi wakamuuliza ,”bibi kwanini hao wamegeuka mawe? Nini cha kufanya ili usiwe jiwe?”
Bibi yule mzee akawatazama kwa muda kidogo akameza mate kidogo akawaambia ,”wajukuu zangu katika kupanda mlima huu kuelekea kileleni kuna masharti unayopaswa kuyatimiza na kukikosea tu unageuka jiwe kama haya mengine unayoyaona”. Mwilo na Joe wakatazamana wakaendelea kumsikiliza bibi kwa makini ili wasipitwe na jambo hata moja. Basi bibi yule akaendelea ,”wajukuu zangu mnaona ule mti pale mbele yenu uliokauka? Mkifika pale ndio masharti nitakayowambia yaanza kufanya kazi, sasa nisikilizeni kwa makini”. Bibi akasema Wajukuu zangu? Vijana wale wakaitikia kwa pamoja Naam bibi. Bibi akasema ,”mkishaanza kuupanda mlima na mkapita ule mti niliowaonyesha mtaanza kusikia sauti zinaanza taratibu zinasema UYOOO, UYOOOOOO UUUUUYOOOOOO, MKAMATEEEEE, MUUEEEEEE, UYOOOO UYOOOOO, ACHINJWEEEE UYOOOOOOOO, UYOOOOOO na kadiri unavyozidi kwenda juu sauti zinaongezeka mvumo kiasi ambacho hamtaweza kusikilizana wewe na mwenzio lakini msigeuke nyuma hata iweje, atakayegeuka nyuma tu hapo hapo atageuka kuwa jiwe kama haya mengine unayoyaona”. Loooh! Vijana wale wakamshukuru bibi kwa jinsi alivyowambia na kuwapa maelekezo hayo. Wakati wananza safari Bibi akawasisitiza bado ipo nafasi ya kutokwenda huko juu maana alijua watageuka mawe tu, kwakuwa Mwilo na Joe walishanuia kupanda wakamuaga bibi na safari ikaanza kuelekea mlimani.
Hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu mara wakatokomea tena katika chochoro za kuelekea kileleni mara wakafika katika ule mti aliowaonyesha bibi. Mwilo akamtazama rafiki yake akamwambia ,”rafiki yangu Joe sasa ile kazi ndio inaanza, usisahau tukifika kileleni yule msichana ni wa kwangu kama ulivyosema”. Joe akatingisha kichwa ishara ya kukubali na kuwa anakumbuka. Wakaupita mti ule wakatembea kwa muda bila kusikia sauti yoyote wakasema yule bibi alikuwa anatukatisha tamaa tu. Wakiwa katika kuongea huko mara upepo ukaanza kuvuma kwa mbaliii na sauti iliyo ya upole ikasikika HAOO HAOOOO UYOOO UYOOOOO MKAMATEEEE UYOOO MCHINJEEEE, vijana wale wakaendelea kusonga mbele lakin kadri walivyosogea hatua moja sauti iliongeza sauti na upepo ukavuma kwa nguvu zaidi UYOOOOO UYOOOO UYOOOO MKAMATEEEE UYOOOO MCHINJEEEE UYOOOOO. Sauti zikaongezeka zaidi mpaka wakasimama lakini hazikunyamaza ziliendelea. Wakiwa katika hali hiyo Walishaanza kukata tamaa maana vishindo nyuma kama vilikuwa vinawakaribia kuwakamata, ooooh pasipo kutarajia Kijana Mwilo uzalendo ukamshinda akageuka ili achungulie wamefika wapi hao wanaotaka kuwakamata, ghafla akageuka Jiwe hapo hapo... oooh Joe akaogopa sana akalia mno lakini hakuacha kusonga mbele huku analia kwa kumpoteza rafiki yake ambaye alikuwa kama kaka yake. Baada ya mwendo wa Masaa yasiyopungua sita Joe akaanza kuona juu kidogo kuna nyumba nzuri imejengwa (wakati huo sauti bado zinavuma kwa sauti kuu na ngurumo kama jeshi linakuja nyuma yake) Joe asogea kwenye nyumba ile iliyokuwa na uzio mkubwa sana. Joe akagonga katika mlango wa uzio ule, wakati huo ndio mpaka vumbi linavuma na kelele za UYOOO UYOOOO AULIWEEE UYOOO MKAMATE UYOOO. Wakati akiwa katika hali hiyo ngumu mlango ukafunguliwa na msichana mmoja mrembo sana aliyevaa mavazi mazuri ya thamani kubwa sana, akamkaribisha Joe aingie ndani kwa tabasamu pana sana. Basi wakati Joe anaweka hatua yake ya kwanza kuingia ndani mara ghafla sauti zote zikakoma hapo hapo. Mara pasipo kutarajiwa Joe akadondoka na kuzimia hapo hapo. Msichana yule akamchukua Joe akamuingiza ndani akamlaza katika eneo lenye upepo, mara baada ya muda Joe akazinduka akajikuta yuko katika mazingira mazuri sana na pembeni yake yuko msichana mrembo amemuandalia chakula.
Msichana yule akamkaribisha Joe ale chakula na maji maana alionekana kadhoofika. Joe akaanza kula kwa haraka sana maana alikuwa na njaa. Baada ya kula msichana yule akamuuliza Joe ni wapi anatokea anaitwa nani na dhumuni la yeye kuja mpaka kule juu. Basi kijana Joe akamjibu maswali yote kama yalivyo. Joe akaukiza je ndio wewe yule msichana mrembo wa mlima huu wa ajabu? Yule msichana akasema ,”ni mimi”. Joe akamwambia kuwa nilikuwa nakuja na rafiki yangu lakini yeye aligeuka Jiwe wakati tunakaribia hapa, nilikuahidi kuwa tutakapofika kileleni yeye atakuchukua wewe mrembo.
Msichana yule akamtazama Joe kwa umakini akamwambia kweli wewe unamoyo mzuri ndio maana uliweza kufanikiwa kufika hapa. Msichana yule akaendelea ,”Joe yule mwenzio alishindwa kufika hapa na hivyo amepoteza haki ya mimi kuwa mke wake, nitakachoweza kukusaidia ni jambo moja, ni kumrejesha rafiki yako asiendelee kuwa jiwe lakini kuna masharti hapa. Ili kupata dawa ya kumponya rafiki yako ni lazima uchague kati ya Chupa hii ya DAWA au BEGI LILE LA DHAHABU”. Dooh ukawa mtihani mwingine tena kwa Joe maana alikuwa kijana masikini hana hata jembe la kulima. Msichana yule akaendelea leo utalala hapa kesho ukiamka tutaanza safari ya kushuka toka hapa kilimani lakini pia asubuhi hiyo utafanya uchaguzi kati ya vitu nilivyokuambia. Basi wakaenda kulala.
Usiku kucha Joe aliwaza lile begi la Dhahabu lakini pia akawaza chupa ile ya dawa kumponya rafiki yake kipi achukue.
Kulipokucha asubuhi na mapema msichana yule akaja akamuamsha Joe na kumpeleka kwenye chumba cha kufanya uchaguzi kati ya Dawa na Dhahabu. Basi Joe kwa kuzingatia hekima aliyonayo akachagua dawa ili akamponye rafiki rafiki yake. Msichana yule akamtazama Joe kwa makini sana akamwambia kuwakuwa hukuchagua mali bali ulichagua kumponya rafiki yako umedhihirisha wewe ni mtu mwema na begi hilo la dhahabu utapata mara mbili yake. Looh! Kijana Joe alifurahi sana. Safari ya kushuka kilima ikaanza. Wakashuka mpaka pale ambapo Mwilo aligeuka jiwe akataka kuweka dawa kwa lile jiwa ambali ndio Mwilo aligeuka. Msichana yule akamwambia ukimwagia Mwilo peke yake ndio atapona, je hawa wengine hutaki wapone?? Joe akauliza sasa nifanyaje??? Msichana akamwambia Joe unaukumbuka ule mti mlioonyeshwa na bibi pale chini?? Akasema ndio naukumbuka. Msichana yule akamwambia ,” ili uwaponye watu wote hawa kamwage dawa katika mlima huu nao watapona. Basi wakashuka walipofika pale kwenye mti Joe akamwaga dawa ile mara watu wote wakasimama wakashangilia na kumpongeza Joe kwa ukarimu wake na ujasiri wake. Rafiki yake Mwilo nae alikuwa miongoni mwao.
Habari za Joe zikaenea nchi yote na vijiji vyote. Basi Joe akajijengea heshima katika kijiji chake. Na maisha yake na msichana yule yakaendelea na kuzaa watoto huku wakiendelea kusaidia jamii iliyomzunguka kwa mawazo na kifedha pia maana alikuwa na fedha nyingi mno.
Na huu ndio mwisho wa Hadithi yetu ya JE UNAJUA THAMANI YA UNACHOKITAKA?.
—————MWISHO—————
JE UMEJIFUNZA NINI KATIKA HADITHI HII? Usiache KUWEKA MAONI YAKO au KUTUTUMIA UJUMBE MFUPI KATIKA MAWASILIANO YETU HAPO CHINI... KARIBU SANA
___________________________________
Mwandishi: Joseph Geotham Mrema
Joche Inspirational and Motivational Inc
www.jocheinc.blogspot.com
Contact: +255712851687 (Call&Whatsapp)
Email: josephgeotham4@gmail.com
Follow us
Fb: Joseph Geotham Mrema
Instagram: joseph_geotham_mrema
Tweeter: Joseph Geotham Mrema
Youtube: Joseph Geotham Mrema
Fb Page: Joche Talks
————————————————
No comments
Post a Comment