KWANINI HAPA?
Karibu katika mfululizo wa makala zetu katika Application ya JocheApp
Imeandikwa na Joche wa JocheApp
Nakusalimu na natumaini hujambo kabisa.
Wengine wakiwa makazini muda huu, na wengine wakiwa katika biashara zao na wengine wakiwa katika kipindi cha likizo na wengine wakiwa katika madarasa kuendelea na kusoma.
Leo natamani kuzungumzia juu ya jambo moja ambalo muda mwingi huwa tunakosea au tunajisahau pindi tunapokipata kile ambacho tumekuwa tukikitamani kukipata.
Ngoja nianze kwa kuongelea kwa namna hii.
🖊Ni kweli umekuwa na ndoto za kuwa na biashara. Baada ya muda ukaweza kuanzisha biashara. Swali linalofuata je nini kinafuata baada ya kuwa na biashara?
🖊Ni kweli umekuwa ukitamani kuwa na kazi (kuajiriwa). Swali linalofuata je ni nini kinafuata baada ya kupata kazi hiyo?
🖊Ni kweli umekuwa ukitamani kurudi shule au kupata elimu na kusoma zaidi. Swali linalofuata je nini kinafuata baada ya kupata hiyo nafasi ya kurejea darasani tena?
🖊Ni kweli umekuwa ukitamani kuwa na mahusiano/ndoa. Swali la ziada ni nini kimefuata baada ya kupata hayo mahusiano/ndoa?
🖊Ni kweli umekuwa ukitafuta marafiki wa kusapoti ndoto zako. Je ni nini kimefuata baada ya kupata hao marafiki?
🔘Ni maswali machache lakini unaweza kujiuliza katika nyanja zote za maisha ambayo unayoyaishi. Na kwakupitia maswali haya unaweza ona vitu vichache ambavyo hutokea navyo ni kama ifuatavyo:-
1. KUJISAHAU
Hapa ni eneo sugu sana kwa watu wengi ambapo pindi wakishapata kile kitu walichokuwa wanakitaka basi hujisahau kabisa.
Mfano: Mtu alikuwa anataka kazi kapambana kasaidiwa kaipata lakini baada ya muda fulani huyu mtu utashangaa anaanza kuchelewa kazini au muda mwingine anatega kazini au muda mwingine hatekelezi majukumu yake kazini (achana na kipindi ambacho unakuta mtu huyu anamatatizo).
Au Umeanza biashara lakini oda za wateja wako hauzitekelezi kwa wakati au hautimizi ahadi zako kwa wateja wako. Na muda mwingine unawapelekea bidhaa duni tofauti na ulichowaambia
Huku tunaita kujisahau na muda si mrefu biashara au kazi hii utashangaa imekuponyoka na kapewa mtu mwingine au unafukuzwa kazi kabisa.
2. KURIDHIKA
Eneo hili la kuridhika huwakumba watu wengi sana. Kitendo ambacho hufanya mambo kwa namna ya kawaida kabisa na huwa hawajiongezi kwa namna yoyote ile. Yaani mtu akiwa na uwezo wa kupata kile kiwango alichonacho basi hataki kuongeza bidii katika kukikuza zaidi na zaidi. Mwisho wa siku hugotea hapo.
Hii hutokea kwa kwa watu wa maeneo mengi katika mahusiano pia watu hukutana na hizi hali. Mwanzoni mtu anakuwa na moto lakini akishafanikiwa kuanzisha mahusiano hayo basi hugotea hapo excitement yote hupotea.
Na hata katika maeneo mengine vivyo hivyo. Kuridhika kumefukia mambo mengi sana na hasa katika kufanikiwa kwa mtu. Maana ukisharidhika shauku yote uliyokuwa ndani hupotea na huona kila kitu ni sawa. Hatamani kusonga mbele zaidi na zaidi.
3. KUKOSEKANA KWA MALENGO ENDELEVU
Malengo mara nyingi huonyesha dira ya kule unapotaka kwenda na katika kutumiza huko malengo kuna kuna na hatua kwamba nikifika hapa nitafanya hili na hili na mara baada ya hili nitafanya lile ili nifike pale yaani kwa lugha rahisi wanasema ramani ya jambo unalolifanya kwa kuzingatia hatua ukizojiwekea.
Hivyo kutokana na watu wengi kukosa malengo endelevu huwafanya hata wanapoanzisha vitu vyao vinakosa mwendelezo maana utakuta mtu anatamani kuwa na biashara lakini ukimuuliza nini kinafuata baada ya kuwa na biashara hana majibu. Lakini kama angekuwa na hatua inayofuata basi mtu huyu angesonga mbele kwa nguvu sana na wala asingefanya vitu kimazoea au kwa kuridhika.
Mfano: Mtu anandoto za kuwa Profesa siku moja katika taaluma yake. Utamuona hata katika mfumo wake wa usomaji na mwenendo wake wa kimasomo.
Lakini pia hata wafanyabishara. Mtu mwenye ndoto za kuwa mfanyabiashara wa kimataifa utamuona speed yake na mwenendo wake. Haiwezekani unatamani kuja kuuza bidhaa nchi ya jirani wakati mteja wa mtaa wa pili kumuhudumia oda yake inachukua miezi tena bila sababu ya msingi.
Au unataka kuwa kiongozi wa watu siku za usoni wakati unaishi maisha yasiyo na mwelekeo. Kama huna mwelekeo huna sifa ya kuwa kiongozi ambaye anatakiwa kuonyesha watu mwelekeo.
“Utendaji wako wa vitu unamchango mkubwa sana katika kutoa picha yako ya maisha katika siku za usoni”
4. KUTOKUWA NA MSIMAMO THABITI
Katika maisha ni muhimu sana kuwa na misimamo hasa juu ya maisha yako ya kila siku na mambo unayoyafanya. Umeamua kuwa mcheza mpira basi tia bidii hapo katika eneo hilo mpaka ufikie katika mafanikio uliyoyataka, unataka kuwa muuzaji wa ice cream fanya kwa bidii usiyumbishwa na mawazo na matamanio ya vitu wanafanya wengine kisa leo kapata faida kubwa na wewe hujapata hiyo faida bado.
Ni dhahiri bila kuwa na msimamo utajikuta unayumba kila siku unajambo jipya kila siku hukamilishi ukichokianza (sio mbaya kuwa na vyanzo vingi vya mapato or kuwa na mambo mengi ya kufanya) lakini angalia je ni kweli moyo wako umetaka kufanya hayo? Or ni matamanio ya kisa fulani kafanikiwa na wewe unafanya? Au kisa fulani kapata faida zaidi na wewe unataka kufanya?
Ni muhimu sana kuwa na msimamo ili uweze kufanya mambo yako kwa uzuri na kwa nafasi na kwa shauku kubwa ya kufanikiwa.
Ziko sababu nyingi sana sana ambazo husababisha kuwa hapo ulipo.. hutegemea na mtu husika na mazingira yake ya kila siku na uwezo wake wa kielimu na kiuzoefu katika kuyafikia mafanikio anayoyataka au aliyojipangia kuyafikia.
Nikirejea katika agenda husika ya “KWANINI HAPA”
Kwa kusoma hizo pointi chache hapo juu umeweza ona vitu vinavyokufanya uwe hapo ulipo na usisogee mbele zaidi.
Hii ni katika nyanja zote ukiona hausogei na hujui sababu ni nini jaribu kuangalia hizo chache nilizozitaja na nyinginezo kama hizo.
Jaribu kuzibadilisha na utaona mafanikio na mabadiliko makubwa sana ambayo utafurahia na kuhamasika kwa hatua moja zaidi kila siku.
Asante.
JocheApp
—————————————————-
Author: Joseph G Mrema
Contacts: 0712851687
Email: josephgeotham4@gmail.com
www.jocheinc.blogspot.com
—————————————————-
Share with others....
No comments
Post a Comment