SIRI ILIYO BAYANA
Mtunzi~Kinyafu Marco.
©️2018,
kinyafumarcos@gmail.com.
0714 129 520.
1.Kuna misingi mitano,katika haya maisha
Sikiliza hili neno,njia litakuonyesha
Hii siri nzito mno,wengi yawafanikisha.
Maisha bila kanuni,katu hatuwezi shinda.
2.Wa kwanza ndio uzima,ambao Mola katupa
Pumzi katupa twahema,na leo ndo tupo hapa
Elewa hili mapema,usitumie kwa pupa
Timiza malengo yako,hali ungali uzima.
3.Wa pili ndio wakati,ambao twautumia
Kwenye mingi mikakati,mipango tulonuia
Hili ndilo swala nyeti,mwenzangu hebu sikia
Wakati ukipoteza,hauwezi jirudia.
4.Watatu ndio nidhamu,katika yako malengo
Tumia yako kalamu,andika yote mipango
Ili ushike hatamu,nidhamu ndio kiungo
Nidhamu yako binafsi,hiyo ndo silaha yako.
5.Wanne ndio juhudi,katika kwako kutenda
Kila siku jitahidi,kitu kipya kukiunda
Cha jana leo kizidi,hapo ndipo utashinda
Juhudi ukiiweka,utafaidi matunda.
6.Wa mwisho huu mzito,huu waitwa subira
Hapa ipo changamoto,wengi wakosa busara
Matumbo yajaa joto,wanaogopa hasara
Subira ikiwa ndogo,faida huwezi pata.
7.Siri iliyo bayana,kila mtu kaijua
Nimekupa kwa mapana,kazi kwako kuamua
Siri sio siri tena,fumbo nimelifumbua
Siri iliyo bayana,anza leo kuitenda.
___________MWISHO_______________
🌐JocheApp
No comments
Post a Comment