INJINI 11 ZA KUJA NA MAWAZO MAZURI YA BIASHARA - 2
1. INJINI YA KWANZA: Fursa au Mawazo ya Biashara yatokanayo na MATATIZO.
Injini ya kwanza katika Somo la kwanza la Injini 11 za Kubuni Mawazo bora ya Biashara, inaitwa TATUZI. Injini hii imetokana na MATATIZO.
TATUZI ni Mawazo ya Biashara au aina za Fursa zinazotatua matatizo ya watu. Na watu wapo tayari kulipia gharama kutatua matatizo hayo.
2. Kabla sijaendelea na SOMO hili la kwanza ninaomba usimame kidogo.
Fikiria, Mara ngapi umemsikia rafiki yako analalamika na kero Fulani?
Mara ngapi umemsikia mfanyakazi mwenzako analalamika na changamoto Fulani?
Mara ngapi umemsikia ndugu yako analalamika na tatizo Fulani?
Mara ngapi umesikia Serikali au hata wabunge wanalalamika na kero Fulani?
Mara ngapi umemsikia wanafunzi wanalalamika na Kero Fulani?
Mara ngapi umesikia abiria wanalalamika na tatizo Fulani?
Mara ngapi umesikia wafanyabiashara wanalalamika na tatizo Fulani?
Mara ngapi umesikia wamama wanalalamika na kero Fulani?
Mara ngapi umekutana na changamoto yoyote ?
Kero zote, Changamoto zote, Matatizo yote na lawama zote ulizowahi kuzisikia ama kukutana nazo ni FURSA.
Ukitathmini lawama, kero na changamoto tunazoishi nazo kila siku ni FURSA.
Ukiangalia mazingira uliyozungukwa yapo matatizo mengi sana yanayohitaji utatuzi.
Yapo matatizo yanayokera, yanayodharirisha, yanayoua, yanayosababisha msongo wa mawazo, yanayopoteza muda, yanayokosesha raha, yanayovuruga ndoa yaani ni mengi.
Watu wote tupo tayari kumlipa mtu yeyote anayeweza kutatua matatizo tunayoyapitia.
Ukubwa wa tatizo ndiyo ukubwa wa Malipo utakayolipwa ikitokea umetatua TATIZO.
Maumivu makali ya matatizo ya watu maana yake ni hela nyingi unazoweza kutengeneza kupitia matatizo hayo , ukija na majibu ya matatizo hayo.
Nimeshuhudia watu wanauza nyumba ili apate hela atatue tatizo,
Kuna watu wengine mpaka wanadiriki kutengeneza matatizo kwa jamii ili waweze kuuza bidhaa zao kutatua matatizo hayo.
Nikisema kuwa hata Corona inawezekana ni tatizo lililotengenezwa na mjasiriamali mwenye njaa ya hela ili aweze kuuza MAJIBU au kutawala kiuchumi utanibishia?
Unadhani Billgates akifanikiwa kushinda kupitisha Vaccines zake zinazoaminika labda zinaweza kutibu Corona au kuzuia ...ni mabilioni kiasi gani atakayotengeneza kupitia tatizo linaloitwa Corona?
Fuatilia utashangaa kuwa viwanda vinavyozalisha madawa ya binadamu yaani Pharmaceutical industries vinalaumiwa kwa kuzalisha madawa yanayozalisha matatizo mengine zaidi ili waendelee kuzalisha madawa zaidi yanayotatua matatizo hayo na kujipatia hela.
3. Anza kujiuliza sasa hivi, kipindi hiki cha Corona bidhaa unazozalisha zinatatua tatizo gani?
Biashara yako inatatua tatizo gani?
Wengi wetu tunakuja na biashara za Kuiga, ukimuona mtu anatengeneza bidhaa za Lishe , unaanza kumsumbua naomba unifundishe formula.
Umekaa na kujiuliza unataka kutatua tatizo gani?
Kipindi ambacho watu tunapitia Changamoto kubwa kubwa kama Corona ni kipindi cha kunufaika na kutajirika. Ni kipindi cha Fursa.
Anza kuangalia kwenye mtaa wako, kijiji chako, mkoa wako, nchi yako na bara lako la Afrika. Unaona matatizo mangapi?
4. Nakupa tu mfano wa jamaa mmoja anaitwa, Tristan Walker aliyeamua kutumia tatizo na akaanzisha kampuni yake maarufu inaitwa Bevel. Huyu jamaa alikuwa anapitia matatizo ambayo wanaume wote wenye ndevu tunayapitia. Kama ni mwanaume mwenye ndevu umewahi kunyoa ndevu na ukasikilizia maumivu ya vile vipele vinavyouma?
Mimi nina ndevu najua maumivu yake.
Tristan aliamua kuja na vifaa vya kunyolea visivyoumiza au vinavyoondoa maumivu ya vipele kwenye ndevu. Kila mtu alitaka kununua hivyo vifaa, kwasababu vipele vinauma ndugu yangu. Vipele Vinauma sana kwa wale wanaofahamu maumivu yake. Ndani ya muda mfupi akafanikiwa kupata mpaka wawekezaji waliowekeza Zaidi ya dola 33Million. Ndani ya miaka 6 kampuni ya Proctor & Gamble ilikuja kununua kampuni yake na kutengeneza mabilioni ya dola.
5. Mwingine ni rafiki yangu wa muda mrefu sana kutoka Kenya, yeye alipojifungua mtoto wake wa kwanza. Chuchu zake zilikuwa ndogo na wala hazikuweza kutoa maziwa kwa mtoto. Yeye na mume wake walianza kutumia pesa nyingi sana kununua maziwa ya kopo. Lilikuwa ni tatizo kubwa sana kwake kiasi ambacho mama mkwe wake alimnyanyasa. “kwanini huzalishi maziwa. Hizo chuchu kifuani ni maembe au mawe?” Aliteseka sana. Ilibidi aanze kutafuta njia mbadala. Alihangaika sana bila suluhu.
Rafiki yake mmoja akamwelekeza namna ya kutengeneza mbegu za mronge, na kutumia unga wake. Alianza kutumia bidhaa za mronge kutatua matatizo yake anakuambia baada ya muda mfupi maziwa yalianza kutoka tena kwa wingi kama yamefunguliwa bomba. Ilikuwa ni furaha kubwa kwenye familia yake. Hicho kipindi ameajiriwa, akaanza kufanya tafiti Zaidi kuhusu mbegu za mronge. Ikawa kama madhumuni yake duniani ya kutatua matatizo ya wanawake wenye matatizo kama yake. Ikawa biashara yake kuu, yenye lengo la kutatua matatizo ya wanawake wenye matatizo ya kutopata maziwa kwa watoto. Alianza kutembea mpaka nchi mbalimbali kama balozi wa bidhaa za Mronge. Akaacha kazi na mpaka sasa ni mwanadada maarufu Kenya anayesambaza bidhaa za tiba kwa wanawake hasa zitokanazo na mronge.
Naomba nikuulize swali, hiyo biashara yako inatatua matatizo gani haswa. Unaweza kuyataja?
6. Afrika ni bara lililojaa matatizo mengi. Maana yake ni dunia iliyojaa fursa za hela.
1. MAGONJWA.
Magonjwa ni hela. 24% ya Magonjwa yote yanayotokea duniani yapo Afrika.
Matatizo ya Ukosefu wa madawa Muhimu pamoja na Chanjo , ni nani ataitumia fursa hii kuwa msambazaji wa vifaa vya maabara pamoja na madawa kwa mfumo rahisi na kwa bei rahisi.
Matatizo ya huduma mbovu mahospitali kwengine hakuna hata vifaa, kuna sehemu nimeenda vijijini wanatembea zaidi ya 50Km kufuata huduma za Afya? Nani anaweza kuja na fursa ya Telemedicine yaani huduma ya Afya kwa tekinolojia , mobile health Care.
Matatizo ya Utapiamlo, yaani ni kero kubwa. Nani atakuja na bidhaa za Lishe, ziwe za maji, au Unga au hata matunda na michanganyiko mbalimbali.
Matatizo ya Ugonjwa wa Corona , nani atakuja na njia mbadala ya kusambaza bidhaa zinazojenga kinga ya Mwili.
Matatizo ya Malaria, Ukimwi, Kansa, Vitambi, Upungufu wa Nguvu za Kiume, kifua kikuu, Matatizo ya Uzazi na mengine mengi. Haya matatizo yote yanahitaji Mjasiriamali mmoja ajitokeze na kutatua. Ni hela
Tuwapate wapi wajasirimali kama akina Emmanuel Katongole, kutoka Uganda mzalishaji na mwenye kiwanda cha Kuzalisha Madawa?
Kampuni yake ya Quality Chemicals Limited, inazalisha madawa ya Malaria na Ukimwi. Kabla ya hapo alikuwa ni msambazaji wa Madawa mbalimbali kwa kuagiza kutoka Asia, kwa mtaji wa Tshs.70million, lakini akaingia zaidi kwa kuungana na wazalishaji waliokuwa wanamuuzia kutoka Asia , wanafahamika kama CIPLA na kuanzisha kiwanda cha Madawa ambacho kimekua kiwanda kikubwa ambacho kina zaidi ya thamani ya Tshs. 250 Billion na zaidi.
Kwahiyo kampuni yake ya Quality Chemicals Limited ipo pamoja kama kampuni ya pamoja na CIPLA.
Zipo fursa nyingi sana zitokanazo na matatizo ya Magonjwa ambazo zinahitaji mtaji mdogo sana, nyingine zinahitaji tekinolojia kidogo sana , na uzuri wapo watu ambao wanawekeza kwenye sekta hizi.
Kuna fursa za kutibu magonjwa ya Ngozi kama Ranchia Droganis kutoka Afrika kusini, yeye alianza kwa kuingiza Tshs.800,000 na zaidi kwa mwezi kwa kuuza mafuta yanayotibu ngozi yaani natural essential oils pamoja na sabuni za kiasili zinazotibu magonjwa mbalimbali ya Ngozi kama dada Grace Products na wengine wanaofanya vizuri. Yaani kampuni yake kwasasa ya Africology Spa inaingiza zaidi ya dola za kimarekani $ 1millio sawa na billion 2.3 kwa mwezi kwa pesa za kitanzania.
Kuna Fursa ya Kuzalisha bidhaa za Kinga ya Mwili, ukizingatia kwasasa tuna Changamoto ya kiafya kutokana na Corona. Nani atatengeneza jamani?
Kuna Fursa ya Kuzalisha Bidhaa za Lishe hata kuwa na kampeni ya kupunguza Utapiamlo kwa watoto vijijini nani atajitokeza, kuna pesa nje nje..
Kuna fursa ya kusambaza vifaa vya maabara na madawa.
Kuna fursa za Tiba Chakula na tiba lishe, nani ataingia na kuanza kuuza formula ya Vyakula kwa kusambaza vyakula maofisini hasa vyakula vinavyotibu kisukari, kitambi, nguvu za kiume, unene na mwili kujaa mafuta, Uzazi….Yaani hapa unaweza kusajili watu wakawa kwenye mpango mkakati wa kuwapelekea tiba Chakula na Lishe kwenye maofisi yao. Nani anafanya?
Kuna watu wana tibu magonjwa sugu yanayotisha ikiwa ni pamoja na mifupa, kuna wasukuma wanatumia tiba mbadala aisee. Yaani hospitali zikalale. Nani anaweza kutengeneza mtandao na kuwajengea mazingira mazuri wakawa partners wake na wakaingiza hela na kutrendi hapa mjini. Tusiwe na tabia ya kudharau hawa watu, mie nimejionea kwa macho yangu mwenyewe.
Matatizo ni mengi sana unayoweza kuanzia nayo kama fursa kwako , NJAA, ELIMU, USAFIRI, MUDA, UMEME, MAKAZI, MAZINGIRA NA UCHAFU, AJIRA, NDOA, MAPENZI, MALAZI, WATOTO, WAKINA MAMA, MALEZI NA MENGINE MENGI.
Hizi zote ni Fursa zinazotajirisha na zilizotajirisha wengi. Hii ni sehemu ya kwanza ya Somo la kwanza. Tutamalizia sehemu ya pili ya somo la kwanza.
Endelea kufuatilia kozi hii itabadili mwelekeo mzima kuhusu fursa na biashara unazoweza kuanza.
Fursa 101 Afrika
No comments
Post a Comment