KIMETA

1. Kabla ya kuwika jimbi,Natoka usingizini
Kandili yangu ya tambi,Ninaiweka mezani
Kiti napangusa vumbi,Sasa natulia chini
Kalamu yangu nashika,Wazo langu kulileta

2. Ninaanza kwa huzuni,Iliyokosa kifani
Nina mengi ya moyoni,Nayaleta hadharani
Nayatoa mafichoni,Sote tupone jamani
Kimeta hiki kimeta,cha tutafuna jamani

3. Jamani kuna kimeta,kimefika kijijini
Hivi nani kakileta,kutoka huko mjini
Jawabu nalitafuta,naumia akilini
Kimeta hiki kimeta,chanzo chake ni kwa nani?

4. Kilianza mwaka juzi,nikakiona kwa mbali
Nyumbani kwa baba Suzi,niliziona dalili
Mara kakipata Rozi,sasa kikawa dhahili
Kimeta hiki kimeta,chatutafuna jamani



5. Kikasogea mwembeni,kwenye nyumba ya udongo
Kakipata mama Jeni,yule muuza matango
Kimeshuka na bondeni,kule kwa mzee jongo
Kimeta hiki kimeta,kinaenea jamani

6. Hivi sasa kinameza,wananchi wakijiji
Vipi tutakifukuza,ndio bado najihoji
Janga kulikotokomeza,tuupate uponyaji
Kimeta hiki kimeta,dawa tuitafuteni.

7. Tushapoteza watoto,wababa nao wamama
Hili kwetu janga zito,limeileta zahama
Limekuwa kama moto,nyoyoni linatuchoma
Kimeta hiki kimeta,sote tukiondoeni.

8. Sasa na tujadilini,tuufanye upekuzi
Sote na tukae chini,tutafute ufumbuzi
Tufikiri kwa makini,tumpate mchochezi
Kimeta hiki kimeta,tukiondoe jamani.

9. Kila mtu apambane,kuilinda kaya yake
Sote na tusemezane,kimeta hiki kitoke
Tena na tushikamane,kwa pamoja tusichoke
Kimeta hiki kimeta,tukitoe kijijini.
_______________________________
Mtunzi: Kinyafu Marcos
Contacts: +255 714 129 520

Imeletwa kwako na JocheApp
www.jocheinc.blogspot.com

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...