PENIELA (Season 1 Ep 27)

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA

Najua nimekukosea sana mambo mengi lakini tafadhali naomba tofauti zetu tuziweke kando kwa sasa na tulishughulikie suala hili.Ni muhimu sana kwangu ” Akasema Flaviana.Jaji Elibariki akainama akawaza halafu akainua kichwa na kusema

“ Ok my love.I’ll do it for you”

Wakakumbatiana na Flaviana akaondoka.Kichwa cha Jaji Elibariki kilikuwa kizito kama kimefungwa jiwe.Alihisi kuchanganyikiwa,hakujua angewezaje kuipata ripoti ile aliyoitaka mke wake.Alibaki ameegemea mti kwa dakika kadhaa akiwaza

“ How am I going to do it? Nahisi kuchanganyikiwa sielewi nitafanya vipi kufahamu nini kilimuua Dr Flora.”

Kwa takribani dakika kumi alikuwa amezama katika mawazo na mwishowe akachukua simu yake na kuzitafuta namba za simu za Mathew

“ I need Mathew.” Akasema na kumpigia.Simu ikaita bila kupokelewa.Akapiga tena lakini bado simu haikupokelewa ,akahisi kuchanganyikiwa

ENDELEA………………………

Mathew na Dr Michael walipigwa na butwaa wakabaki wakitazamana.Mathew alitamani iwe ni ndoto lakini haikuwa hivyo.Ni kweli chumba kilikuwa kitupu na John Mwaulaya hakuwepo mle chumbani.

“ Haya ni mazingaombwe makubwa .Mgonjwa John amekwenda wapi? Saa nne na dakika ishirini nimetoka humu na kumuacha akiwa amelala hapo kitandani sasa amekwenda wapi? Nani kamtoa? Akauliza Dr Michael.Mathew akafungua mlango wa maliwato akachunguza kila pembe akatoka na kuchungulia dirishani ,halafu akamfuata Dr Michael.Akamkaba shingoni na kumgandamiza ukutani akamuwekea bastora kichwani

“ Niambie John yuko wapi? Akasema kwa ukali .

Dr Michael alikuwa akitetemeka mwili mzima kwa namna Mathew alivyokuwa amebadilika. “ Si..s..sifahamu mahala aliko” akasema kwa woga.Jasho lilikuwa likimtoka

“ Nakupa dakika moja ya kusema ukweli ama sivyo mwanao hutamuona tena.John mwaulaya yuko wapi?!!..

“ Sifahamu aliko.Naomba uniamini sifahamu mahala aliko. Hata mimi nashangaa ni kitu gani kimetokea.Ninaapa sifahamu John yuko wapi” akasema Dr Michael na kwa mbali machozi yakimlenga kwa woga

Sura ya Mathew ilikuwa imebadilika.Alikuwa na hasira zisizomithilika.Akamtazama Dr Michael kwa macho makali na kuzidi kumuogopesha

“ Dr Michael hii ninafasi yako ya mwisho. Tafadhali niambie John Mwaulaya yuko wapi?

“ Sifahamu yuko wapi.Kama ningejua mahala aliko ningekwambia,lakini sifahamu yuko wapi” akasema Dr Michael huku akitetemeka.

“ Dr Michael nitazame vizuri machoni” akasema Mathew.

“ Unavyoniona ninafanya utani siyo?

“ Hapana hautanii!! Akasema Dr Michael kwa woga

“ Ok basi kabla ya saa moja jioni ya leo,familia yako yote itakuwa imeteketea tukianzia na mwanao mdogo Michael kama hutaweza kunieleza yuko wapi John Mwaulaya” akasema Mathew.Machozi yakamtoka Dr Michael

“ Ndugu yangu sifahamu mahala aliko huyu mgonjwa.Kama ningejua mahala aliko ningekwambia.Ta

fadhali naomba usiidhuru familia yangu.Naombeni mnidhuru mimi lakini si familia yangu” akaomba Dr Michael.Mathew akamtazama kwa sekunde kadhaa halafu akamuachia.Dr Michael akakaa chini

“Anasema ukweli,hafahamu chochote” akawaza Mathew huku akipumua kwa kasi.

“ Team SC 41 wamefahamu kwamba tuko hapa na shida yetu ni John mwaulaya na ndiyo maana wakawahi kumuondoa.Ninachojiuliza ni vipi wameweza kugundua kwamba tuko hapa na tumekuja kwa ajili ya John Mwaulaya? Akajiuliza Mathew na kushindwa kupata jibu akakumbuka kwamba hakuwa amewataarifu wenzake kile alichokikuta mle ndani.

“ Anitha,John ametoweka humu chumbani.Narudia tena John ametoweka humu chumbani”

“ Mathew hii imetokeaje?Ameruhusiwa na daktari? Akauliza Anitha

“ Hapana Anitha.John hajaruhusiwa na daktari ,ametoroshwa.They know we are here.” Akasema Mathew na kumshika mkono Dr Michael akamuinua

“Twende tuondoke” akasema Mathew

“ Unanipeleka wapi? Mwanangu yuko wapi?

“ Nasema twende tuondoke hapa haraka sana!! …Akafoka Mathew.Dr Michael akaogopa na kuanza kutembea kwa kasi akimfuata Mathew wakashuka ghorofa na moja kwa moja wakaelekea katika maegesho ya magari wakaingia katika gari la Mathew.Kabla hajawasha gari simu ya Dr Michael ikaita

“ Mke wangu ananipigia” akasema Dr Michael

“ mwambie aondoke nyumbani haraka sana kwani si sehemu salama kwa sasa.Sisi tunakwenda kwanza shuleni kuwachukua wanao wawili halafu tutampitia na yeye mahala atakapokuwa amekwenda na tutakwenda katika sehemu salama.Kwa sasa wewe na familia yako maisha yenu yako hatarini” akasema Mathew.Bila ubishi Dr Michael akabonyeza kitufe cha kupokelea

“ Hallow “ akasema Dr Michael

“ Hallow Dr Michael” ikasema sauti ya upande wa pili.Nusura Dr Michael aangushe simu kwa mstuko alioupata.Aliyekuwa akiongea upande wa pili hakuwa mkewe bali sauti nzito ya kiume.Mathew aliuona mstuko alioupata Dr Michael ,akamuelekeza abonyeze kitufe cha kuwezesha sauti kubwa kusikika ili aweze kusikia maongezi yale.Bila ubishi Dr Michael akakibonyeza.

“ Hallow Dr Michael “ akasema mtu Yule.

“ Wewe ni nani na kwa nini uko na simu ya mke wangu? Akauliza Dr Michael

“ Dr Michael nakufahamisha kwamba mkeo tunaye hapa ,tunamshikilia “

“ unasemaje?!! Dr Michael akapatwa na mstuko mkubwa

“ Mkeo tumemchukua tuko naye kwa hiyo usisumbuke kumtafuta”

“ Wewe ni nani? Akauliza Dr Michael kwa wasi wasi

“ Huna haja ya kunifahamu lakini nataka tu ufahamu kwamba mkeo tunaye,yuko salama na atakuwa salama endapo tu utakuwa msikivu na kufuata kile tutakachokuelekeza.”

“ Mungu wangu ! kitu gani hiki kinanitokea mimi na familia yangu? Akajiuliza Dr Michael

“ Dr Michael! Akaita Yule jamaa simuni

“ Tafadhalini naomba msimfanye chochote mke wangu.” Akaomba Dr Michael

“ Hatuna haja ya kumfanya chochote mke wako Dr Michael ila tutalazimika kufanya hivyo pale utakapokwenda kinyume na sisi.”

“ Mnataka nini toka kwangu? Akauliza Dr Michael

“ Nitakupigia baadae kukupa maelekezo lakini nakuonya kwamba usithubutu kupeleka suala hili polisi wala kumweleza mtu mwingine yeyote .Kufanya hivyo kutasababisha umkose mke wako.Usifanye jambo lolote la kijinga na kuhatarisha uhai wa mke wako.Kwa sasa ongea na mkeo” akasema Yule jamaa na kumpa simu mke wa Dr Michael aongee na mumewe

“ Hallow “ akasema mke wa Dr Michael

“ Hallow mpenzi,uko salama? Hawajakuumiza hawa mabazazi? Akauliza Dr Michael

“ Hapana hawajanidhuru lakini wametishia kwamba watanifanyia kitu kibaya endapo hautafanya wanachotaka ukifanye.Tafadhali mume wangu fanya chochote wakatachokuambia ufanye ili uweze kuniokoa.Ninaogopa sana” akasema mke wa Dr Michael huku akilia.

“ Usilie mke wangu,tafadhali usilie.Nakujua wewe ni mwanamke jasiri kwa hiyo usilie nitafanya kila watakachoniamuru kufanya kwa ajili ya kukuokoa wewe..Siko tayari udhurike mke wangu” akasema Dr Michael na mara simu ikakatwa.Mwili ulikuwa ukimtetemeka hakujua afanye nini.

“ Wamemteka mke wangu” akasema Dr Michael

“ Watamuua mke wangu.Watu hawa ni akina nani na wanataka nini kwangu? !!Kwa nini wamemteka mke wangu? Akauliza Dr Michael

“ Dr Michael ni vigumu kusema moja kwa moja watu hawa ni akina nani lakini ni watu wanaokufahamu vyema .Nakuahidi kwamba tutawatafuta na kuwapata pamoja na kumpata mkeo akiwa salama.Ninachoh

itaji ni ushirikiano wako”

“ Tafadhali naomba ufanye kila linalowezekana umkomboe mke wangu.Unafahamu mahala alipo? Unawafahamu waliomteka? Akauliza Dr Michael ambaye alionekana kuchanganyikiwa

“ Dr Michael sina jibu lolote la kukupa kwa sasa lakini nakuahidi kukulinda wewe na familia yako.Mimi na wenzangu tutafanya kila linalowezekana kumtafuta mkeo” akasema Mathew huku akiwasha gari na kuliondoa kwa kasi.

“ Ndugu yangu sema chochote unachohitaji nikifanye ili familia yangu iweze kuwa salama.” Akasema Dr Michael.Kabla Mathew hajamjibu Anitha akamuita

“ Mathew kuna kitu nimekigundua,mtazame vizuri Dr Michael kuna kifaa anacho ambacho kinarusha mawasiliano.Nimeona hapa kwenye kompyuta yangu kuna mawasiliano yanatoka” .Mathew akasimamisha gari na kumtazama Dr Michael

“Kuna nini mbona umesimamisha gari? Mbona unanitazama hivyo? Akauliza Dr Michael lakini Mathew hakumjibu kitu akaendelea kumkagua.Akachukua simu ya Dr Michael na kuizima.

“ Anitha vipi hapo bado unaona kitu chochote? Akauliza Mathew

“ Bado kuna kitu anacho kinachorusha mawasiliano kupeleka sehemu Fulani”

Mathew akamtoa Dr Michael nje ya gari akaanza kumkagua .Katika mfuko wake wa koti kulikuwa na kalamu mbili,akazichukua zile kalamu na kuzifungua.Katika kalamu moja akakutana na kitu kisicho cha kawaida.Akashuka na kuziweka kalamu zile mbele ya tairi halafu akawasha gari na kuzikanyaga halafu akasimamisha gari.

“ Anitha ulikuwa sahihi.Dr Michael alikuwa amewekewa kifaa kidogo sana cha mawasiliano katika kalamu yake na ndiyo maana watu wale waliweza kusikia kila tulichokuwa tunakiongea na Dr Michael hivyo kwa haraka wakamuondoa John Mwaulaya.” Mathew akamfahamisha Anitha

“ Kwa sasa naona shwari sioni kama kuna mawasiliano yanayoruka kwenda sehemu nyingine” akasema Anitha

“ Good Job anitha”

“ So whats next Mathew? Akauliza Anitha

“ Tunasubiri maelekezo atakayopewa Dr Michael na watekaji halafu tutajua nini cha kufanya lakini wakati tukisubiri hayo tunaelekea White shield international high school kuwachukua watoto wa Dr Michael na kuwaweka sehemu salama.” akasema Mathew

“ Unasema nilikuwa nimewekewa kifaa cha mawasiliano? Akauliza Dr Michael

“ Ndiyo Dr Michael.Katika kalamu yako moja kulikuwa na kifaa kidogo cha mawasiliano ambacho kazi yake ni kunasa kila utakachokiongea na kuyarusha kwa wahusika.Kifaa hiki ndicho kilinasa maongezi yetu asubuhi nilipokuwa ninakuamuru unipeleke chumba cha John na kwa kuwa walihisi kuna hatari inaweza kutokea ikawalazimu kumuondoa John haraka sana.” Akasema Mathew na kuzidi kumshangaza Dr Michael

“ Unataka kuniambia kwamba watu waliomteka mke wangu wana uhusiano na Yule mgonjwa aliyetoroka?

“ Ndiyo.” Akajibu Mathew.Dr Michael akainama chini akafikiri na kukumbuka kitu

“ Unaweza kuwa sahihi ndugu yangu.Nimekumbuka kuna siku moja nilipokuwa nikimuhudumia John,mmoja wa wale vijana aliniomba kalamu lakini hakunirudishia kalamu yangu na badala yake akanirejeshea kalamu nyingine kabisa kwa madai kwamba kalamu yangu haiandiki vyema.Nilishukuru na sikuuliza chochote na wala sikufahamu jambo lolote kuhusiana na nini kilikuwamo ndani ya kalamu ile.Kama ni wao ndio waliomteka mke wangu basi watakuwa wamefanya hivyo kwa sababu moja tu.”

“ sababu gani? Akauliza Mathew

“ John anatakiwa afanyiwe upasuaji wa kichwa na mimi ndiye daktari pekee wanayemtegemea kufanya upasuaji huo..Huyu John ni nani? Akauliza Dr Michael

“ Upasuaji huo ulitakiwa ufanyike lini?

“ Kuna dawa tulizokuwa tunazisubiri ziwasili ndani ya siku mbili hizi halafu tumfanyie upasuaji”

“ ok vizuri.Tutaongea zaidi baadae kwa sasa tusipoteze wakati tuelekee moja kwa moja shuleni kuwawahi watoto” akasema Mathew na kuwasha gari wakaondoka kuelekea White shield international high school.

“ Hii ni vita kali na inabidi kujihami kwa kila namna inavyowezekana.Team SC 41 tayari wanafahamu kwamba kuna watu wanaowafuatilia .Ninaanza kuingiwa na woga lakini sintarudi nyuma,lazima nipambane nao.Safari hii sintokubali wanishinde” akawaza Mathew.

Walifika katika shule wanakosoma watoto wa Dr Michael .

“ Usiwaeleze chochote watoto kwa sasa ili usiwasababishie mstuko .Hatutaki suala hili lisambae“Mathew akamwambia Dr Michael ambaye alishuka na kuingia ndani ya jengo la shule.Baada ya kama dakika saba akarejea akiwa na watoto wawili.Mathew akafungua mlango wakaingia ndani ya gari

“ Tunaelekea wapi sasa hivi? Akauliza Dr Michael

“ Tunaelekea nyumbani kwangu” akasema Mathew na kuwasha gari wakaondoka.

Waliwasili katika makazi yake na Dr Michael alishindwa kuonyesha furaha yake kwa kukutanishwa tena na mwanae Michael Jr aliyekuwa ameongozana na akina Anitha.Watoto wote wa Dr Michael hawakuelewa kilichokuwa kinaendelea na kwa nini walikuwepo pale kwa Mathew.Mathew akamuelekeza Anitha awapeleke watoto katika chumba cha kupumzikia kilichokuwamo na runinga na michezo ya kompyuta.

“ Dr Michael pole sana kwa matatizo yaliyokupata “ akaanzisha mazungumzo Mathew

“ Nashukuru sana,lakini ningependa niwafahamu ninyi ni akina nani? Ni polisi au usalama wa taifa? Akauliza Dr Michael

“ Mimi ninaitwa Mathew,mwenzangu pale anaitwa Noah na Yule mwanadada anaitwa Anitha.Sisi si polisi wala usalama wa taifa ila kwa pamoja sisi ni kikosi cha uchunguzi tunaochunguza kuhusu tukio Fulani la mauaji tata.Uchunguzi wetu umetufikisha hadi kwa John mwaulaya mgonjwa aliyekuwa amelazwa wadi PV2 – 78 na ndiyo maana lengo langu lilikuwa ni kumuhoji na kutaka kuufahamu ukweli.” Akasema Mathew

“ Kama ni hivyo msingetumia njia ya kumteka mwanangu na kumfanya chambo ili niweze kufanya mnachokitaka.Endapo ungenieleza ukweli ningeweza kuwasaidia bila hata ya kutumia njia ile ya utekaji.” Akasema Dr Michael

“ Dr Michael ,huwa tunatumia njia kama hii kwa sababu kwa njia ya kawaida watu wengi huwa hawako tayari kutoa ushirikian😮k sasa tujad……” kabla hajaendelea na alichotaka kukisema simu yake iliyokuwa mezani ikatetema,akainuka na kutazama mpigaji alikuwa ni Jaji Elibariki

“ Hallo Elibariki”

“habari yako Mathew? Akasema jaji Elibariki

“ habari yangu nzuri Mheshimiwa jaji,pole sana na matatizo”

“ Tumekwisha poa Mathew,poleni na nyie “

“ Ahsante sana Eli.Ninashukuru pia kwa mzigo wa jana Jason alinifikishia na tayari tumekwisha ufanyia kazi”

“ Ok nashukuru kama ulipata ule mzigo.Muda wowote ukikwama nitaarifu ili nikukwamue” akasema Elibariki halafu kikapita kimya kifupi akasema

“ Mathew nimekutafuta sana simuni leo lakini simu imekuwa ikiita tu bila kupokelewa.” Akasema Jaji Elibariki

“ Tulikuwa tumetoka kikazi na na simu niliitoa mlio kwa hiyo sikuweza kusikia uliponipigia.Kuna habari gani?

Jaji Elibariki akavuta pumzi ndefu na kusema

“ Mathew kuna jambo lingine limeibuka ambalo sina mwingine anayeweza kunisaidia zaidi yako”

“ jambo gani Elibariki?

“ Sintoweza kuongea nawe simuni ni jambo nyeti sana ,nitakuja hapo kwako jioni kukuona na tutaongea vizuri.”

“ Elibariki nadhani ingekuwa vyema kama ungeniambia sasa hivi kwa sababu siwezi kujua baadae nitakuwa sehemu gani kwani tunapokuwa tunaifanya kazi Fulani huwa hatuna muda maalum wa kupumzika.Naomba unieleze ni tatizo gani hilo?akauliza Mathew

Elibariki akavuta pumzi defu na kusema

“Nadhani una tarifa kuhusiana na kifo cha mke wa rais Dr Flora Joshua?

“ Ndiyo Eli nina taarifa hizo aliniambia Jason jana.”

“ Dr Flora alifariki ghafla lakini mpaka sasa bado hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusiana na sababu ya kifo chake.Kitu kingine cha kushanganza ni kwamba madaktari katika hospitali ya jeshi walikwisha anza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kubaini nini kilimuua lakini walipokea taarifa kwamba waachane na zoezi hilo” akasema Jaji Elibariki na kumstua sana Mathew

“ hebu subiri kidogo Eli ,unasema madaktari Waliambiwa waache wasifanye uchunguzi kubaini kilichomuua Dr Flora?

“ Ndiyo Mathew ,kwa mujibu wa daktari anayefahamiana na mke wangu”

“ Taarifa hiyo ilitoka kwa nani?

“ Mpaka sasa hatuelewi taarifa hiyo ilitoka kwa nani .Mke wangu ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu ana wasi wasi mno ameanza kuingiwa na mashaka sana kuhusiana na kifo cha mama yake kwa sababu jioni ya siku ile walikuwa wakutane kuna jambo kubwa ambalo alitaka kuwaeleza watoto wake lakini hakufika jioni akafariki ghafla.”

“ Ana wasi wasi kwamba yawezekana Dr Flora akawa ameuawa?

“ Kutokana na mazingira yalivyo kuna weza kuwa na hisia hizo” akajibu Elibariki

Mathew akafikiri kidogo na kusema

“ Unataka nifanye nini mheshimiwa?

“ Sifahamu kama hili linaweza kuwa ndani ya uwezo wako lakini nataka kufanya uchunguzi kubaini nini kilimuua Dr Flora.This is for my wife.” Akasema Jaji Elibariki.

Mathew akavuta pumzi ndefu akainama na kuzama katika mawazo.

“ Mathew if this is too much for you then we can leave it…” akasema Jaji Elibariki baada ya kuona kimya kinapita na Mathew hajibu chochote

“ Hapana jaji Eli,tutaifanya hiyo kazi.Consider it done” akasema Mathew

“ Thank you so much Mathew.”

“ Ok Elibariki,let me figure out how I can do this,and then I’ll get back to you” akasema Mathew

“ Ok Mathew,thank you so much.Kama kuna tatizo lolote linalohitaji msaada usisite kunitaarifu” akasema jaji Elibariki na kukata simu

“ Dah ! nahisi nimeutua mzigo mkubwa sana uliokuwa unanielemea.Suala hili ni zito na sijui litafanyikaje lakini nilishindwa kumkatalia Flaviana.” Akawaza Elibariki baada ya kumaliza kuongea na Mathew simuni

Mathew alisimama kwa sekunde kadhaa akiwaza .Jambo aliloambiwa na jaji Elibariki lilimstua sana ingawa alishindwa kukataa

“ How am I going to do it? Akajiuliza Mathew .Akainama akafikiri kwa muda halafu akamuendea Dr Michael

“ Dr Michael ,naomba unisikilize kwa makini ” akasema Mathew

“ Nakusikiliza Mathew”

“ Kwa sasa wewe na familia yako mko hatarini na mke wako tayari yuko katika mikono ya watekaji.Ninaku

ahidi kwamba mimi na wenzangu tutafanya kila tunachoweza kumtafuta mkeo na kumuokoa mikononi mwa watekaji hao.”

“ Nitashukuru sana Mathew kama utaweza kunisaidia kwa hilo”

“ Nitakusaidia kwa hilo Dr Michael lakini kwa sharti moja”

“ Sharti gani?

“ Kuna kazi ambayo nitaomba unisaidie kuifanya”

“ kazi gani?

“ Nitakueleza baadae ni kazi gani “ akasema Mathew na kuwaita akina Anitha katika chumba kingine

“ ndugu zangu mapambano yameanza.Team SC 41 tayari wamekwisha fahamu kwamba tunamfuatilia John Mwaulaya na ndiyo maana wakamuondosha pale hospitali haraka sana.Nina hakika lazima hivi sasa watakuwa wakijiuliza sisi ni akina nani na kwa nini tunamtafuta John Mwaulaya.” Akasema Mathew akanyamaza kidogo ba kuendelea

“ John Mwaulaya anaumwa na Dr Michael ndiye mtu pekee ambaye anategemewa kumfanyia upasuaji wa kichwa na hii ndiyo sababu ambayo imewapelekea wamteke mke wa Dr Michael ili kumshinikiza afanye upasuaji huo.Mpango mkubwa ulioko mbele yetu kwa sasa ni kumkomboa mke wa Dr Michael akiwa hai.Hata ikitokea Dr Michael akimfanyia upasuaji John mwaulaya lazima watamuua tu.hawako tayari kumuacha hai mtu ambaye tayari amefahamu siri zao.Tusikubali hilo litokee.We have to save Dr Michael and his family.” Mathew akanyamaza kidogo halafu akaendelea

“ Muda mfupi uliopita nimepokea simu toka kwa jaji Elibariki.Kuna jambo ambalo ameniambia ambalo limenishangaza kidogo.Mke wa rais alifariki ghafla na mpaka sasa hakuna taarifa zozote za kuhusu nini kilisababisha kifo chake.Madaktari katika hospitali kuu ya jeshi walipewa amri ya kutokufanya uchunguzi wao.Bado haifahamiki ni nani aliyewapa amri hiyo ya kutokufanya uchunguzi wa kilichosababisha kifo cha mke wa rais.Usiku wa kuamkia siku ya kifo chake Dr Flora alizungumza na wanae wawili na kuwataka waonane jioni alikuwa na jambo muhimu sana la kuwaeleza.Kwa bahati mbaya haikufika jioni na Dr Flora akafariki dunia ghafla.Ukiunganisha mambo haya mawili kuna picha inayojengeka hapa .Tunahitaji kufanya uchunguzi wa nini kilimuua Dr Flora mke wa rais”

Anitha na Noah walikuwa kimya wakimsikiliza Mathew.Suala la kufanya uchunguzi wa kifo cha Dr Flora liliwastua sana.

“ Mathew usinielewe vibaya ndugu yangu,lakini nina mashaka kidogo na kazi hii iliyoibuka ghafla kuhusiana na kufanya uchunguzi wa kifo cha Dr Flora.Hapa unazungumzia mke wa rais,unadhani inaweza kuwa rahisi ? Sisi hatuna taaluma yoyote ya udaktari tutaweza vipi kufanya uchunguzi huo? Kifo cha mke wa rais kina mahusiano yoyote na suala tunaloendelea kulichunguza ?Noah akauliza



“ Noah usianze kuogopa angali mapema.Bado tuna kazi pevu sana mbele yetu.Kwa kufanya uchunguzi huu tutamtumia Dr Michael.Nimemuahidi kumtafuta mke wake na kumpata kwa hiyo lazima atakubali kuifanya kazi hii.Kitu kikubwa na kigumu hapa ni namna gani tutaweza kuupata mwili wa Dr Flora na kuufanyia uchunguzi.Kuhusu mahusiano ya suala hili la Dr Flora na suala tunaloendelea kulichunguza,sina hakika bado kama yana mahusiano yoyote lakini yote mawili lazima tuyafanye.Tutafanya uchunguzi wa nini kilisababisha kifo cha Dr Flora na tutamkomboa mke wa Dr Michael” akasema Mathew

“ Kuhusu Team SC 41,nataka nikaingie tena katika mtandao wa hospitali na kwa kupitia kamera iliyopo nje ya lile jengo la private ward 2 ,tutaweza kuwabaini watu ambao walimtorosha John mwaulaya.Kwa kutumia program ya kulinganisha sura tunaweza kuwafahamu watu hao ni akina nani” akasema Anitha.

“ wazo zuri sana hilo Anitha.Shughulikia suala hilo na mimi ngoja nikaongee na Dr Michael ili nione namna tunavyoweza kuufanyia uchunguzi mwili wa mke wa rais kufahamu kilichomuua.” akasema Mathew.Anitha na Noah wakaelekea katika chumba chenye mitambo mbali mbali ,Mathew akaenda kuongea na Dr Michael

“ Dr Michael muda unazidi kwenda hivi sasa ni saa kumi na moja za jioni ,wakati tunasubiri hawa jamaa wapige simu na kutoa maelekezo naomba nikufahamishe kazi ninayotaka unisaidie”

“ kazi gani unataka nikusaidie Mathew?

“ Kuna mwili wa mtu ninataka kuufanyia uchunguzi ili kubaini kilichosababisha kifo chake”

Kabla Dr Michael hajajibu chochote simu yake ikaita.

“ Wamepiga tena.Hii ni namba ya mke wangu”akasema Dr Michael.

“Usiipokee kwanza,ngoja tuifuatilie tujue inapigwa toka wapi” akasema Mathew halafu akakimbia kwenda kumchukua Anitha ambaye alifika mara moja na kompyuta yake,na kuweka chombo fulani karibu na Dr Mathew halafu akamwambia aipokee na aweke sehemu ya kuongelea kwa sauti kubwa ili wote wasikie

“ Hallow”akasema Dr Michael

“ hallow Dr Michael,uko wapi?

“ Nimetoka kazini niko mahala nimepumzika nasubiri maelekezo yenu”

“ ok vizuri.Endelea kusubiri tutakupigia tena baadae kidogo.Nakukumbusha kwamba tunakufuatilia kila unachokifanya,ukithubutu kwenda polisi au kumwambia mtu yeyote Yule basi mkeo hutamuona tena.Tumeelewana Dr Michael?

“ Tumeelewana.Tafadhalini naomba msimdh..” kabla hajamaliza alichotaka kukisema simu ikakatwa

“ Umefanikiwa Anitha? Akauliza Mathew

“ Hapana,simu imewahi sana kukatika ,sijapata chochote”

“ Ok hakuna tatizo tutaendelea kusubiri maelekezo yao.Mmepata chochote katika kamera?

“ Tumegundua kwamba kuna wakati kamera iligeuzwa na kuelekezwa sehemu nyingine.Nadhani walifanya hivi ili waweze kutoka bil akuonekana katika kamera, walipotoka kamera zilirudi kama kawaida .” akasema Anitha

“Team SC41 ni watu hatari sana,muda wote wanafanya mambo yao kwa tahadhari kubwa” akasema Mathew.

TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO……………………

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...