PENIELA (Season 2 Ep 1)

SEASON 2

SEHEMU YA 1

Shughuli ya kuuaga mwili wa Dr Flora Joshua mke wa rais zilihudhuriwa na watu wengi sana.Viwanja vya ukombozi vilifurika watu waliokuja kutoa heshima zao za mwisho kwa mama huyu ambaye katika enzi za uhai wake aliweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha kiuchumi akina mama ..Alikuwa na taasisi yake ambayo iliwasaidia sana wanawake kwa kuwapatia mikopo ya biashara.

Wakati shughuli za kuuaga mwili wa Dr Flora zikiendelea Flaviana mtoto mkubwa wa marehemu alikuwa katika mawazo mengi sana kuhusiana na kile kilichomuua mama yake.

“ Usiku uliotangulia siku ya kifo chake,mama alitupigia simu mimi na Anna na akatuomba jioni ya siku ile akutane nasi kuna jambo kubwa analotaka kutueleza.Kwa bahati mbaya sana hatukufanikiwa kulifahamu jambo hilo ambalo alitaka kutueleza kwani alifariki ghafla mchana kabla ya kukutana nasi.Ni kitu gani alichotaka kutuambia? Ninahakika lazima litakuwa ni jambo kubwa kwa sababu aliweka msisitizo mkubwa .Lakini ni nani aliyemchoma dawa ile kwa kiwango kikubwa na kusababisha kifo chake? Ni kwa nini alimchoma? Akaendelea kujiuliza

“ Ninavyofahamu ni kwamba mama alikuwa akihudumiwa na daktari wa familia Dr Amos.Nina hakika yeye atakuwa akifahamu nini kilitokea.Huyu ndiye anayetakiwa abanwe na aeleze ni nani aliyemchoma mama sindano ile.Kitu kingine kuna mfumo wa kamera za ulinzi ,nina hakika lazima zitaonyesha kila mtu aliyeingia chumbani kwa mama siku ile.Lazima tumpate mtu aliyefanya kitendo hiki cha kikatili na tujue ni kwa nini alifanya vi…………….” Flaviana akastuliwa toka katika lindi la mawazo baada ya kusikia kitu Fulani cha baridi kikimgusa shingoni.Akageuka ghafla ghafla na kukutana na sura ya mwanadada aliyekuwa amejitanda sare zilizovaliwa na akina mama pale msibani ambaye sura yake ilikuwa na simanzi na alionekana kama ni mtu aliyeguswa sana na msiba ule

“ Flaviana unahitajika mara moja kule wenye gari la wagonjwa” akasema yule mwanadada.Flaviana akamtazama kwa makini lakini hakuwa akimfahamu.Hakuwa na kumbukumbu kama wamewahi kuonana.Bila kuhoji kuna kitu gani huko katuika gari la wagonjwa Flaviana akainuka na kuongozana na Yule mwanadada kuelekea katika gari la wagonjwa lililokuwa limeegeshwa pembeni kidogo ya viwanja vile kwa ajili ya dharura endapo ingetokea mtu yeyote Yule kuzidiwa.Walipolikaribia lile gari la wagonjwa Flaviana akaanza kuhisi kizungu zungu na kutaka kuanguka.Macho yake hayakuwa yakiona vizuri,akamuomba Yule mwanadada amsaidie kwani hali yake ilibadilika ghafla.Mara wakatokea wanaume watatu waliokuwa na mavazi yaliyowatambulisha kama wafanyakazi wa msalaba mwekundu wakamshika Flaviana na kumuingiza katika lile gari la wagonjwa halafu likawashwa na kuondolewa pale viwanjani huku likipiga king’ora kuashiria kwamba kulikuwamo na mgonjwa ndani yake.Macho ya Flaviana yalipoteza nguvu ya kuona taratibu na mara kukawa giza.Mmoja wa wale jamaa waliokuwamo mle garini akachukua simu na kuwasiliana na mtu Fulani


“ Dr Kigomba kazi imekamilika.Tayari muhusika tunaye na tunataka kulifanya lile zoezi” akasema Yule jamaa


“ Good job,fanyeni kama nilivyowaelekeza halafu mumpeleke hospitali ili atakapozinduka ajikute akiwa kule na asigundue lolote lililotokea.Hakikisheni dawa aliyopakwa kumpoteza fahamu si nyingi sana kiasi cha kuweza kumletea madhara.” akasema Yule mtu wa upande wa pili.

“ Sawa mzee tutafanya kama ulivyoelekeza” akasema Yule jamaa na kukata simu,akafungua mkoba mdogo na kutoa kifaa Fulani mithili ya kompyuta akakiunganisha katika simu ya Flaviana waliyoichukua toka katika pochi yake halafu akabonyeza namba kadhaa katika kile kifaa na kusubiri kwa muda wa dakika kama tano hivi kikawaka taa ya kijani halafu akakitoa kile kifaa na kukirudisha katika kile kisanduku kidogo.

“ Kila kitu tayari.Kuanzia sasa yeyote atakayewasiliana naye tutasikia kila watakachokiongea.” Akasema Yule jamaa na kisha safari ikaendelea kuelekea hospitali


******


Saa tano za mchana Mathew na Anitha walirejea nyumbani wakitokea uwanja wa ndege kuwasindikiza Dr Michael na familia yake ambao waliofanikiwa kupata ndege iliyokuwa ikielekea Nairobi na kutokana na mambo yaliyowakuta ,hawakutaka kuendelea kupoteza muda tena hapa nchini hivyo wakaamua kuitumia nafasi hiyo kuondoka.


“Whats next Mathew? Akauliza Anitha wakati wakiingia ndani

“Kwa sasa baada ya kumaliza ile kazi ya Elibariki tunarejea katika shughuli yetu ya msingi ambayo ni kuchunguza kifo cha Edson” akasema Mathew ,Anitha aliyekuwa dereva akasimamisha gari wakashuka na kumkuta Noah amekaa sebuleni na wote wakaelekea katika chumba ambacho hukitumia kwa majadiliano ya kazi.


“Tunaendelea na zoezi letu.” Akasema Mathew

“Tunaendelea na kazi yetu ya kumtafuta muuaji wa Edson.Ile kazi ya kufanya uchunguzi wa kilichosababisha kifo cha Dr Flora iliingilia kati kati na kwa kuwa tumeimaliza basi tuko huru kuendelea na kazi yetu ya awali. Kabla ya kuingia katika kazi ile iliyojitokeza ,tulitakiwa kuchunguza mahusiano yaliyopo kati ya Peniela na Team SC41. Kama Peniela naye ni Team SC41 basi tutakuwa na uhakika kwamba Edson aliuliwa na Team SC 41 na Peniela atakuwa akifahamu sababu ya ya kifo chake .” akasema Mathew


“ Nakubaliana nawe Mathew kwamba kunaweza kuwa na mahusiano kati ya Peniala na Team, Sc 41 au hata Peniela mwenyewe akawa ni mmoja wao lakini ninachojiuliza ni kwamba kama Peniela ni mwenzao kwa nini basi wamuache ahusishwe na kesi ile kubwa ya mauaji ya Edson na kunusurika kufungwa? Kwa nini wamuache mwenzao ateseke gerezani kwa karibu mwaka mzima? Jambo hili ilinanipa shaka kidogo “ akasema Anitha.

“Hata mimi wakati mwingine nimekuwa nikijiuliza swali kama hilo unalojiuliza wewe Anitha.Inakuwa ni vigumu kuingia akilini kwamba Team Sc 41 wanaweza wakafanya mauaji halafu wakamuacha mmoja wa watu wao abebe mzigo ule wa kesi.Ninavyowafahamu Team SC 41 hufanya mambo yao kwa siri kubwa kwa hiyo kumuacha mwenzao akashikiliwa na vyombo vya dola ni kujihatarisha hata wao wenyewe na ndiyo maana hata matibabu ya John Mwaulaya yalikuwa ya siri mno na walipogundua kwamba tunamfuatilia wakamuhamisha haraka mno.Hivi ndivyo Team SC41 wanavyofanya kazi zao.Hiki ni kikosi ambacho kinafanya kazi zake kwa siri kubwa sana.” Akasema Mathew akainma akafikir kidogo na kusema

“ Kuna wazo limenijia,yawezekana kuna watu waliomuua Edson na Peniela ambaye kwa wakati huo alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Edson akajikuta amenaswa katika mtego.Kama ni hivyo ni nani basi waliomuua Edson na kumtupia Peniela mzigo wa kesi ile ya mauaji? Kuna ulazima wa kumfahamu zaidi Peniela.Kuna kitu tunaweza tukakipata toka kwake” akasema Mathew

“ Kuna zile kamera kipepeo ulizozitega nyumbani kwa Penny zinaweza zikawa na msaada mkubwa sana kwetu.Zinaweza kutusaidia kufahamu kuhusu nyendo za Penny na ni akina nani anaohusiana nao” akasema Anitha


“ Ni kweli Anitha lakini hatutazitegemea kamera tu,lazima twende ndani zaidi.Lazima tumfahamu Peniela kiundani na katika hilo tutamtumia Jaji Elibariki.Naomba niwaweke wazi kwamba Jaji Elibariki na Peniela wana mahusiano ya siri ya kimapenzi.Hilo alinihakikishia Elibariki mwenyewe.Kwa hiyo basi tukitaka kumfahamu Peniela tunatakiwa tumtumie Elibariki.” Akasema Mathew na kuchukua simu yake akampigia Elibariki


“ Hallow Elibariki,” akasema Mathew baada ya Jaji Elibariki kupokea simu


“ Elibariki samahani kwa kukusumbua.”

“ Bila samahani Mathew.Kuna taarifa gani mpya?

“ Hakuna taarifa mpya ila ninahitaji kukuona.Kuna jambo Fulani nataka tuongee kuhusiana na Peniela.”


“ Ok Mathew nitafika baadae kidogo ,kwa sasa niko hapa viwanja vya Ukombozi kuna shughuli ya kuuaga mwili wa Dr Flora.Mara tu shughuli zitakapomalizika hapa nitakuja hapo mara moja” akasema Elibariki .Baada ya kumaliza kuongea na Elibariki simuni,Mathew akawageukia wenzake


“ Nilimtaka Elvis afike hapa ili tuonge naye kuhusiana na suala hili lakini hataweza kufika kwa sasa kwani wako katika shughuli ya kuuaga mwili wa Dr Flora.Lakini atafika baadae baada ya shughuli ile kumalizika”


“ What about Jason? Hatuwezi kumtumia yeye? Jason na Jaji Elibariki ni marafiki na wote wako pamoja katika jambo hili.” Akashauri Anitha


“ Ninadhani ingefaa zaidi endapo tutamtumia El………………”kabla hajamaliza sentensi yake simu yake ikaita.Alikuwa ni Eva.


“ Hallow Eva” akasema Mathew

“ Mathew samahani kwa usumbufu lakini naomba msaada wako”


“ Kuna tatizo gani Eva?


“ Mathew , I guess I’m in trouble”

“ Eva kuna tatizo gani? akauliza Mathew


“ Kuna watu wananifuatilia .”


“ Wanakufuatilia?!

“Ndiyo.Wamekuwa wakinifuatilia toka nilipotoka nyumbani na sijui lengo lao ni nini kwangu.Nimejaribu kuzunguka mitaa kadhaa ili nihakikishe kama ni kweli wananifuata mimi lakini ni kweli wananifuatilia kwani kila nikisimama nao husimama nikianza safari nao huanza.”

“ Unawafahamu watu hao? Akauliza Mathew

“ Hapana Mathew siwafahamu watu hao ni akina nani na nini lengo lao kwangu.Please Mathew help me I dont know what to do.Nina hakika watu hawa wana lengo baya nami”


“ Ok Eva.Uko wapi mida hii?

“ Nimeishika hii barabara ya Jakaya ninaelekea baharini kuingia katika barabara ya ile ya majimaji Drive.”

“ Ok fanya hivi,ukifika pale kwenye mzunguko karibu na hoteli ya Panda Ocean view,ifuate barabara inayoeeleka chuo cha utalii ,kabla hujafika pale chuo cha utalii ,kuna jengo kubwa la maegesho limefunguliwa hivi karibuni maarufu kama maegesho ya mchina.Ingia ndani ya jengo lile hadi ghorofa ya juu kabisa.Mimi najitahidi kufika pale ndani ya kipindi kifupi.Ukifika kabla sijafika nipigie simu unitaarifu.” Akasema Mathew


“ Ahsante Mathew.Samahani lakini kwa kukusumbua”


“ Usijali Eva.Fanya kama nilivyokuelekeza” akasema Mathew na kukata simu

“ Kuna tatizo lingine limetokea.Kuna watu wanamfuatilia Eva.Unajua Eva ndiye aliyetusaidia mpaka tukampata Kanali Adolf kwa hiyo lazima tumsaidie awapo matatizoni.” Akasema Mathew


“ Eva ni nani? Akauliza Noah


“ Hakuna muda wa maswali Noah.Lazima tuwahi kumsaidia Eva.Anitha jiandae tuondoke,Noah utaendelea kubaki hapa hadi tutakapohakikisha umepona jeraha lako” akasema Mathew na kukimbia kuelekea chumbani kwake akakusanya baadhi ya vifaa vyake vya kazi na kutoka.Anitha naye alikuwa tayari,ili kuwahi ikawalazimu kupanda piki piki .Mara chache sana Mathew hutumia pikipiki ili kuepukana na msongamano mkubwa wa magari jijini Dar.


“ Nakumbuka Eva aliniomba nimsaidie kumsaka msichana aliyetekwa na kufichwa mahala kusikojulikana.Nani waliomteka msichana huyo na kwa nini ? Je ni hawa wanaomfuatilia hivi sasa ndio hao waliomteka huyu msichana? Hapa inaonekana kuna kazi nyingine inaweza kujitokeza.Ngoja kwanza tuwafahamu watu hawa wanaomfuatilia na tujue nini wanakitaka kwake” akawaza Mathew wakiwa katika mwendo mkali kuwahi mahala walikopanga wakutane na Eva


*******


Nyumbani kwa John Mwaulaya kulikuwa kimya sana tofauti na ilivyozoeleka.Ni watu wawili tu walioonekana pale nyumbani kwa John.Kijana mwenye taaluma ya udaktari ambaye amekuwa akimtibu John na Josh mlinzi wa siku nyingi wa John Mwaulaya


“ Leo kuna nini hapa mbona kumekuwa kimya sana? Siku zote kabla hawajaelekea katika kazi zao vijana wote hupita hapa kunijilia hali lakini leo imekuwa tofauti,sijawaona kabisa vijana,wako wapi? Laiti ningekuwa na uwezo wa kuinuka na kwenda kujua nini kinaendelea huko nje,manake hata Osmund leo sijamuona toka nilipoamka” akawaza John halafu akanyoosha mkono na kubonyeza kitufe cheusi chini ya kitanda chake na mlango ukafunguliwa haraka akaingia Desmond kijana mwenye taaluma ya udaktari ambaye ndiye amekuwa akimuuguza John .

“ Desmond,vijana wote wako wapi ? Sijawaona wote toka asubuhi.” Akauliza John

“Mzee,vijana leo hawapo,niko mimi na Josh pekee.Wengine wote wametawanyika”

“ Wamekwenda wapi? Akauliza John kwa sauti dhaifu


“ Kuna matatizo yalitokea jana”

“ Matatizo gani? Tafadhali naomba unieleze”

“Mzee nadhani si wakati muafaka kwa wewe kufahamishwa kuhusiana na mambo haya kutokana na afya yako.Endelea kulala upumzike.Mambo yote yanashughulikiwa kikamilifu “

“Desmond,nimelala hapa kitandani ninaumwa sina nguvu za kuweza kufanya jambo kubwa lakini kichwa changu bado kina uwezo wake mkubwa wa kufikiri na kufanya kazi sawasawa.Ninafahamu mambo mengi sana kuliko yeyote katika Team Sc41 kwa hiyo tafadhali naomba unieleze ni kitu gani kimetokea?

Desmond akamtazama John Mwaulaya kana kwamba anaogopa kumweleza kile kilichotokea lakini baada ya tafakari ndogo akaamua kumweleza

“ Kuna shambulio lilitokea jana usiku na vijana wetu sita wakauawa”


“ What ?! John akastuka


“Vijana wetu sita waliuawa katika shambulio jana usiku.Leo hii watu wote wametawanyika wanakwenda kuwazika katika sehemu mbali mbali ndiyo maana umeona nyumba iko kimya leo” akasema Desmond


“ Kwa nini Ossy hakunieleza jambo lolote kuhusiana na suala hili? Nadhani ni kwa sababu niko kitandani na siwezi kufanya lolote.Alikosea sana ,mimi nina uwezo mkubwa wa kuwaongoza hata kama niko kitandani” akawaza John.


“ Ni akina nani waliofanya shambulio hilo na kusababisha vijana wetu wote hao kuuawa? Akauliza John

“ Bado haijafahamika ni akina nani lakini watu hao walikwenda kumkomboa mke wa daktari aliyekuwa ametekwa ili kumshinikiza daktari huyo akufanyie upasuaji.”

“ Kwa nini Osmund alifanya hivi? Hakupaswa kufanya hivi hata kidogo.Team SC41 si watekaji wa watu hata simu moja na jukumu letu ni kushughulika na maslahi ya serikali ya marekani tu na si kuingia katika suala la utekaji.Hili ni kosa kubwa alilolifanya na kwa nini hakunieleza mapema ili nimpe ushauri? Akajiuliza John.Pamoja na kuumwa lakini alionekana wazi kuchukizwa na kitendo cha Osmund kuamrisha kutekwa kwa mke wa Dr Michael.

“Desmond naomba uniitie Josh.” Akasema John Mwaulaya.Desmond akatoka na kwenda kumuita Joseph kijana mlinzi wa John wa muda mrefu.


“ Josh kuna jambo nataka nikueleze” akasema John Mwaulaya


“ Nakusikiliza mzee” akajibu Josh kwa adabu


“ Mimi kwa sasa ni mgonjwa lakini nina hakika nitapona na kurejea katika hali yangu ya kawaida.Bado nina matumaini hayo na Mungu ananisaidia hali yangu si mbaya sana japokuwa kuna watu ambao wamekuwa wakinidharau kwa hali yangu hii ,wakitegemea kwamba ninaweza kufariki muda wowote.They are all wrong.Wataanza kufa wao na mimi nitabaki.Anyway tuachane na hayo.Kuna kazi nataka nikupe na nimekuchagua wewe kama kijana wangu mtiifu sana na ninayekuamini.Katika vijana wote ndani ya Team SC41 ni wewe pekee ninayekuamini.Uko tayari kwa kazi nitakayokupatia? Akauliza John

“ Niko tayari mzee” akasema Josh


“ Ok nashukuru kwa hilo.Kuna mtu ambaye anatumwa kutoka makao makuu marekani kwa ajili ya kuja kunichunguza ugonjwa wangu.Ki ukweli ni kwamba mtu huyu haji kwa dhumuni la kunichunguza ugonjwa wangu,bali anakuja kuniua.Dr Burke is a devil.Nimemtahadharisha Osmund kuhusu jambo hili lakini haonekani kunielewa.I want you to stop him.Stop Dr Burke for me” akasema John.Josh akatafakari kidogo na kusema


“ Unataka nimfanye nini Dr Burke? Akauliza Josh.John akamtazama kwa muda kidogo kisha akasema


“Kill him”


“Mzee niko tayari kuifanya kazi hiyo lakini kuna tatizo kidogo hapa.Ni namna ya kupata taarifa za kuhusiana ujio wa Dr Burke.Kila kitu anakifahamu Osmund pekee.”akasema Josh


“ Usijali kuhusu hilo.Nitakupatia kadi ya kuufungulia mlango wa ofisi ya Osmund pamoja na namba za siri ambazo zitakuwezesha kuingia katika kompyuta yake na utafahamu kila kitu kuhusiana na Dr Burke” akasema John na kumuelekeza afungue kasiki lililokuwa ukutani akampatia kadi maalum ya kufungulia mlango wa ofisi ya Osmund pamoja na Josh namba za siri ambazo angezitumia katika kuingia katika kompyuta ya Osmund.

“ Mzee nashukuru sana kwa kuniamini.Nitafanya kama ulivyoniagiza.” akasema Josh na kutoka

“ Osmund alikosea sana kunidharau na kuamini kwamba sina uwezo wa kufanya chochote kwa sababu tu niko kitandani na sina nguvu za kutembea lakini alisahau kwamba akili yangu bado ina nguvu sana na ninaweza kufanya mambo makubwa tofauti na anavyofikiri.Nilimweleza Ossy kuhusu Dr Burke lakini hajanielewa.Alisahau kwamba pamoja na kwamba ninaumwa ,mimi ndiye niliyeanzisha Team SC 41 na bado kuna vijana wengi wanaoendelea kunitii.” akawaza John na sura ya Dr Burke ikamjia .

“Dr Burke !!..akasema kwa sauti ndogo na kumbukumbu zikamrejesha mbali sana

“ I killed his father.Dr Burke aliapa kulipa kisasi kwa wote waliohusika katika kifo cha baba yake” akawaza John na kumbu kumbu zikamrejesha jijini Washington DC


WASHINGTON DC


1988


Gari la kifahari linafunguliwa geti na kuingia katika jengo moja kubwa na la kupendeza.Baada ya kuegeshwa kijana mmoja aliyekuwa amevalia suti nzuri nyeusi akalisogele gari lile na kuufungua mlango na kijana mmoja mtanashati aliyevalia nadhifu akashuka toka ndani ya ile gari


“ This way Sir” kijana Yule aliyeufungua mlango akamuelekeza kijana Yule aliyeshuka garini ka adabu.Wakaingia ndani ya lile jengo na kulifuata varanda moja refu hadi katika mlango mmoja wa kioo,akaufungua kisha wakaingia ndani,na kuingia tena katika chumba kingine ambamo kulikuwa na watu watano.Wote walionekana kuwa walikuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa Yule kijana .


“John Mwaulaya !! akasema mmoja wa wale wazee na kuinuka akamkubatia John kwa furaha kubwa.

“ Karibu sana John.” Wale wazee wengine nao wakamsalimu John kwa furaha kubwa.

“ nashukuruni sana” akasema John na bila kupoteza muda wakaanza kikao


“ John tumekuita hapa kuna kazi ambayo unatakiwa uitekeleze mara moja.Kama unavyofahamu kwamba Team SC41 inafanya kazi kwa siri kubwa kwa ajili ya kuyalinda maslahi ya Marekani katika afrika ya mashariki.Hata ndani ya serikali ya Marekani ni watu wachache sana wanaofahamu kuhusiana na suala hili.Kuna Seneta mmoja anaita Joe Burke kutoka chama cha Republican,huyu amepata taarifa za kuwapo kwa Team SC41 kwa hiyo kwa sababu zake za kisiasa anataka kuja kuliweka wazi suala hili kwa raia wa Marekani.Najua wamarekani wengi hawatafurahishwa kabisa na suala hili na ni suala linaloweza kuleta mgawanyiko mkubwa kwa raia wa marekani.Hatutaki suala hili lifahamike.Hatutaki Team SC41 ijulikane” Akasema Profesa Edward McNill .Akatulia akamuangalia John halafu akaendelea

“ Hivi tunavyoongea Joe Burke amekwenda afrika mashariki kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa vyama vya upinzani ili waweze kulipinga suala hili kwa kuanzisha maandamano makubwa.Kwa taarifa tulizonazo tayari amekwisha zungumza na kiongozi wa chama kikubwa cha upinzani nchini Tanzania ndugu Elisante mkulwe na mazungumzo yao yanaendelea na siku ya jumamosi anatarajiwa kuelekea nchini Kenya kuzungumza na viongozi wa upinzani wa kule na kisha ataelekea Uganda ili kuwasha wishi viongozi hawa waweze kulianika suala hili kwa pamoja.Endapo jambo hili litafanikiwa basi litampandisha sana kisiasa seneta huyu ambaye anatajwa sana katika watu wanaopewa nafasi kubwa ya kuwania urais wa Marekani hapo baadae.Ili kulizima jambo hili,seneta Joe Burke na viongozi wa upinzani ambao tayari amekwisha ongea nao lazima wote wauawe.Hilo ndilo jambo kuu tulilokuitia hapa “ akasema Edward McNill na kuifungua droo yake akatoa picha mbili.Moja ikiwa ya seneta Joe na nyingine ya Elisante Mkulwe akampatia John.

John Mwaulaya akafumba macho baada ya kumbu kumbu ile kumjia


“ Ubongo wangu umejaa kumbu kumbu za mauaji niliyowahi kuyafanya huko nyuma.Kumbu kumbu hizi zinanjia kama jinamisi na kunitesa mno” akawaza John


******


Mathew na Anitha waliwasili katika jengo lililojengwa maalum kwa maegesho ,maarufu kama maegesho ya mchina kutokana na jengo hili kumilikiwa na raia wa china.Mathew akatoa simu na kumpigia Eva 

“ Hallow Eva,umefika wapi?

“ Ninakaribia kufika katika maegesho ya mchina,niko hapa katika hospitali ya macho”

“ Ok sisi tayari tumekwisha fika.Imetulazimu kutumia piki piki ili kuwahi kufika kwa sababu ya foleni kubwa.Ukifika pitiliza moja kwa moja ndani hadi juu halafu sisi tutashughulika nagg wale jamaa wanaokufuatilia” akasema Mathew na kukata simu

Mathew na Anitha waliendelea kusubiri pale nje ya jengo lile na baada ya dakika kumi na mbili gari moja likawasha endiketa kuashiria kwamba linakata kona kuingia katika jengo lile la maegesho,na mara simu ya Mathew ikaita.Alikuwa ni Eva


“ Mathew ninaingia sasa katika jengo,gari yangu umeiona? Ninatumia hii BMW nyekundu”

“ Nimekuona Eva.Jamaa wao wanatumia gari gani?


“ Wanatumia Harrier yenye rangi nyeusi”

“ Ok Good ,Endelea kwenda mpaka juu kabisa.UKifika egesha gari na utoke garini ujifiche mahala ili tujue lengo lao ni nini” akasema Mathew na kukata simu.Gari la Eva likaingia ndani ya jengo lile na baada ya dakika mbili Toyota Harrier lenye rangi nyeusi nalo likakata kona kuingia ndani ya jengo lile.



“ Jamaa wenyewe ni hawa hapa.Its show time” akasema Mathew akaiwasha piki piki yake nao wakaingia ndani ya jengo lile wakiifuata ile gari iliyokuwa ikimfuatilia Eva.


NINI KITATOKEA NDANI YA JENGO HILO? NANI WANAOMFUATILIA EVA? TUKUTANE SEHEMU IJAYO………

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...