SIMULIZI: PENIELA (Season 1 Ep 36)

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA

“Ripoti ya uchunguzi hii hapa.kwa ufupi tu ni kwamba Dr Flora alichomwa dawa iitwayo Encozynes yenye kiambata kijulikanacho kama Spinolin.Dawa hii hutumiwa na watu wenye matatizo ya shinikizo la damu lakini ni kwa kiwango kidogo sana.Mgonjwa akipewa dawa hii kupita kiwango chake basi husababisha kifo ndani ya muda mfupi kutegemea na kiwango alichopewa.Kwa hiyo tunatakiwa tuchunguze ni nani aliyemchoma dawa hiyo na kwa nini alimchoma.Tukimpata mtu aliyemchoma tutakitegua kitendawili hiki”akasema mathew

“ Kwa maana hiyo kuna kila dalili zinazoonyesha kwamba Dr Flora aliuawa kwa kuchomwa kwa makusudi sindano ile .Na hii ni sababu kumekuwa na jitihada kubwa za kutaka kuzuia uchunguzi wa kifo cha Dr Flora usifanyike kwa sababu waliogopa itabainika kwamba aliuawa.” Akasema Jaji Elibariki


ENDELEA……………………


“ Kwa namna jambo hili lilivyotokea na hali halisi ilivyo kuna kila sababu za kunifanya niamini kwamba Dr Flora alichomwa dawa ile kwa makusudi kabisa na aliyemchoma alikuwa na lengo la kumuua.Hebu jiulize ni kwa nini uchunguzi wa kifo cha Dr Flora ulizuiwa na kulikuwa na kila jitihada za kuhakikisha kwamba hakuna uchunguzi unaofanyika? Ni wazi walifahamu kwamba ukifanyika uchunguzi itagundulika kwamba Dr Flora aliuawa.”akasema Mathew

“ kwa hiyo nini kinafuata baada ya hapa? Nimeanza kuogopa Mathew ” akasema jaji Elibariki

“ Kwa upande wangu ,kazi yangu nimeikamilisha.Nilihitajika kupata ukweli wa kilichomuua Dr Flora na tayari nimekwisha upata.Kinachotakiwa hapa ni kuifikisha taarifa hii sehemu husika kwa mheshimiwa rais ili aweze kutumia vyombo vyake vya uchunguzi kulifanyia uchunguzi jambo hili.Nguvu yangu mimi inaishia hapa na kwa kuwa jambo hili limefanyika ndani ya ikulu sina nguvu ya kuweza kuingia mle na kufanya uchunguzi.Mheshimiwa rais ana uwezo mkubwa wa kulichunguza suala hili na kujua ni nani aliyefanya kitendo hiki na kuchukua hatua zipasazo” akasema Mathew

“ Mathew nakushukuru sana kwa msaada wako huu mkubwa.Bila wewe tusingeweza kuupata ukweli huu.Nitafanya utaratibu wa kumkabidhi mheshimiwa rais ripoti hii mapema asubuhi ya leo ili aweze kuchukua hatua zipasazo “ akasema jaji Elibariki

“ Jitahidi Elibariki ripoti hii ifike katika mikono husika ili iweze kufanyiwa kazi “

“ Ahsante sana Mathew” akasema jaji Elibariki .

“ Ok Elibariki ,I need to take some rest now.Utanifahamisha baadae utakapokuwa umemkabidhi taarifa hii mheshimiwa rais”akasema Mathew na kutoka mle chumbani akaelekea katika chumba alichokuwamo Anitha .

“ Anitha ninakwenda kupumzika kidogo,jitahidi nawe ukapumzike baada ya kumaliza kazi zako .Usiku ulikuwa mrefu sana.Mambo mengi yametokea usiku wa kuamkia leo.”

“ Pole sana Mathew.Umechoka sana .Hata mimi ninaenda kupumzika muda si mrefu .Nataka kwanza nishughulikie lile suala la ndege alilo omba Dr Michael” akasema Anitha

“ Ok Anitha.Nilisahau kusema ahsante sana.Bila wewe tusingeweza kufanikiwa zoezi lile la kumuokoa mke wa Dr Michael”akasema Mathew na kutabasamu kisha akaondoka na kwenda katika mlango wa chumba cha Dr Michael akagonga na mlango ukafunguliwa

“ Hallow Mathew” akasema Dr Michael

“ Dr Michael mkeo anaendeleaje?

“ Anaendelea vizuri sana Mathew”

“ Sawa Dr Michael ,mimi ninakwenda kupumzika kidogo .Ninachoweza kusema ni ahsante sana kwa msaada wako mkubwa.Bila wewe tusingeweza kufanikiwa kuufahamu ukweli wa kilichomuua Dr Flora.Kwa sasa mnaweza kuendelea kupumzika wewe na familia yako Anitha anaendelea kufanya utaratibu wa kupata ndege na atakapofanikiwa atawafahamisha.”

“ Ahsante sana pia Mathew.Familia yangu iko salama sasa kwa sababu yako .Bila wewe na timu yako tusingeweza kuwa pamoja tena.Sintokushau katika maisha yangu yote.Lakini kuna jambo moja dogo ninahitaji kukuomba.”

“ Omba chochote Dr Michael”

“ Tutahitaji kwenda nyumbani kwetu kuchukua vitu vyetu muhimu kama vile mavazi,nyaraka za kusafiria n.k kwa hiyo tutahitaji ulinzi”

“Usijali Dr Michael,tutawapeleka nyumbani kuchukua kila kitu mnachokihitaji” akasema Mathew na kuondoka akaelekaa chumbani kwake na kujilaza kitandani

.Picha ya matukio yote yaliyotokea usiku ule ikajirudia kichwani

“ Ulikuwa ni usiku mbaya sana.Damu imemwagika na tumempoteza kanali Adolf.Pamoja na hayo tumefanikiwa kupata kile tulichokuwa tukikihitaji.Tumempata mke wa Dr Michael na tumefanikiwa kufahamu kile kilichomuua Dr Flora.Ngoja niipumzishe akili yangu kidogo kabla ya jua kuchomoza “ akawaza Mathew na kufumba macho na hazikupita dakika tano kijiusingizi kikampitia


*******


Ulikuwa ni usiku mrefu sana kwa Jason.hakuweza kupata usingizi usiku ule kwa mawazo mengi yaliyokijaa kichwa chake.Kubwa lililoisumbua akili yake ni tukio lililotokea nyumbani kwa peniela.Picha ya Jaji Elibariki na peniela wakifanya mapenzi katika sofa sebuleni kwa Peniela ilimtesa sana.Picha nyingine iliyokuwa ikimfanya atetemeke na uogopa kila akiikumbuka ni ile ambayo Elibariki alikuwa amelala chini huku damu nyingi ikimtoka baada ya kumpiga na chupa.

“ Mwili wote unanitetemeka sana kila nikilikumbuka tukio lile.Sijui nimeua! ..akawaza Jason

“ Sijui nini kitatokea endapo nitakuwa nimeua.Sielewi nini kilinitokea hadi nikachukua uamuzi ule wa kumpiga Elibariki na chupa.Nadhani ni hasira zilivuka mipaka ndiyo maana nikaamua kuchukua uamuzi ule” akaendelea kukumbuka .Akaumia sana

“ Katika maisha yangu sijawahi kupigana na mtu yeyote yule jana ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupigana tena na mtu ninayeheshimiana naye sana kama Elibariki.”

Picha ya Elibariki na Peniela ikamrudia tena

“ Sikujua kama Elibariki ni mtu mshenzi namna ile.Ni mtu niliyemuheshimu sana lakini kwa tukio la jana sintomuheshimu kamwe.Siku zote kumbe alikuwa akimtamani Peniela.Kumbe mipango yake yote ya kutaka kumtafuta muuaji wa Edson ni kwa ajili ya kujiweka karibu na Penny.Baada ya kuona juhudi zake za kumpata Peniela zinashindikana akaamua kutumia nguvu.Angejua namna ninavyompenda Peniela katu asingethubutu kufanya vile alivyofanya.” Akainuka na kwenda nje baada ya dakika tatu akarudi tena ndani

“ Natamani nimpigie simu Peniela nifahamu anaendeleaje na nini kilitokea baada ya ugomvi ule.” Akaichukua simu yake na kuzitafuta namba za Peniela akampigia.Simu ya Penny haikuwa ikipatikana.

“ Amezima simu.Inawezekana kukawa na tatizo kubwa lililotokea na ndiyo maana amezima simu yake.Nitamtafuta tena baadae. Sintoweza kukimbia ,kama nitakuwa nimeua basi nitasubiri hapa nije nikamatwe na hatua stahiki zichukuliwe Pamoja na yote bado ninampenda sana Peniela na siku zote ataendelea kuwa ni mwanamkeninayempenda kuliko wote katika hii dunia na kama jaji Elibariki hatakuwa amekufa nitafanya kila linalowezekana mpaka mimi na Penny tuishi pamoja kwani hata yeye mwenyewe amekwisha onyesha kila dalili kamba ananipenda . Ngoja nilale nisubiri kama watakuja askari asubuhi kunikamata kwa mauaji endapo Elibariki atakuwa alifariki baada ya kumpigana ile chupa kichwani.He deserved that” Jason akawaza na kulala kwani macho yalikuwa mazito sana kwa usingizi


******


Kumepambazuka Dar es salaam na kijua tayari kimechomoza.Jaji Elibariki alistuka toka usingizini akatazama saa yake ilipata saa moja na dakika nane.Simu yake ilikuwa imezima haikuwa na chaji.Alihitaji kuwasiliana na mke wake Flaviana akatoka mle chumbani na kuelekea sebuleni ,akamkuta Noah

“Noah,habari za asubuhi ? Unaendeleaje na jeraha? akauliza

“ Habari za asubuhi nzuri,ninaendelea vizuri .Vipi wewe unaendeleaje?

“ Hata mimi ninaendelea vizuri japokuwa nasikia maumivu kwa mbali.Watu wote bado wamelala?

“Ndiyo bado wamelala.Wamechoka sana kwa kazi ya jana usiku”

“ yah ! kazi ya jana haikuwa ndogo.Noah unaweza ukaniazima simu yako nahitaji kumpigia mke wangu simu yangu haina chaji hata kidogo ” akasema Elibariki.Noah akampatia simu yake akaziandika namba za Flaviana akampigia

“ Hallow “ akasema Flaviana

“ Hallow Flaviana ,samahani nimetumia simu nyingine kukupigia simu yangu imekwisha chaji” akasema Elibariki

“Eli,uko wapi? Are you ok? Akauliza Flaviana

“ I’m ok Flaviana.Unaendeleaje?

“ Ninaendelea vizuri sana.Vipi wewe unaendeleaje? Akauliza Flaviana

“ Ninaendelea vizuri pia.Kuna habari gani hapo msibani ?

“ Ratiba imeshatolewa na leo kutakuwa na zoezi la kumuaga mama ambalo litafanyika katika viwanja vya ukombozi ili kuwapa nafasi watu wengi waweze kumuaga.Kesho tutaelekea kijijini kwa mazishi.Vipi kuhusu lile suala umefikia wapi?”

“ Flaviana ninahitaji kuonana nanyi wewe na Anna asubuhi hii .Naomba tukutane pale kwenye mgahawa wa Maria Stella.Utanikuta ninakusubiri pale.Tafadhali kuweni makini sana”

“kwani kuna nini Eli mbona unaniogopesha?

“Ni kuhusiana na lile suala .Kuna mambo ambayo nahitaji kuwafahamisha.” Akasema Elibariki na kukata simu.

“Noah kuna jambo lingine ambalo naomba unisaidie. Nahitaji kufika sehemu fulani asubuhi hii lakini siko na gari langu.Nahitaji kuongea na Mathew ili kama kuna uwezekano aniazime gari lake moja linifikishe sehemu Fulani nikaonane na mke wangu.”

“ Mathew bado anapumzika mida hii lakini usihofu nitakupeleka mimi” akasema Noah

“ Noah utaweza kuendesha gari na maumivu uliyonayo?

“Usijali Elibariki,nitaweza kuendesha.Maumivu ni vitu tulivyovizoea ”akasema Noah na kuinuka wakaingia katika mojawapo ya gari la Mathew wakaondoka na kuelekea moja kwa moja katika mgahawa unaomilikiwa na dada mmoja aitwaye Maria stella.Noah akamuacha Elibariki pale akarejea.Baada ya dakika kama ishirini hivi toka awasili pale mgahawani Flaviana na Anna wakatokea .Walikuja na gari la kukodi.Flaviana akastuka baada ya kumuona mume wake akiwa na jeraha kichwani

“Eli umefanya nini hilo jeraha ? Akauliza

“ Ni katika purukushani za jana.Kulikuwa na kazi nzito”akasema jaji Elibariki.

“Pole sana mpenzi wangu.Najuta ni kwa nini nilisababisha ukaingia katika jambo la hatari kama lile.Usiku kucha wa leo sijaweza kupata usingizi hata kidogo nikifikiria kama utakuwa salama”akasema Flaviana

“ Usihofu mke wangu,ilikuwa ni kazi ya hatari sana lakini namshukuru Mungu imemalizika na niko salama”

“Pole sana shemeji”akasema Anna

“Nimekwisha poa Anna” akasema Jaji Elibariki halafu akafika muhudumu na kuwahudumia supu halafu Flaviana akauliza

“kwa hiyo umelala wapi leo?

“ Ilinilazimu kulala sehemu salama kutokana na hali ilivyokuwa.”akasema

“ Ile kazi haikuwa rahisi lakini nashukuru Mungu imekwisha salama na tayari tumegundua nini kimemuua Dr Flora”

“ Ouh thanks God”akasema Flaviana

“Mmegundua ni nini? akauliza Anna

“ Tulifanikiwa kuingia katika hospitali ile ya jeshi tukaanza kufanya uchunguzi lakini wakati tukiendelea,ukanipigia simu ikatulazimu kuondoka haraka sana lakini tuliondoka na sampuli kadhaa ambazo tulikwenda kuzifanyia uchunguzi katika maabara nyingine.Katika uchunguzi huo ilibainika kwamba Dr Flora alichomwa dawa iitwayo Encozynes ambayo hutumiwa na wagonjwa wa shinikizo la damu.Natumai hata Dr Flora alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu”akasema Mathew

“ Ndiyo alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu kwa muda mrefu”akasema Flaviana

“ Dawa hiyo ina kiambata kiitwacho Spinolin ambacho huweza kusababisha madhara kwa mgonjwa endapo itatumika kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana dawa hii hutumika katika kiwango kidogo sana.”akanyamza kidogo halafu akaendelea

“ Vipimo vinaonyesha kwamba Dr Flora alichomwa kiasi kikubwa cha dawa hii hatari na hivyo kusababisha kifo chake ghafla”

Anna akainama akashindwa kuyazuia machozi kumtoka.Flaviana naye michirizi ya machozi ikaonekana mashavuni pake.

“Ladies please not now.Tafadhali msianze kuangua kilio humu mgahawani ”Jaji Elibariki akatoa angalizo

“ They killed my mother”akasema Anna

“ Anna please futa machozi.Huu si wakati wa kulia tena.Ni wakati wa kuutafuta ukweli wa jambo hili”akasema Elibariki.Baada ya Flaviana na mdogo wake kufuta machozi akaendelea

“ Kutokana na majibu haya kuna mambo ambayo lazima tujiulize.Kubwa ni kwa nini uchunguzi wa kifo cha Dr Flora uzuiliwe? Nyote ni mashahidi juhudi kubwa zimefanyika ili kuhakikisha kwamba mwili wa Dr Flora haufanyiwi uchunguzi ili kubaini ni kitu gani kimemuua.Waliokuwa wakifanya juhudi ili jambo hili lifanyike ni wazi walielewa kilichokuwa kinaendelea.Jambo lingine la kujiuliza ni je dawa hii ilichomwa kwa uzembe au mchomaji alidhamiria kufanya alichokifanya? Majibu ya maswali haya ni magumu kwetu sisi kuyafahamu kwa hiyo ripoti hii anatakiwa apewe mheshimiwa rais yeye atatumia vyombo vyake kufanya uchunguzi wa jambo hili na kulipatia jawabu.” Akasema Jaji Elibariki

“ Dr Kigomba lazima atakuwa anajua kuhusu jambo hili”akanong’ona Anna

“ Unasemaje ana? akauliza Elibariki

“Dr Kigomba lazima atakuwa akilifahamu suala hili.Yeye ni katibu wa baba na ndiye niliyemsikia akipiga simu akitoa amri madaktari wanaofanya uchunguzi kwa mwili wa mama wakamatwe haraka sana.Lazima ni yeye atakayekuwa amemuua mama” akasema Anna na macho yake yakaonyesha hasira za wazi.

“Nakubaliana nawe Anna kwamba huyo Dr Kigomba anaweza akawa anahusika katika suala hili lakini lazima jambo hili lichunguzwe kuanzia mzizi wake.Kama ni kweli Dr Flora alichomwa dawa ile kwa makusudi kwa lengo la kuutoa uhai wake basi lazima kutakuwa na watu wengi wanaohusika na suala hili.Dr Kigomba hawezi kuwa peke yake.Unatakiwa ufanyike uchunguzi wa kina ili kuwabaini wote waliohusika katika suala hili aidha kwa uzembe au kwa makusudi. ” Akasema jaji Elibariki.

“ Moyo wangu unakataa kabisa kuhusu ushauri wako Elibariki ,kwa nini suala hili tusilifanye wenyewe na kuubaini ukweli? Akasema Flaviana

“Flaviana ushauri wako ni mzuri na tungeweza kulifanya suala hili sisi wenyewe kama tungeweza lakini hili ni suala kubwa zaidi ya unavyolifikiria.Huu ni uchunguzi wa kifo cha mke wa rais,huyu si mtu mdogo.Kama aliuawa basi ni kwa sababu nzito na kuifahamu sababu hiyo kunahitaji vyombo vya usalama.Kwa hiyo basi naomba ukubali tumuachie mheshimiwa rais suala hili atumie vyombo vyake vya usalama vifanye uchunguzi na kuufahamu ukweli wa jambo hili” akashauri jaji Elibariki.Flaviana akakubaliana na mawazo ya mume wake na bila kupoteza muda wakaingia katika gari na kuelekea moja kwa mojakatika makazi ya rais.

Asubuhi hii katika makazi ya rais kulikuwa na pilika pilika nyingi.Ni siku ya kumuaga mke wa rais Dr Flora .Flaviana hakupoteza muda akaomba kuonana na baba yao kisha wakiambatana na jaji Elibariki wakaingia katika chumba cha maongezi.

“ Pole sana mheshimiwa jaji.Ilikuwa ni ajali? ” Dr Joshua akampa pole jaji Elibariki baada ya kumuona na jeraha kichwani

“ Ahsante sana mheshimiwa rais.Haikuwa ajali bali mkwaruzo mdogo tu,nilijigonga mahala” akasema Jaji Elibariki

“ Flaviana mbona tumeitana asubuhi asubuhi namna hii kuna nini? Akauliza Dr Joshua

“Baba kuna taarifa tunataka kukupatia.Ni kuhusiana na kilichosbabisha kifo cha mama”

“ Ouh Flaviana,nilikwisha kueleza toka jana kwamba nitalifanyia uchunguzi suala hili na hivi tunavyoongea tayari madaktari wako katika uchunguzi.Kabla ya mwili kupelekwa viwanja vya ukombozi kwa kuagwa tayari tutakuwa tumepata majibu nini kilisabisha kifo cha mama yenu.Msihofu wanangu tutafahamu tu muda si mrefu nini kilimuua mama yenu.” Akasema Dr Joshua

“ Baba tayari tunafahamu nini kilimuua mama “

“Mmefahamuje” akauliza Dr Joshua kwa mstuko kidogo

“ Unakumbuka jana nilikufahamisha kwamba nimemuomba mume wangu anisaidie kufanya uchunguzi wa siri?

“Ndiyo nakumbuka”

“ Basi Elibariki na jopo lake walifanikiwa kuufanya uchunguzi huo kwa siri licha ya amri ya kuusimamisha iliyotolewa na ripoti yake ni hii hapa” akasema Flaviana na kumkabidhi Dr Johua bahasha yenye ripoti.

“ Mheshimiwa jaji pole sana kwa misuko suko.Jana alinifuata mwenzako akiwa na mdogo wake na kunieleza mambo mazito ambayo sikuwa nikiyafahamu.Kwa kuwa ndiyo kwanza niliyasikia ninahitaji muda wa kuyachunguza zaidi na kuubaini ukweli.Ripoti yenu inasemaje? Mmegundua ni kitu gani kilimuua Dr Flora? Akauliza Dr Josha akimuelekezea macho jaji Elibariki

“ Mheshimiwa rais ,uchunguzi tulioufanya unaonyesha kuwapo kwa sumu aina ya Spinolin .Hiki ni kiambata kinachopatikana katika dawa aina ya Encozynes inayotumiwa na watu wenye shinikizo la damu.Dawa hii hutumiwa katika kiwango kidogo sana na endapo ikitumika katika kiwango kikubwa inaweza kusababisha kifo.Uchunguzi unaonyesha kuwapo kwa kiwango kikubwa cha spinolin dalili kwamba Dr Flora alichomwa kiwango kikubwa cha dawa hii na hivyo kusababisha kifo chake.Maelezo ya kitaalamu zaidi namna dawa hiyo inavyofanya kazi yapo ndani ya hiyo bahasha”akasema Jaji Elibariki.Uso wa Dr Joshua ukabadilika .Akamtazama jaji Elibariki kwa muda wa kama sekunde Arobaini hivi halafu akasema

“ Nashukuru sana mheshimiwa jaji.Good job.Taarifa hii imenistua sana na ninaombeni mnipe muda niwezekulifanyia kazi ili kuwabaini wote waliofanya kitendo hiki” akasema Dr Joshua.

“ Baba hiki kitu kilicho wazi kabisa.Watu waliofanya hivi wanajulikana kabisa.Dr Kigomba ndiye aliyetoa amri uchunguzi wa kifo cha mama usifanyike.Anatakiwa akamatwe na awataje wenzake”akasema Anna huku akilia.Dr Joshua akamfuata na kumbembeleza

“ Anna nyamaza usilie.Najua umeumizwa sana kwa jambo hili.Natamani sana ningefanya kama hivyo unavyoshauri nifanye lakini mambo hayaendi namna hiyo.Uchunguzi wa jambo hili ni mkubwa .Naombeni mniachie suala hili nilishughulikie .Nina watu wangu ambao wanaweza wakaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa.Yeyote ambaye amehusika katika suala hili lazima apate adhabu stahili.”akasema Dr Joshua

“ Flaviana na Anna ,tafadhali naombeni mliache suala hili katika mikono ya mzee ili alishughulikie kama alivyoahidi. “ akasema Jaji Elibariki.Flaviana na mdogo wake wakakubali kuliacha suala lile katika mikono ya rais

“ Muda unakwenda kwa kasi,nendeni mkajiandae mtaongozana na msafara kuelekea hospitali kuufuata mwili .” akasema Dr Joshua na wanae wakatoka kwenda kujiandaa.Dr Joshua akabaki chumbani amesimama akiwaza.Halafu akachukua simu na kuzitafuta namba fulani akapiga

“ Hallo Mr president” ikasema sauti ya upande wa pili

“ Dr Kigomba,mambo yamebadilika.Wale jamaa walifanikiwa kufanya uchunguzi na wakagundua kila kitu”

“ What ?!! Dr Kigomba akashangaa

“ Hapa nilipo nimeishika bahasha yenye maelezo ya kuhusiana na kilichomuua Flora.Umefanyika uzembe mkubwa sana na tusipofanya juhudi za haraka kila kitu kitaharibika.”

“ Ok mzee usijali,we’re going to fix this.Hivi tunavyoongea Amos anatengeneza ripoti ya kifo cha Flora.Ikishapatikana ripoti hiyo,ikatae taarifa waliyokuletea,na uwaonyeshe ripoti ya kwetu ambayo itaonekana imetoka hospitali kuu ya taifa na uchunguzi umefanywa na madaktari bingwa.Baada ya hapo tutaangalia namna nyingine ya kufanya”akasema Dr Kigomba

“ Ok good plan.lakini kuna jambo lingine.”

“ Jambo gani mzee?

“ Tunatakiwa tumuondoe Amos katika picha.Yule ni hatari sana kwetu kwani yeye ndiye aliyemchoma Flora sindano ile.”

“ Una maana tumuue?

“ yah.Kuendelea kuwa hai ni jambo la hatari kubwa sana kwetu”

“ Ok nimekuelewa mzee” akasema Dr Kigomba.

‘One more thing”

“Nakusikiliza Mzee’

“ Keep an eye on my daughters.Wanatakiwa wachunguzwe nyendo zao,wanahusiana na nani ,wanaongea na nani na wanaongea nini.Hawa nao wanaweza kuwa ni hatari kubwa sana kwetu.Endapo itaonekana kwamba wanaweza wakasababisha hatari sintakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwaondoa katika picha pia.Mtu mwingine ni jaji Elibariki.Yeye ndiye aliyeshughulikia uchunguzi huu ukafanyika.Huyu ndiye nyoka mwenye sumu kali sana.Huyu naye inatakiwa itafutwe namna ya kumuondoa haraka sana.Tayari anafahamu kilichotokea na hatujui amekwisha mueleza nani .Kabla ya kuanza na Amos,anza kwanza na Jaji Elibariki.“



“ Ok nimekuelewa mzee,nitalifanyia kazi hilo suala “

“ Kigomba ,naomba utambue kwamba hii ni nafasi ya mwisho ninakupa.Please don’t mess up.”

“ I wont mr President” akasema Dr Kigomba na Dr Joshua akakata simu.Alikuwa akiangalia juu ya dari akiwa na mawazo mengi sana.

“ Suala hili linaanza kufuka moshi.Inatubidi kuwahi mapema kuuzima moto ule kabla haujaanza kuwaka na kusambaa .Ukiwaka moto huu hautazimika na utatuunguza wengi.I wont let that happen.kwa gharama zozote zile lazima nihakikishe ninalizima suala hili” akawaza Dr Kigomba na kutoka mle katika chumba maalum cha maongezi ya faragha cha mheshimiwa rais


******


Jiji la Dare s salaam limeamshwa na habari kubwa ya kifo cha kanali Adolf.Karibu magazeti yote yaliandika kuhusiana na habari ile lakini hakuna hata gazeti moja lilioandika habari ya kweli kuhusiana na nini kilisababisha kifo cha kanali Amos.

Akiwa bado kitandani ,Peniela alisikia kitu kama mlio wa simu na alipofumbua macho ni kweli ile simu anayotumia kuwasiliana na rais ilikuwa inaita.

“ Joshua anataka nini asubuhi yote hii?akajiuliza huku akiunyoosha mkono na kuichukua simu ile

“ Hallo Dr Joshua”

“ Hallow Penny.Bado umelala?

“ Bado asubuhi sana Dr Joshua”akasema Penny.Dr Joshua akacheka kidogo na kusema

“ Ok Peniela.Nimekupigia kukutaarifu kwamba leo inafanyika shughuli ya kumuaga mke wangu katika viwanja vya ukombozi na kesho tutamzika kijijini kwao.Nimemkabidhi Kareem jukumu zima la kukuhamisha siku ya leo.Nitawasiliana nawe tena baada ya kurejea kesho kutoka katika mazishi”

“Ahsante sana Dr Joshua.Nakutakia safari njema hapo kesho.Nina hamu sana ya kuongea nawe mambo mengi lakini tutaongea ukisharudi” akasema Peniela

“Usijali malaika wangu ,hata mimi nina mambo mengi sana ya kuongea nawe.Kwa heri kwa sasa”akasema Dr Joshua na kukata simu

Hazikupita hata dakika tano toka akate simu,kengele ya getini ikalia akaamka na kwenda kufungua akakutana na kareem

“ Kareem karibu sana “ akasema Penny na kumkaribisha Kareem ndani

“ Penny ,mheshimiwa rais amenikabidhi mimi kazi ya kuhakikisha leo unahamia katika lile kasri.Nimekuja mapema namna hii nataka tuelekee katika maduka ya fenicha na uchague kila kitu unachokihitaji kiwepo ndani ya ile nyumba .Hutakiwi kuchukua kitu chochote toka huku kwako hata nguo.Kila kitu utanunua kipya..”akasema Kareem.Penny hakujibu kitu akabaki akitabasamu akaelekea chumbani kwake akaoga na kujiandaa kwa ajili ya mizunguko ya siku ile.Alikusanya baadhi ya vitu vyake vidogo vidogo na bila kulisahau kasha alilopewa na John Mwaulaya.

“Hii yote ni katika kuhakikisha kasha hili linakuwa salama.”akawaza huku akilishika kasha lile akalipakia katika sanduku lle kubwa na kulikokota akatoka mle chumbani.Kareem akamsaidia kulibeba sanduku lile hadi katika gari ,Penny akafunga milango yote ya nyumba yake kisha akaingia garini na kuondoka”

“Safari ya kuelekea katika maisha mapya imeanza.” Akawaza akiwa garini.

RAIS WA JAMHURI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DR JOSHUA AMEIPOKEA RIPOTI YA UCHUNGUZI ULIOFANYWA KWA SIRI NA AKINA MATHEW NINI KITAWATOKEA WATOTO WAKE ANNA NA FLAVIANA PAMOJA NA JAJI ELIBARIKI? PENIELA TAYARI AMEHAMIA KATIKA NYUMBA ALIYOPEWA NA DR JOSHUA .MWISHO WA PENIELA SEASON ONE..

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...