PENIELA (Season 1 Ep 12)

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA

Mara tu alipomkumbuka Penny,akatabasamu na kutoa simu yake akazitafuta namba za Penny akapiga lakini bado simu yake haikuwa ikipatikana

“ Ameamua kuizima simu yake,inawezekana hataki usumbufu toka kwa watu.Ametoka katika matatizo makubwa na anahitaji muda wa kukaa mwenyewe atafakari maisha yake bila usumbufu toka kwa watu” akawaza Jaji Elibariki Moja kwa moja alielekea Mandarini Hotel mahala ambako hupenda sana kwenda kupata kifungua kinywa. “ Watu wengi wananishangaa ni kwa nini mtu kama mimi,Jaji wa Mahakam kuu ninakuja kupata kifungua kinywa hotelini? Hawajui Kero nilizonazo katika ndoa yangu.lakini soon mambo yote haya yatakwisha and I’ll be happy again.” Akawaza wakati akiendelea kupata kifungua kinywa. Toka Mandarin hotel,akaelekea ofisini kwake ambako hakukaa sana akatoka akaelekea mahala alikopanga akutane na Mathew.

ENDELEA……………………………..

Dakika kumi baada ya kuwasili Malaika Lounge mahala walikopanga wakutane na Mathew,Jason akawasili, wakasalimiana akavuta kiti na kuketi

“ Jason” akaanzisha mazungumzo Jaji Elibariki

“ kama nilivyokueleza simuni ,nimefikiria sana kuhusiana na jambo tunalotaka kulifanya na kuona ugumu wake .Sisi tumebobea katika masuala ya sheria na hatuna taaluma yoyote ya kufanya uchunguzi.Ni kwa sababu hii nimelazimika kumtafuta Mathew Kwanga” akanyamaza kidogo ,akamtazama Jason na kuendelea.

“ Mathew Kwanga aliwahi kufanya kazi katika idara ya ujasusi ya taifa na aliacha kazi hiyo baada ya familia yake yote kuteketezwa kwa moto.Kwa hivi sasa yeye ni mtu anayekodishwa na mataifa kazi za siri za kiuchunguzi .Ni mtu aliyebobea mno katika kazi hizi .Nina imani atatufanyia kazi nzuri “ akasema Jaji Elibariki

“Umefanya jambo la msingi sana mheshimiwa jaji.Hata mimi nilikuwa nafikiria kukushauri tufanye kitu kama hicho.Sisi peke yetu hatuwezi kulifanikisha jambo hili .Tunahitaji msaada wa mtu mwenye uzoefu wa kutosha na mambo haya.Natumai Mathew ni chaguo sahihi na atakuwa na msaada mkubwa sana kwetu” akasema Jason

“ Exactly !...Thats my point..Mathew ni mtu ambaye tumefahamiana kwa muda refu na sina shaka yoyote na uwezo wake.Ni mtu mwenye uwezo wa hali ya juu sana.By the way how’s Peniela? Akauliza Jaji Elibariki.Jason akaguna kidogo na kusema

“ Siku ya pili sasa hapatikani simuni”

“ May be she needs sometime alone. Unajua ametoka katika matatizo makubwa kwa hiyo yawezekana akahitaji kuituliza akili yake bila bughudha za watu.Let’s give her sometime” akasema Jaji Elibariki na mara Mathew akatokea.Alikuwa ni kijana nadhifu aliyevaa suti nzuri iliyompendeza

“ Hallo gentlemen…” akasema Mathew huku akipeana mikono na akina Jason

“ Mathew kutana na Jason,wakili maarufu sana hapa Tanzania.” Bila kuchelewa Jaji Elibariki akaanza kutoa utambulisho

“ Jason kutana na Mathew Kwanga.Ni rafiki yangu wa siku nyingi na mtu aliyebobea katika masuala ya kiuchunguzi”

Jason na Mathew wakashikana mikono kwa kujuana

“ Mtanisamehe sana ndugu zangu kwa kuchelewa .Nilipatwa na dharura ya ghafla” akasema Mathew

“ Usijali Mathew.Hakuna kilichoharibika.Nadhani umelifanyia kazi lile suala letu” akasema Jason

“ Ndiyo mheshimiwa Jaji.Nimejaribu kutafakari kwa kina kuhusiana na kazi mliyonipa na namna nitakavyoweza kuifanya.Naomba niwaweke wazi kwamba kazi hii si ndogo kama mnavyoifikiria. Edson alikuwa mfanyakazi katika kitengo cha habari Ikulu,huyu si mtu mdogo kama watu wanavyoweza kudhani.Ninashawishika kuamini kwamba lazima aliuawa kwa sababu maalum.Kazi yetu ni kuitafuta sababu hiyo iliyopelekea yeye kuuawa pamoja na watu waliomuua na kesi kumuangukia Peniela.Kazi hii si nyepesi lakini nawaahidi kwamba hakuna yeyote ambaye alikuwa na mkono wake katika mauaji hayo atabaki salama.Nitawatafuta katika kila pembe ya nchi hii na dunia mpaka nihakikishe nimewatia mikononi wale wote waliofanya kitendo hicho cha kinyama na mzigo wote wakamuangushia Penny.” akanyamaza kidogo na kuendelea

“ Kabla hatujaendelea mbele zaidi naomba tukubaliane kwanza kitu kimoja.kazi hii ni ya gharama kubwa.Kabla sijaingiza mguu wangu katika uwanja wa mapambano nahitaji kufahamu kama mtakuwa tayari kwa gharama za shughuli hii japokuwa haitakuwa kubwa kwani ninaifanya tu kwa ajili ya ninyi ndugu zangu lakini sikuwa nataka kufanya kazi yoyote hapa nyumbani.” Akasema Mathew.Jason na Jaji Elibariki wakatazamana na Jason akasema

“ Tuko tayari Mathew.Usihofu kuhusu gharama”

“ Ok Good.Sasa tunaweza kuendelea” akasema Mathew.

“ Katika kazi hii pia nitashirikiana na watu wawili.Wa kwanza ni Anitha Monera na wa pili ni Noah Ikuso.” Akasema Mathew huku akiwapa akina Jason mafaili ya watu hao wayapitie.



“ Anitha Monera ana miaka ishirini na tisa.Ni mtanzania anayeishi nchini Marekani.Huyu ninamuita ni mchawi wa kompyuta. Anaichezea kompyuta kwa kiasi cha kushangaza .Nimekuwa nikimtumia sana katika kila kazi ninayoipata na siwafichi ndugu zangu huyu amekuwa ni msaada mkubwa kwangu na ndiye amenifanya nifanikiwe katika kila kazi ninayopata” akanyamaza kidogo na kuendelea

“ Noah ikuso naye ni mtanzania pia.Ana umri wa miaka thelathini na tatu .Aliwahi kufanya kazi katika idara ya usalama wa taifa .Ni kijana mahiri na hodari katika kazi.Ninao wengi ambao ninaweza kufanya nao kazi hii lakini nimewachagua hawa wawili ambao naamini wanatosha sana kuikamilisha hii kazi kwa umahiri na haraka” akasema Mathew.Jason na jaji Elibariki waliendelea kupitia mafaili ya vijana wale halafu Jason akasema

“ Kwa upande wangu sina kipingamizi chochote.Kama unawaamini vijana hawa kwamba wanaweza kazi basi unaweza kuwatumia”

“ Yah ! ninawaamini sana.Ni mahodari na hawana mchezo katika kazi.” Akasema Mathew,kikapita kimya kifupi akauliza

“ Kuna kitu kimoja bado hamjaniweka wazi.Nina hakika nitawapata watu hawa waliofanya kitendo hiki,lakini je wakipatikana nini kitafuata? Wanashughulikiwa vipi? Au mtawakabidhi katika mikono ya dola?

“ Lengo letu sisi ni kuwafichua na kuwakabidhi katika mikono ya dola.Kitu kikubwa kinachonisukuma mimi na mwenzangu tuwe tayari kugharamia jambo hili ni kuudhihirishai umma wa watanzania kwamba sikufanya maamuzi ya kukurupuka kumuachia huru Peniela.Nataka watu wawe na imani na mahakama kwamba ndicho chombo pekee chenye kutenda haki bila kujali mtu.Hatuna lengo la kulipiza kisasi,bali tukimbaini muuaji tutamfikisha katika mikono husika na sheria itachukua mkondo wake na sisi tutabaki salama.” Akasema Jaji Elibariki

“ Ok sasa nimekuelewa mheshimiwa jaji.usijali watapatikana tu.Kitu kingine ninachohitaji ni kumpata Peniela ili niweze kuongea naye mawili matatu kwani yeye ndiye aliyekutwa eneo la tukio.Nataka niyafahamu mazingira ya tukio namna yalivyokuwa.” akasema Mathew

“ Peniela leo ni siku ya pili simu yake haipatikani na sijui yuko wapi.” Akasema Jason

“ Are you sure she’s ok? Akauliza Mathew

“ Sina hakika sana kwa sababu jana nilikwenda nyumbani kwake lakini getini kulikuwa na makufuli na ilionyesha wazi kwamba hakukuwa na mtu ndani”

“ Ok Vizuri.Wakati tukimsubiri nitaanza uchunguzi wangu kwa Edson.Ninataka mnielekeze mahala alipokuwa akiishi na baada ya hapo mtaendelea na kazi zenu kama kawaida na mimi nitaendelea na kazi yangu,popote nitakapokwama na kuhitaji msaada wenu nitawaambia” akasema Mathew.Wakaendelea na kikao chao na kupeana maelekezo kadhaa halafu Jason na Mathew wakaeleekea mahala alipokuwa akiishi Edson.

“ Umeshawahi kuonana na huyo kijana Edson? Akauliza Mathew wakiwa garni

“ Hapana sijawahi kuonana naye hata mara moja”

“ Umewahi kuingia ndani mwake?

“ Ndiyo nimeingia mara moja tu wakati kesi ikiendelea.Kuna wakati iliilazimu mahakama ihamie hapa kuthibitisha madai ya upande wa mashtaka.”

“ Ok Good.” Akasema Mathew na safari ikaendelea.

Jason akaegesha gari nje ya nyumba aliyokuwa akiishi Edson

“ Ni hapa” akasema.Mathew akaitazama nyumba ile halafu akashuka na kumuomba Jason amsubiri garini.Akaelekea getini akabonyeza kengele ya getini na baada ya dakika moja mlango mdogo wa getini ukafunguliwa akatoka kijana mmoja .

“ Habari yako ndugu”

“ Habari yangu nzuri.Karibu sana.Nikusaidie nini? Akauliza Yule kijana

“ Samahani ndugu yangu.Nimemkuta Edson? Akauliza Mathew

“ Edson?!.. yule kijana akashangaa

“ Ndiyo Edson.”

“ Yawezekana umekosea nyumba.Hakuna Edson anayeishi humu ndani”

“ Yawezekana nimekosea .Ninaishi nje ya nchi na mara ya mwisho nilipokuja huku Tanzania Edson alinileta hapa mahala alipokuwa anaishi na ndiyo maana nimekuja moja kwa moja hapa.Yawezekana nimepotea nyumba lakini kumbukumbu zangu zinaniambia ni hapa hapa.” Akasema Mathew

“ Anafanya kazi wapi huyo Edson? Pengine naweza kukusaidia kumtafuta “ akasema Yule kijana

“ Edson anafanya kazi ikulu” akajibu Mathew

Yule kijana akamtazama Mathew kwa mshangao kidogo na kuuliza

“ Mara ya mwisho mliwasiliana lini ?

“ Nina zaidi ya mwaka sasa sijawasiliana naye”

“ Dah ! pole sana kaka.Kama unamuongelea huyo kijana aliyekuwa akifanya kazi ikulu ni kweli alikuwa akiishi hapa lakini inasemekena aliuawa na ndiyo maana wazazi wake wakaamua kuiuza nyumba hii”

Mathew akaonyesha mstuko mkubwa.

“ Dah sikuwa na taarifa hizo.Ahsante sana kwa taarifa hizo ndugu yangu.Nitakwenda kuwapa pole wazazi wake” akasema Mathew na kurejea garini.

“ Wazazi wa Edson wamekwisha iuza nyumba hii .Kwa maana hiyo vitu vyote vya Edson viliondolewa hapa na nina hakika vilipelekwa nyumbani kwa wazazi wake.Nahitaji kukagua vitu vyake.Nahitaji kuikagua simu aliyokuwa akiitumia na kompyuta yake kama bado vipo.“ akasema Mathew

“ Kama ni hivyo itatulazimu kwenda nyumbani kwa wazazi wake na kuonana nao na kuwaomba kupitia vitu hivyo” akasema Jason

“ Hiyo ndiyo hatua inayofuata.Unafahamu mahala wanakoishi wazazi wake?” Akasema Mathew.

“ Ndiyo ninapafahamu.Baba yake ni mtu maarufu sana hapa mjini..” akasema Jason..

“ Ok.Kama tukionana na wazazi wa Edson tukaongea nao tunaweza kupata japo sehemu ya kuanzia.” Akasema Mathew.

TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO………

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...