PENIELA (Season 1 Ep 18)

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA

“ Walikuwa wakiwasiliana kwa siri na hata vifo vyao vimetokea kwa kufuatana.Mathew kuna kitu hapa si bure.Kama walikuwa ni marafiki kuna jambo lazima watakuwa wakilifahamu kwa pamoja au wakilificha na ndiyo maana hata mawasiliano yao yalikuwa ya siri kubwa na hawakutaka mtu mwingine yeyote Yule afahamu kama walikuwa wakiwasiliana.Siri hiyo waliyokuwa wakiificha ndiyo iliyowagharimu maisha yao.” Akasema Anitha

“ Anitha inatosha kwa leo.Tupumzike na kesho tuanze kazi rasmi.Tutaanza kazi kwa kutafuta taarifa za Brigita Samini .Anaonekana ni mtu muhimu sana katika suala hili” akasema Mathew.Anitha akamtazama na kutabasamu halafu akazima kompyuta zake

“ Uko sahihi Mathew.Leo imekuwa ni siku ndefu sana.Tupumzike ili kesho tuanze kazi “ akasema Anitha

ENDELEA…………………………..

Kumekucha Dar es salaam,saa tatu za asubuhi Iliwakuta Mathew na Anitha nje ya hoteli ya kitalii ya Potina Palace.Waliegesha gari na kushuka wakaingia hotelini na moja kwa moja wakaelekea mapokezi ambako walimkuta mwanadada mmoja mrembo wakajitambulisha kama rafiki wa Brigita Samini aliyekuwa akifanya kazi pale hotelini.Yule mwanadada wa mapokezi akashangaa kidogo na kuuliza

“ Hamkuwa na mawasiliano naye au ndugu zake?

“ Sisi tunaishi Marekani na kwa muda msrefu kidogo hatukuwa tumewasiliana naye.Mara ya mwisho tulipowasiliana naye alituelekeza kwamba anafanya kazi hapa.” Akasema Mathew

“ Poleni sana ndugu zangu.Brigita hatuko naye tena,alifariki dunia yapata mwaka mmoja sasa umepita” akasema yule dada ambaye kitambulisho cha kazi alichokivaa kilionyesha anaita Stella manana .Mathew na Anitha wakaonyesha mstuko ili kumfanya Yule dada asiwe na wasi wasi wowote kuhusu wao.

“ Nini ilikuwa sababu ya kifo chake? Akauliza Anitha

“ Mtungi wa gesi ulilipuka na kusababisha nyumba yao iteketee kwa moto.Hakuna hata mtu mmoja aliyetoka hai.Ilikuwa ni ajali mbaya sana.Brigita alikuwa ni meneja wetu na mtu mwenye roho nzuri sana na kila mtu hapa alimpenda “

Kikapita kimya cha sekunde kadhaa Mathew akauliza

“ Kuna mtu yeyote ambaye alikuwa ni mtu wake wa karibu sana ili aweze kutuelekeza kwa ndugu zake tukawape pole? Akauliza Mathew

“ Brigita alikuwa na marafiki wengi na kila mtu alikuwa ni rafiki yake lakini kuna mmoja ambaye alikuwa ni rafiki yake mkubwa anaitwa Subira.Kwa sasa hayupo hapa hotelini anasomea shahada ya hoteli pale Ikandala University.Kama mnahitaji taarifa za kina kuhusiana na Brigita mtafuteni huyo Subira kwani ni yeye anayewafahamu hadi ndugu zake “ akasema Yule dada na kuwapatia namba za simu za Subira wakaagana Mathew na Anitha wakarejea katika gari lao.

“Mpigie simu Subira tufahamu yuko wapi” akasema Mathew.Anitha akaziandika zile namba katika simu yake na kupiga.Simu ikaita na kukatika,akapiga tena ikaita lakini haikupokelewa

“ Simu yake inaita tu lakini haipokelewi” akasema Anitha

“ Jaribu tena kumpigia.Isipopokelewa tutamfuata pale pale chuoni kwao” akasema Mathew ,Anitha akapiga tena na safari hi ikapokelewa

“ Hallow !..Ikasema sauti ya mwanadada upande wa pili

“ Hallow naongea na nani? Akasema Anitha

“ Unaongea na Subira Abdul.Wewe ni nani mwenzangu?

“ Ninaitwa Anitha”

“ Nikusaidie nini Anitha? Akauliza Subira ambaye alikuwa na sauti ya upole

“ Subira ninahitaji kukuona.Nina maongezi nawe kidogo” akasema Anitha

“ Una maongezi na mimi? Subira akashangaa

“ Ndiyo Subira.Nahitaji sana kukuona”

“ Ni maongezi kuhusu nini? Halafu mbona sikufahamu?

“ Usihofu Subira.Hata mimi sikufahamu nimepewa namba zako za simu pale Potina Palace ulipokuwa ukifanyakazi kabla ya kuanza kusoma.”

“ Ok Unataka tuongee jambo gani?

“ Mimi ni rafiki wa siku nyingi wa Brigita Samini ambaye nimeelezwa kwamba wewe ulikuwa na ukaribu naye mkubwa .Ninaishi Marekani kwa sasa na nimekuja kwa mapumziko mafupi.Nimeenda kumtembelea Brigita mahala nilikomuacha akifanya kazi kipindi cha kama mwaka mmoja uliopita nikaambiwa kwamba alifariki dunia katika ajali ya moto.Nimestuka sana .Ninataka kufahamu mengi kuhusiana na kifo hicho na hata kuwafahamu ndugu zake ili nikatoe pole.Nimeelekezwa kwako kwamba unaweza ukanisaidia kwa hilo Subira” akasema Anitha

“ Kwa sasa uko wapi? Subira akauliza

“ Kwa sasa ninaondoka hapa Potina Palace.wewe uko wapi?

“ Mimi niko chuoni hapa Ikandala University.Ninamalizia kipindi cha mwisho .Unaweza ukaja kunisubiri hapa chuoni nimalize kipindi?

“ Usijali Subira ninakuja” akasema Anitha na kukata simu

“ Yuko chuoni anamalizia kipindi,anasema tumfuate tukamsubiri” Anitha akamwambia Mathew

Wakiwa njiani, kuelekea chuoni,Mathew akawasiliana na Jason kutaka kujua kama Penny amekwisha rejea lakini mpaka muda huo Jason hakuwa na taarifa zozote za kumuhusu Penny

“ Penny atakuwa amekwenda wapi? Mpaka leo hajaonekana na hajulikani yuko wapi” akasema Mathew

“ Unahisi anaweza kuwa amepatwa na tatizo? Akauliza Anitha

“ Sina hakika sana lakini hata kama hajapatwa na tatizo bado hayuko salama.Bado nawafikiria watu wale walioingia ndani ya nyumba yake jana na kuweka kamera za siri ni akina nani na wana lengo gani kwa Penny.Nashawishika kutaka kumfahamu vizuri zaidi Penny.” Akasema Mathew



“ Have you met her? Akauliza Anitha huku akiendelea kucheza na kompyuta yake

“ No I haven’t” akajibu Mathew

Waliendelea na safari hadi walipofika Ikandala University,Anitha akamtumia Ujumbe Subira kumfahamisha kwamba tayari wamekwisha fika wako nje wanamsubiri.Baada ya dakika ishirini Subira akatoka.Hakuwa akimfahamu Anitha hivyo ikamlazimu kumpigia simu ,Anitha akamuelekeza mahala walipo akawafuata

“ Habari yako Subira” akasema Anitha.Subira alionyesha hofu kidogo alipogundua kwamba Anitha hakuwa peke yake bali alikuwa na Mathew

“ Habari yangu nzuri.habari zenu?

“ Habari zetu nzuri.Pole na masomo”

“ Ahsante” akajibu Subira

“ Subira huyu hapa ni mwenzangu anaitwa Mathew kwa hiyo naomba usiwe na hofu.” Anitha akafanya utambulisho kwani alimuona Subira akiingiwa na uoga.

“ Subira hatutaki kuchukua muda wako mwingi kwani najua una shughuli nyingi za kufanya.Tunaweza kupata sehemu hapa karibu tukakaa na kuongea japo kwa dakika chache? Akauliza Anitha

“ Kuna hoteli pale karibu tunaweza kwenda kukaa tukaongea” akajibu Subira halafu wakaongozana kuelekea katika hoteli iliyokuwa kandoni mwa chuo.

“ Subira kama tulivyoongea simuni,mimi ni rafiki wa siku nyingi wa Brigita.Kwa sasa ninaishi Marekani na nimerudi nchini kwa mapumziko mafupi.Ni muda umepita sijawasiliana naye na mara ya mwisho kuwasiliana naye alinielekeza mahala anapofanyia kazi nikamwambia kwamba nikija Tanzania nitamtembelea.Nimefika kumtembelea mahala alikonielekeza anafanya kazi nikakutana na taarifa hizi za kustusha za kifo chake.Nimeumia sana.Hebu nieleze japo kwa undani kidogo nini kilitokea na kusababisha kifo chake? Akauliza Anitha.

Subira akavuta pumzi ndefu na kusema

“ Brigita alikuwa ni rafiki yangu mkubwa na tulikuwa tunaelewana mno.Usiku wa siku alipofariki tulipanga twende taarabu mashauzi Classic lakini baadae alibadili maamuzi na kuniambia kwamba hangekwenda tena Mashauzi kwani alipigiwa simu na babu kwamba wanatakiwa waonane jioni ya siku ile.Safari yetu ikawa imeishia hapo,hatukutoka tena hadi nilipopata taarifa za kifo chake asubuhi.Kwa kweli hata mimi niliumia mno na hadi leo hi bado ninaendelea kuumia.Nilimpenda sana Brigita.Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa inasemekana kwamba mtungi wa gesi ulilipuka na kusababisha maafa yale” akasema Subira

“ Pole sana Subira” akasema Anitha

“ Nimekwisha poa” akajibu subira

“ Umesema kwamba mlipanga muende mashauzi Classic lakini mkaahirisha aliposema kwamba alipigiwa simu akaonane na babu.Huyu babu ni nani?

Subira akatabasamu kidogo na kusema

“ Brigita alikuwa na mahusiano na mzee mmoja hivi ambaye ndiye aliyemjengea nyumba,akamnunulia gari na ndiye aliyekuwa akimuhudumia kwa kila kitu.Mzee Matiku alifariki dunia wiki mbili tu baada ya Brigita kufariki kwa kujipiga risasi ya kichwa.Inasemekana kifo cha Brigita kilimuumiza sana na ndiyo maana akaamua kujimaliza kwa risasi. ”

“ Dah ! akasema Anitha

“ Nakumbuka Brigita aliwahi kuwa na mahusiano na kijana mmoja hivi anaitwa Edson.Aliwahi kunitumia picha wakiwa naye.Gosh he was very handsome,je waliachana hadi akaamua kuingia katika mahusiano na huyo mzee? Akauliza Anitha

“ Edson ninamfahamu lakini naye alikwisha fariki dunia.Aliuliwa na mpenzi wake.Ninachokifahamu mimi,Brigita na Edson walikuwa wanakutana kwa siri.Hakuwa akimpenda mzee Matiku na alikuwa naye kwa ajili ya pesa zake tu lakini moyo wake ulikuwa kwa Edson.Mzee Matiku alikuwa na wivu uliopitiliza na aliwahi kumwambia Brigita kwamba siku akimkuta na mwanaume mwingine basi huo ungekuwa ni mwisho wake.Brigita alimuogopa sana mzee Yule hivyo akawa akiwasiliana na Edson kwa siri.Mzee Edson alikuwa akimfuatilia sana hadi alimuwekea kifaa maalum katika simu yake cha kuchunguza watu aliokuwa akiwasiliana nao.Hakutaka kabisa amuone na mwanaume yeyote zaidi yake.Brigita alianza kuchoshwa na mahusiano yake na Yule mzee na kila siku alikuwa akiniambia kwamba siku moja lazima atakuja kumkimbia .Aliniambia kwamba kuna biashara wanataka kuifanya na Edson na endapo ikifanikiwa basi watapata pesa nyingi na kisha atamkimbia mzee yule na kuhama kabisa nchi.Hakuwahi kuniambia ni biashara gani walitegemea kuifanya na Edson.Siku moja aliniambia kwamba kuna kitu amekichukua toka kwa mzee Matiku ambacho endapo angegundua basi kingemletea shida sana.Hakuniambia ni kitu gani hadi alipofariki.” Akasema Subira

“ Huyo mzee Matiku alikuwa anafanya kazi gani? Alikuwa na familia?

“ Mzee Matiku ni mfanyabiashara,ndiye mwenye ile hoteli niliyokuwa nikifanya kazi na ndiyo maana Brigita alikuwa na kazi nzuri sana pale.Watu wanasema kwamba ni mwanajeshi mstaafu.Wanasema kwamba aliwahi kuwa mlinzi wa rais miaka ya nyuma sana.Kwa upande wa familia mzee Matiku hakuwa na familia” akasema Subira.

“ Subira nashukuru sana kwa kunipa mwanga kuhusiana na kifo cha rafiki yangu Brigita.Kwa sasa kuna mahala ninatakiwa kwenda ila nitakutafuta mwishoni mwa wiki tukae tuongee na unieleze mambo mengi kuhusiana na Brigita na pia unitambulishe kwa ndugu zake unaowafahamu ili niweze kuwapa pole.Ahsante sana kwa muda wako na tutaonana tena” akasema Anitha huku akifungua pochi yake na kumpatia Subira kiasi cha dola hamsini za Marekani halafu wakasimama na kuondoka

“mambo mapya yanazidi kuibuka kila siku.Kwa sasa tuna mtu mwingine ameongezeka katika uchunguzi wetu,babu Matiku.” Akasema Mathew wakiwa garini wakiondoka maeneo ya chuo

“ Brigita alikuwa na mahusiano na mzee Matiku na wakati huo huo akawa na mahusiano ya siri na Edson.Walikuwa wakiwasiliana kwa siri ili mzee Yule asigundue na ndiyo maana laini ile ya simu ya Edson iliwekewa uzio ili mtu mwingine asiweze kugundua walichokuwa wakikiongea.Kwa mujibu wa Subira siku chache kabla ya kifo chake Brigita alimweleza kwamba kuna kitu alikichukua toka kwa mzee Matiku je ni kitu gani hicho? Ni biashara gani aliyokuwa akiifanya na Edson ambayo ingewapatia pesa nyingi kiasi cha kumfanya Brigita afikirie hatan kukimbia na kuhama nchi? Akauliza Mathew

“ Majibu ya maswali haya yanakuwa magumu kupatikana kwa sababu wahusika wote ambao wangeweza kutupatia majibu wamekwisha fariki.Tumerudi katika sifuri .Lakini kuna muunganiko wa kifo cha Edson,Brigita na mzee Matiku.Sababu ya vifo vyao ni moja.Ninahisi hicho kitu Brigita alichokichukua toka kwa mzee Matiku alimshirikisha pia Edson na inawezekana ndiyo iliyosababisha vifo vyao.Je ni kitu gani hicho? Ni biashara gani walitaka kuifanya? Mzee matiku ni nani? Nadhani ili tupate mwangaza tunatakiwa tumfahamu pia huyu mzee ni nani ,vyanzo vyake vya mapato n.k.Yawezekana akawa ni mtu aliyekuwa akijishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya..” akasema Mathew lakini akastuliwa na Anitha

“Mathew…!!” Anitha akaita

“ Kamera kipepeo nyumbani kwa Penny imetoa mlio.Kuna watu wanaingia nyumbani kwa Penny” akasema Anitha.Mathew akasogeza gari pembeni na kusimama akawatazama watu wale waliokuwa wakiinga kwa Penny kupitia kompyuta ya Anitha

“ Ni sura zile zile za jana.Who are these people? Wanatafuta nini kwa penny?

“ We need to find out” akasema Mathew huku akiwashuhudia watu wale wakiufungua mlango wa Penny na kuingia ndani

“ Twende nyumbani kwa Penny.Leo lazima tuwafahamu” akasema Mathew na kuwasha gari wakaelekea nyumbani kwa Penny

TUKUTANE SEHEMU IJAYO…

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...