SIMULIZI: PENIELA (Season 1 Ep 4)
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“ Afadhali sasa nitaweza kulala usingizi.Kesi ya Penny iliyokuwa ikininyima usingizi imekwisha “ akawaza Jason
“ Nitamsaidia kwa kadiri niwezavyo hadi nihakikishe amerejea katika maisha yake ya awali.Uchumi wake umeyumba sana baada ya kukaa mwaka mzima gerezani.Bado Penny anahitaji sana msaada wangu” Akawaza halafu akastuka baada ya kukumbuka kitu
“ Kuna kitu nimekuwa najiuliza sana kuhusu Penny.Toka nimemfahamu sijawahi kuwaona ndugu zake,wala wazazi wake.
Mwaka mzima nimehangaika naye katika kesi na sijawahi kumuona ndugu yake yeyote wala hajawahi kutamka lolote kuhusu ndugu zake.Jambo hili linanifanya nijiulize maswali mengi kuhusiana na maisha yake.Je hana ndugu? Kama anao wako wapi? Kwa nini walimuacha wakati wa kipindi kigumu alichokuwa nacho?Nadhani ninahitaji kumfahamu Penny kwa undani zaidi.Kuna mambo mengi kumhusu yeye ambayo nahitaji kuyafahamu” akawaza Jason.
ENDELEA……………………………….
Jaji Elibariki aliamka asubuhi na mapema na kufanya mazoezi ya viungo kama ilivyo kawaida yake halafu akajiandaa kwa ajili ya siku hiyo na kuondoka akimuacha mkewe Flaviana akiwa bado amelala.Hakuweza kupata usingizi usiku huo kutokana na kichwa chake kuwa na mawazo mengi sana.
“ Siamini kama mimi na Flaviana tumefikia hatua hii.Dharau zake zimezidi.Dharau alizonionyesha jana zimevuka mipaka. Nadhani kinachompa kiburi na kumfanya awe na dharau ni kuwa mtoto wa rais na baba yake ndiye aliyeniteua kuwa Jaji.
Kwa kigezo hicho walitegemea wanitumie watakavyo.Hapana.Siwezi kukubali kutumika.Nimekwisha vumilia mambo mengi sana toka kwa Flaviana na sasa nadhani imetosha.Nilijitahidi kuvumilia ili kuinusuru ndoa yetu lakini kwa sasa litakalotokea na litokee tu.Kuna mambo mawili ambayo natakiwa kuyafanya .Moja ni kutafuta nani muuaji wa Edson.Pili ni kuanza maandalizi ya maisha mapya kwani nina hakika muafaka kati yangu na Flaviana hautapatikana. Akawaza Jaji Elibariki wakati akikata kona kuingia Mandarini Hoteli kwa ajili ya kupata kifungua kinywa
Alihudumiwa haraka haraka na wakati akiendelea kupata kifungua kinywa akachukua simu yake na kumpigia rafiki yake Stanley
“ Halo Stanley.
Habari za asubuhi?
“ Habari za asubuhi nzuri Jaji.Nimestuka kidogo kwa simu ya asubuhi asubuhi namna hii” akasema Stanley
“ Stanley nimekupigia ninakuomba msaada wako.”
“ Nakusikiliza Jaji”
“ Kuna Yule wakili wa Yule msichana Peniela ambaye kesi yake imekwisha jana akachiwa huru, anaitwa Jason Patrick,unaweza ukanisaidia kupata mawasiliano yake?
“ Usihofu.
Nitakupatia mawasiliano yake ndani ya nusu saa” akajibu Stanley na kukata simu
Jaji Elibariki akavuta pumzi ndefu na kuwaza
“ Nadhani Jason ni sehemu nzuri ya kuanzia uchunguzi wangu.Yeye ni wakili wa Penny na nina hakika kuna mambo mengi anayoyafahamu kuhusiana na maisha ya Penny.Ninaweza kupata kitu toka kwake kitakachonisaidia katika uchunguzi wangu.Nitapenda vile vile nionane na Peniela ana kwa ana lakini makutano yetu yawe katika sehemu ya siri.
Sitaki nionekane nikiongea naye watu wanaweza wakahisi vibaya kwamba pengine nilifanya makusudi kumuachia kwa kuwa nina mahusiano naye Fulani” akawaza Jaji Elibariki na kutabasamu baada ya kumkumbuka Penny.
“ Penny ni msichana mrembo sana aliyebarikiwa uzuri wa aina yake.Ningefanya kosa kubwa sana kama ningemfunga gerezani msichana kama Yule” akawaza jaji Elibariki halafu akamaliza kupata kifungua kinywa na kuondoka kuelekea ofisini kwake.
“ Clara sihitaji kuonana na mtu yeyote siku ya leo.” Akampa maelekezo katibu muhtasi wake kisha akajifungia ofisini kwake.Hakutaka kufanya kazi yoyote siku ya leo,kichwa chake kilikuwa na wazo moja tu kumtafuta muuaji wa Edson.
“ Sina hakika kama nitampata muuaji wa Edson lakini nitajitahidi kwa kila linalowezekana hadi nimpate.Si kazi rahisi na ni ya hatari sana lakini sina namna nyingine lazima niifanye.” Akawaza jaji Elibariki na mara simu yake ikaita alikuwa ni rafiki yake Stanley
“ Hallo Stanley” akasema Jaji Elibariki
“ Jaji tayari nimekwisha pata mawasiliano ya Jason Patrick na nitakutumia sasa hivi katika ujumbe mfupi” akasema Stanley.Baada ya dakika moja ujumbe mfupi ukaingia katika simu ya Elibariki ukiwa na mawasilinao ya Jason,kuanzia namba za simu barua pepe,n.k.
Jaji Elibariki akashusha pumzi na kuziandika namba za simu za Jason akapiga
“ hallow” ikasema sauti ya upande wa pili baada ya kupokea simu
“ hallow.Naongea na wakili Jason Patrick?
“ Ndiye mimi.Nani mwenzangu?
“ Jaji Elibariki.”
“ jaji Elibariki?!...
Jason akashangaa hakuwa ametegema hata siku moja jaji Elibariki angempigia simu kwani hawakuwa na mahusiano yoyote zaidi ya kukutana mahakamani
“ Ndiyo Jason.Ni mimi Elibariki”
“ Nafurahi kupata simu yako Jaji Elibariki.Nikusaidie nini?
“ Jason nina shida nahitaji kukuona.”
“ Shida gani hiyo? Hatuwezi kuzungumza katika simu kwa sababu leo nina mizunguko mingi”
“ Ni jambo ambalo hatuwezi kuliongea simuni Jason”akasema Elibariki
Jason akafikiri kidogo na kuuliza
“ What is that about?
“ Its about Penny “ akajibu Jaji Elibariki
Jason akafikiri kidogo na kusema
“ Ok mheshimiwa.Tuonane wapi?
“ Tukutane Mandarini hotel saa tano asubuhi hii.Nitakuwa juu ghorofani ” akasema Jaji
“ Ok jaji nitajitahidi kufika kwa wakati” akasema Jason na kukata simu
“ Hii ndiyo hatua ya kwanza.Baada ya kuonana na Jason nitajua nini cha kufanya” akawaza Jaji Elibariki
************
Saa tano na dakika saba ,Jason akawasili Mandarini hoteli,akaegesha gari na kushuka akapanda hadi sehemu ya juu alikoelekezwa na Jaji Elibariki ambaye tayari alikwisha wasili kitambo
“Hallo Jason.Karibu sana” akasema Jaji Elibariki akimkaribisha Jason
“ Ahsante sana mheshimiwa jaji.”
Akasema Jason na kuvuta kiti .Muhudumu hakuchelewa akafika na kumuhudumia kinywaji
“ Jason samahani sana kwa kukuharibia ratiba zako,najua wewe ni mtu mwenye shughuli nyingi” akaanzisha mzungumzo Jaji Elibariki
“ Usijali mheshimiwa.Najua usingefanya hivyo kama kusingekuwa na jambo la msingi.Hata hivyo ninashukuru kukutana nawe ana kwa ana.Tumekuwa tunakutana tu katika kesi mahakamani.” Akasema Jason
“ Ni kweli Jason ,kuna jambo la msingi lililonifanya nilazimike kukuita hapa.Hata mimi kwa upande wangu ninafurahi pia kukutana nawe.Ulinifurahisha sana namna ulivyoisimamia kesi ya Penny.Katika maisha yangu ndani ya sheria sijawahi kukutana na wakili mahri kama wewe.You are the best Jason.Hongera sana” akasema Jaji Elibariki na wote wakaangua kicheko.
“ Ahsante kwa pongezi mheshimiwa.Hata mimi vile vile napenda nikupongeze kwa namna ulivyoiendesha kesi ile na hukumu ya haki uliyoitoa.Hukumu ile imedhihirisha kwamba mahakama iko kwa ajili ya kutoa haki bila kujali cheo cha mtu,uwezo rangi au mahala atokako.Nakupongeza sana mheshimiwa” akasema Jason ,wakainuka na kushikana mikono.
“ Ahsante sana Jason.Nilitoa hukumu ile kutokana na namna ulivyoweza kuithibitishia mahakama kwamba Penny hakutenda lile kosa.Upande wa mashitaka uliwasilisha ushahidi mwingi ambao ungeweza kumtia hatiani Penny lakini kwa umahiri wako uliweza kuufanya ushahidi ule ukose nguvu na hivyo Penny akaachiwa huru”Akasema Jaji Elibariki halafu kikapita kimya kifupi kisha akasema
“ Jason kuna jambo ambalo nimekuitia hapa linalohusiana na Peniela.” Akasema Jaji na kukaa kimya kidogo halafu akaendelea
“ Katika kesi iliyomalizika kulikuwa na nguvu kubwa iliyotumika kuhakikisha kwamba Penny anakutwa na hatia ya mauaji,lakini toka ndani ya moyo wangu ninaamini Penny hakutenda kosa lile” akasema Jaji
“ Nashukuru Jaji kwa kulitambua hilo.Nadhani ni mimi na wewe pekee ambao tunaamini kwamba Penny hakuua.” Akasema Jason
“ Kweli kabisa Jason.
Wengi wanaamini kwamba Penny alimuua Edson kutokana na mazingira yenyewe ya tukio.Lakini mwisho wa yote ukweli utabaki pale pale kwamba Penny hakuua.Lakini kuna swali ambalo nimekuwa najiuliza bila majawabu na ambalo limenifanya nikuite hapa asubuhi hii,je kama Penny hakuua nani basi alimuua Edson??
Kimya cha dakika mbili kikapita kila mmoja akifikiria halafu Jason akasema
“ Jaji Elibariki,swali hilo ni gumu mno.Hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali kama hilo je nani aliyemuua Edson na kesi akaangushiwa Penny lakini nimekosa majibu”
“ Jason ,ukweli ni kwamba Penny yuko huru lakini hayuko salama na hata sisi ambao tumefanikisha yeye kuwa huru bado hatuko salama pia.Kuna jambo nalihisi litakua nyuma ya mauaji yale na ndiyo maana nikakuita hapa ili tujadili na kwa pamoja tushirikiane tumpate muuaji wa edson.Ni hilo tu ndilo litamuhakikishia usalmaa Penny na sisi sote.Bila kumpata muuaji ,sikufichi maisha ya Penny yatakuwa hatarini.”
“ Nakubaliana nawe Jaji.Hata yeye mwenyewe amekwisha anza kuhisi kwamba ,maisha yake hayatakuwa na amani kwani aliahidiwa na mtoto wa rais kwamba lazima atayafanya maisha yake yawe magumu”
Jaji Elibariki akatabasamu kidogo na kusema
“ hayo ni mambo ya kawaida kwa wanawake kwani inasemakana Edson alikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na Anna mtoto wa rais kabla ya kuanzisha mahusiano na Peniela kwa hiyo vitisho kama hivyo ni vya kawaida .Tunachohitaji sisi ni kumtafuta muuaji halisi wa Edson.
Jason wewe umekuwa wakili wa Penny na ninatumai kuna mambo mengi ambayo amekueleza .Je hajawahi kukueleza chochote kwamba anahisi nani anaweza kuwa muuaji wa Edson?
“ Hapana mheshimiwa jaji.Penny hajawahi kunieleza chochote kuhusiana na nani anahisi anaweza kuwa muuaji wa Edson.Maelezo aliyonipa mimi siku zote ndiyo yale aliyoyatoa mahakamani kwamba alimkuta Edson ameanguka ametapakaa damu kifuani pake kulikuwa na bastora na kwa taharuki aliyokuwa nayo alijikuta akiishika ile bastora bila ya kujua kwamba inaweza kumtia hatiani kwani alama zake za vidole zilibaki katika ile bastora na ikasadikika moja kwa moja kwamba yeye ndiye muuaji.Mpaka leo hafahamu nani aliyemuua Edson” akasema Jason
“ Jason ninamuamini Penny.Inawezekana ni kweli hafahamu ni nani muuaji wa Edson lakini naomba mimi na wewe tushirikiane tufanye uchunguzi wetu na tumpate muuaji.Hiyo ndiyo itakuwa salama ya Penny na sisi sote.Toka nimeingia katika sheria sijawahi kukutana na kesi ambayo nguvu kubwa imetumika ili kuhakikisha mshtakiwa anapatikana na hatia kama hii.Hii inanishawishi kuchimba kwa undani zaidi kuhusiana na kifo cha Edson.”
“ Nakubaliana nawe jaji.Niko tayari kuungana nawe ili kufanya uchunguzi na kumpata muuaji japokuwa si suala rahisi na ni la hatari kubwa.Je unashauri tufanye nini?
“ Ahsante sana Jason kwa kukubali.Kitu cha kwanza ambacho nataka unisaidie,nahitaji kuongea na Penniela ana kwa ana lakini katika sehemu yenye usiri .Sitaki kuonekana na watu niko naye kwani wataanza kuongea mambo mengine.”
“ Sawa Jaji nimekuelewa.Nitaongea na Penniela na kumuomba akutane nawe kisha nitapanga mahala ambako mtakutana na kuongea”
**********
Wakati akina Jason wakiwa katika mazungumzo hotelini juu ya kumpata muuaji wa Edson,Penny alikuwa amekaa sebuleni kwake akitazama runinga.Hakujisikia kutoka siku hii.Alitaka kubaki ndani akipumzika baada ya mwaka mzima kusota gerezani.Akiwa amejilaza sofani kengele ya mlangoni ikalia,akainuka akachungulia nje kupitia dirishani,na kukutana na sura ambayo ilimstua sana.
Alihisi mwili ukimtetemeka kwa uoga.
No comments
Post a Comment