SIMULIZI: PENIELA (Season 1 Ep 5)
ILIPOSHIA SEHEMU ILIYOPITA
Wakati akina Jason wakiwa katika mazungumzo hotelini juu ya kumpata muuaji wa Edson,Penny alikuwa amekaa sebuleni kwake akitazama runinga.Hakujisikia kutoka siku hii.Alitaka kubaki ndani akipumzika baada ya mwaka mzima kusota gerezani.Akiwa amejilaza sofani kengele ya mlangoni ikalia,akainuka akachungulia nje kupitia dirishani,na kukutana na sura ambayo ilimstua sana.Alihisi mwili ukimtetemeka kwa uoga.
ENDELEA………………………………….
“ Ivan!!..akasema Penny kwa sauti ndogo .Bado mwili uliendelea kumtetemeka.Aliogopa sana.Kengele ya mlangoni iliendelea kulia,akavuta pumzi ndefu na kwenda kuufungua mlango .Mtu mmoja mwembamba mrefu ,aliyevaa suti nzuri nyeusi na miwani myeusi alikuwa amesimama mlangoni akiwa ndani ya tabasamu .Mkononi alikuwa ameshika lundo la maua mazuri.Wakatazamana kwa sekunde kadhaa
“ Welcome back Penny.I missed you so much.Even after a year in prison you are still as pretty as you used to be ” akasema Yule mtu.Penny hakuonekana kujali alichokiongea Ivan akamuuliza kwa ukali
“ What are you doing here Ivan?
“ Ouh Penny bado hujaacha machachari yako tu? Akasema Ivan huku akiendelea kutabasamu
“Ivan sema kilichokuleta tafadhali na uondoke mara moja.I don’t want to see you here” akasema Penny kwa sauti iliyoonyesha lwamba hakuwa na masihara
“ Hunikaribishi hata ndani Penny? Hatujaonana kwa muda mrefu “ akasema Ivan
“ Ivan tafadhali nakuomba sema kilichokuleta na uondoke.” Akasema Penny.Ivan akatabasamu na kusema
“ Ok Penny nimetumwa nikuletee mzigo huu”
“ Nani kakutuma?
“ Ivan hakujibu kitu akampa Penny ule mzigo wa maua.Penny akaupokea na kuuangalia kwa hasira
“ Kwa heri Penny.Nimefurahi kukuona tena” akasema Ivan na kuanza kupiga hatua kuondoka
“ Ivan please don’t come back here again” akasema Penny lakini Ivan hakugeuka akaingia katika gari lake na kuondoka,akimuacha Penny bado amesimama mlangoni
Baada ya Ivan kuondoka ,Penny akafunga mlango na kuyatupa yale maua mezani.Akayaangalia na kusema kwa sauti ndogo
“ After one year in prison,leo ndiyo ananikumbuka bazazi mkubwa Yule” Toka ndani ya maua yale kikaanguka kikadi kidogo chenye maandishi” welcome back”.Akiwa bado amesimama akitafakari mara simu ya mezani ikaita akaenda kuipokea
“ Hallow” akasema penny
“ Hallow Penny” ikasema sauti ya upande wa pili ambayo Penny aliitambua.
Kikapita kimya kifupi
“ What do you want from me? Akauliza Penny
“ Is that how you say hello to the love of your life? Akauliza mtu Yule.
“ Niambie tafadhali ni kitu gani unakitaka toka kwangu? Akauliza Penny
“ Penny naomba kwanza nikupe pole nyingi kwa masahibu makubwa yaliyokupata lakini vile vile napenda kukukaribisha tena uraiani.Tatu, leo jioni nataka kukutana nawe kwa chakula.Nitamtuma dereva aje akuchukue saa moja na nusu za jioni” akasema Yule mtu na kukata simu.Penny akabaki amesimama ameushikilia mkono wa simu.
Alizama katika mawazo.Akiwa bado amesimama akiwaza mara kengele ya
mlangoni ikalia na kumstua.Haraka haraka akayakusanya yale maua na kuyafungia kabatini halafu akaenda kufungua mlango akakutana na wakili Jason
“ Jason” akasema Penny kwa mshangao kidogo kwani hakuwa ametegemea kama Jason angefika kwake mida ile
“ Hi Penny”
“ Hi Jason” akasema Penny na kumkaribisha Jason ndani.
“ Utanisamehe Penny nimekuja bila taarifa”
“ Bila samahani Jason.Hapa ni nyumbani kwako na una ruhusa ya kuja muda wowote na unakaribishwa bila hata kubisha hodi” akasema penny na kumfanya Jason atabasamu
“ Ahsante sana penny”
“ Jason unatumia kinywaji gani?
“ Ahsante Penny lakini kwa sasa sihitaji kinywaji chochote ila nimepita tu kutokana na suala la dharura lililojitokeza asubuhi ya leo”
“ Dharura gani hiyo?
Kuna tatizo? Akauliza Penny kwa wasi wasi
“ Jaji Elibariki alinipigia simu asubuhi akataka nionane naye”
“ Jaji Elibariki?!!..Penny akashangaa
“ Ndiyo “
“ Kuna tatizo gani tena? Akauliza Penny
“ Kuna suala nyeti ambalo aliniitia”
“ Suala gani hilo?
“ Anataka tumtafute muuaji wa Edson”
“ Muuaji wa edson? Penny akazidi kushangaa
“ Ndiyo Penny.Jaji Elibariki amekuwa akijiuliza swali ambalo hata mimi nimekuwa nikijiuliza bila kupata majbu,kwamba nani alimuua Edson ? Wote tuna hakika kabisa kwamba hukumuua lakini sasa nani alimuua? Tunahitaji kufanya uchunguzi na kulibaini hilo.Penny akamtazama Jason kwa sekunde kadhaa na kusema
“ Jason,siwezi kupingana na mawazo yako wala ya jaji Elibariki kwani hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali kama hilo bila kupata jibu lakini kesi imekwisha na mahakama haijanikuta na hatia,ni kazi ya vyombo vya dola sasa kufanya uchunguzi na kubaini ni nani muuaji wa Edson?.Nadhani katika suala hili tuviachie vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake” akasema Penny
“ Nakubaliana nawe Penny kwamba mahakama haijakukuta na hatia na ndiyo maana ikakuachia huru lakini naomba nikuweke wazi kwamba hauko salama.Kulikuwa na nguvu kubwa iliyotaka kuhakikisha kwamba unakutwa na hatia lakini hilo likashindikana.Ni hilo ndilo lililomshangaza jaji Elibariki na kumfanya atake kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio lile na kumbaini muuaji halisi wa Edson.Watu waliofanya kila jitihada kuhakikisha kwamba unakutwa na hatia ya mauaji watakuandama usiku na mchana hadi wahakikishe wamekuangusha baada ya kushindwa mahakamani.Kwa upande wangu nimekubaliana kabisa na jaji Elibariki kwamba kuna ulazima wa kufanya uchunguzi wa siri na kumpata muuaji.
Hiyo ndiyo itakuwa salama kwako na kwetu pia” akasema Jason.Penny akasema
“ Jason nakubaliana nawe kwa kila kitu na ninakushukuru lakini kuhusu hili sina hakika kama lina umuhimu mkubwa kwa sasa.Kuhusiana na maisha yangu usihofu kabisa.I’ll be fine.”
“ No Penny you are not fine and you’ll never be fine hadi hapo tutakapomjua muuaji wa Edson.Please Penny let us do this for you.This is for your own safety “ akasema Jason
Penny akainama akafikiri kwa muda na kusema
“Jason ninaogopa kwa sababu ninajitahidi kwa kila niwezavyo kuifuta kumbu kumbu ya Edson kichwani mwangu .Sitaki tena kujihusisha na mambo yoyote yanayohusiana na Edson.He’s gone for good and I have to forget him”
“ Penny nalielewa hilo lakini hautaweza kuifuta kumbu kumbu hiyo kichwani mwako bila ya kumpata muuaji wa Edson.Utakuwa unajiuliza swali hili mara kwa mara na hautakuwa na amani”
“ Jason this isn’t an easy thing.Ni jambo zito na la hatari kubwa.
How are you going to do it?
“ Ni kweli si jambo jepesi hata kidogo na sisi ni wanasheria na hatuna utaalamu wa kufanya uchunguzi wa jambo kubwa kama hii lakini tukiunganisha nguvu zetu sote watatu tunaweza tukafanikiwa”
Penny akanyamaza akafikiri na kusema
“ Sina kipingamizi hata kidogo kuhusiana na suala hili japokuwa sikuwa nataka kujihusisha katika kitu chochote kinachohusiana na Edson lakini wewe ndiye mwanasheria wangu naamini umeona umuhimu wa jambo hili kwa hiyo naahidi kutoa ushirikiano wangu”
“ Ahsante sana kwa kukubali penny.
Kwa kuanzia,Jaji Elibariki anahitaji kukuona ana kwa ana kwa maongezi ”
“ Kuhusu nini?
“ Ni kuhusiana na suala hili .Kuna mambo ambayo anahitaji kuyafahamu kutoka kwako kabla ya kuangalia tufanye nini tena.”
“ Lini anahitaji kuonana nami?
“ Ni jioni ya leo.Tayari nimekwisha andaa chumba ,Moniz 5 star hotel ambako ndiko mtakakokutania.Jaji Elibarii alitaka makutano yenu yawe ya siri kubwa bila ya mtu yeyote kufahamu”
Penny akainama akazama katika mawazo.
Alikumbuka jioni ya ana ahadi ya kuonana na mtu kwa chakula cha jioni
“ Mambo yanaingiliana.Watu wawili wote wanataka kuonana nami usiku wa leo.Nionane na nani? Akajiuliza Penny
“ Lakini ngoja nikaonane na Jaji Elibariki.Bila yeye hivi sasa ningekuwa kifungoni.” Akawaza Penny halafu akamgeukia Jason
“ Ok Jason.Nitakwenda kuonana na Elibariki jioni ya leo”
“ Ahsante kwa kukubali Penny.Nitakupitia saa moja za jioni nikupeleke mkaonane na Jaji Elibariki halafu nitakurejesha nyumbani”
“ Sawa Jason” akajibu Penny halafu wakaagana na Jason akaondoka
*********
Katika moja ya jengo refu kabisa jijini Dar ,watu saba wameizunguka meza ya duara ndani ya ofisi nzuri iliyo katika ghorofa ya kumi na mbili.Mtu mmoja mrefu na mwenye umbo la wastani alikuwa akiongea na wengine wakimsikiliza kwa makini
“ Nimepigiwa simu na ofisi kuu asubuhi ya leo wakinionya kuhusiana na kutorudiwa tena kwa uzembe mkubwa uliopita kiasi cha kumuacha Penny akaingia katika matatizo makubwa na kuhatarisha mpango wetu wa miaka mingi.Endapo Penny angekutwa na hatia mahakamani na kufungwa ,kila kitu kingefikia mwisho.Juhudi zote za miaka zaidi ya ishirini zingekuwa ni kazi bure. Bila Penny kila kitu kitakwama .
Kwa hiyo basi maagizo niliyoyapata toka ofisi kuu ni kwamba tuhakikishe uzembe kama ule haujirudii tena na Penny apewe ulinzi wa kutosha na kumuepusha na mambo yote yanayoweza kumsababishia matatizo na kuhatarisha mpango mzima.Kazi kubwa imekwisha fanyika na tuko katika hatua za mwishoni.
Tunatakiwa kuongeza umakini maradufu.Tunatakiwa tufahamu na tuwepo kila mahala alipo Penny,tufahamu watu anaokutana nao na kwa kuanzia tunatakiwa kumfahamu Jaji Elibariki Chukuswa ambaye anakwenda kuonana na Penny jioni ya leo.”
Akasema Yule jamaa
No comments
Post a Comment