SIMULIZI: USHUHUDA WA BWANA KICHAA - II
TITLE: USHUHUDA WA BWANA KICHAA - II
ILIPOISHIA…
Chumba chenyewe huwa sio cha kulala. Huwa hakuna kitanda ila meza tu. Nilimlaza mezani hapo kwa pozi f'lani la mvuto nikaanza kumchora. Kazi ya muda mrefu kidogo. Nilipomaliza nilimbusu kwenye paji la uso kisha nikatoa visu vitatu vikali na nyundo.
SASA ENDELEA…
Kazi ukishakuwa mzoefu huwa ni nyepesi sana. Nilikuwa na uhakika wa kuimaliza kazi yangu ndani ya dakika arobaini tu. Nilimsogelea pale mezani akiwa amelala, kisha nikamuondoa nguo zake zote akabaki kama alivyozaliwa. Niliitawanya miguu yake huku na huko, huku nikiendelea kupiga mluzi ambao haukurandana na wimbo wowote ule–basi tu ilimradi nijifurahishe.
Niligeuka tena na kuchukua makasha yangu mawili, moja maalum kwa kutunzia moyo, na jingine lilikuwa na chemba mbili maalum kwa kutunzia figo mbili. Wakati huo wote ule mluzi kinywani mwangu haukutoka. Vitu hivyo vyote niliviweka karibu kabisa na ile meza ambayo nimemlaza yeye.
Nilijaribu kukumbuka kama kuna chochote nilichokisahau kabla sijaanza kazi. Ndiyo; nilikuwa nimesahau spirit. Nilirudi na kunyofoa pande la pamba, kisha nikamimina methylated spirit juu yakr, pande lile likalowa vyema.
Nilirudi mezani na kumpaka ile spirit tumboni, eneo ambalo figo hukaa (lower abdomen) kisha nikampaka na kifuani, juu kidogo ya titi lake la kushoto.
Sasa kazi ilikuwa imeiva. Nilichukua visu vyangu viwili nikamsogelea. Ghafla, bila mimi kutarajia, Malaika yule alifumbua macho, kisha akaidaka shingo yangu.
Ndugu msomaji, nilikuambia kuwa namwita malaika kwa sababu ya urembo wake? Basi hapa kuna sifa yake ya ziada. Wale malaika waliompiga na Lusifa kule mbinguni mpaka wakamshusha duniani, ndicho nilichokiona kwa malaika huyu mwenye mwili kama wa sisi binadamu. Alikuwa na nguvu mno, kiasi cha kunipiga kama mtoto mdogo pamoja na uzoefu wangu kwenye mapambano ya ana kwa ana.
Kwa kasi ya ajabu alinibamiza chini. Nilifyatuka ili nisimame haraka, lakini wapi. Alinitwanga ngumi kwenye paji la uso. Mwanzo, mokono yake niliiona laini sana, lakini aliponipiga ngumi nikahisi nimepigwa jiwe.
Niliinuka ili nijitetee, yeye akaniwahi. Mkononi tayari alikuwa na ile nyundo yangu, akanibonda kwenye bega langu la kushoto. Labda nikwambie kitu kingine ndugu msomaji; Mimi ni mtumiaji mzuri wa mkono wa kushoto (left-handed). Hata katika mapigano, huwa nautumia mkono huu kumaliza mchezo. Nitakupiga ngumi nyingi kwa mkono wa kulia lakini nitakuvizia ujae kwenye mkono wangu wa kushoto ili nikumalize. Malaika alikuwa ameniwahi, akaumaliza mkono wangu wa kushoto nguvu. Kwa maana hiyo alikuwa akinijua vyema. Mimi sikujua hilo.
Pamoja na uwezo alionionesha, sikukata tamaa, nikasimama ili kukabiliana naye. Bahati ilikuwa kwake! Alikuwa karibu na ile meza, hivyo akajiokotea kisu kimoja kati ya vile vilivyokuwepoezani. Mimi sikuwa na silaha yoyote. Tulishambuliana kwa muda mrefu kabla hajanipata tena. Kwa kutumia kile kisu akanigongomelea mkono wa kulia ukutani. Akachukua na kisu kingine, akaugongomelea mkono wa kushoto ukutani, nikaishia kutweta kwa maumivu, nikakosa la kufanya.
Haraka aliiendea blauzi wake akaivaa huku nikimwangalia. Sijui kwa nini sikuwa makini kiasi kile! Kifungo kimoja kilikuwa tofauti na vifungo vingine. Ilikuwa ni camera ndogo ya kijasusi iliyotengenezwa kwa mfano wa kishikizo cha blauzi. Ingawa mtengenezaji alijitahidi kuifanya ionekane sawa na vishikizo vingine, lakini kwa mtu makini angegundua kuwa kile hakikuwa kishikizo cha kawaida. Nilibaki nikijilaumu kwa nini sikuwa makini.
Bila hata kuvaa nguo yake ya chini, akaiendea pochi yake. Hakujihangaisha kuifungua, lakini aliikamata kisha akaongea maneno.
“I got him” (Nimempata!)” Maskini mimi! Kumbe hata ile pochi haikuwa pochi ya kawaida. Ilikuwa na kinasa sauti ambacho kilikuwa kikipeleka mawimbi ya sauti kwa washirika wake! Muda wote sikuyajua hayo.
Mara niliona hali ya yule malaika ikianza kubadilika. Akaanza kujipiga-piga kichwani, akijilazimisha hali ile isimpate, lakini haikuwa hivyo. Akajibwaga chini, ‘Pwaaaah!’ hapo ndipo nikapata majibu ya swali langu.
Bila shaka Malaika alitumia dawa iitwayo Amphetamine. Amphetamine ni dawa ya kuzuia usingizi ambayo hupingana na Valium (dawa ya usingizi). Mtu aliyetumia dawa ya Amphetamine hataweza kupata usingizi akipewa dawa ya Valium. Lakini kuna madhara makubwa kiafya kwa mtu kuchanganya dawa hizi mbili. Yaani ukimeza Amphetamine, halafu ukameza Valium baada ya muda mfupi unaweza kupata madhara kiafya kama vile kuathiri mapigo ya moyo na mzunguko wa damu ambao kama damu haitafika kwa wingi kwenye ubongo inaweza kukusababishia kizunguzungu na hata kuzimia.
Baada ya Malaika kuzimia, niliamua kutoroka upesi. Kwa bahati mbaya nilikuwa nimekwishachelewa, kwani muda huo huo waliingia wanaume watano waliovalia kiraia. Waliingia mapema kabla sijafanikiwa hata kujitoa pale ukutani.
Waliniondoa ukutani na kunivalisha pingu, kisha wakachukua kila kilichokuwepo pale chumbani kwa ajili ya ushahidi. Ushahidi mwingine yalikuwa ni maongezi ambayo Malaika alinirekodi tukiwa tunazungumza kuanzia kule bar mpaka nyumbani kwangu bila mimi kujua, pamoja na video iliyorekodiwa na camera ndogo iliyokuwa kwenye blauzi yake kwa mfano wa kishikizo.
Kama nilivyokuambia, hayo yote yalitokea siku ya juzi. Leo nikusimuliavyo mambo haya nipo mahakamani. Muda si mrefu nitapandishwa kizimbani kwa ajili ya kusomewa mashtaka yangu kwa mara ya kwanza. Namuona Malaika yupo salama salimini baada ya kutoka hospitali. Ananiangalia kwa makini huku akitabasamu; tabasamu lake la leo si la kuchombeza kama lile la juzi.
Ama kweli Malaika ameniweza!
MWISHO
No comments
Post a Comment