PENIELA (Season 1 Ep 14)

 SEASON 1

SEHEMU YA 14

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA

“ Kwa nini mlienda asubuhi?? Ilitakiwa muda ule ule ambao mmeona tukio lile la kukatika kwa mawasiliano mngenitaarifu mara moja ili nijue nini cha kufanya.Uzembe wenu unatugharimu sisi sote.Narudia tena kwamba hili ni onyo la mwisho.Kuhusu Penny kutotoa ushirikiano hilo niachieni mimi.Atake asitake lazima afanye tunavyotaka sisi na si vinginevyo.” Akanyamaza kidogo halafu akaendelea

“ Leo usiku nina kikao na wakuu cha kujadili kuhusu operesheni 26B ambayo inatakiwa kuzinduliwa rasmi upya.Kabla sijaelekea kikaoni usiku wa leo nahitaji kupata taarifa kwamba tayari mmekwisha fahamu mahala alipo Penny.Kuanzia sasa nendeni tena katika vifaa vyenu,fungueni kompyuta zenu,nendeni katika satellite na mjue wapi aliko Penny.Mna kila kitu kinachotakiwa kwa hiyo ifanyeni kazi na kabla ya saa mbili usiku wa leo nataka ripoti.” Akasema kwa ukali Captain na kutoka mle katika chumba cha mikutano akaingia ofisini kwake akajifungia.Alihisi kichwa kizito kwa mawazo.

ENDELEA…………………………………

Saa moja kasoro dakika nane za jioni,Mathew alisimamisha gari nje ya nyumba ya Bwana na Bi Robinson Kobe wazazi wa Edson.Jioni hii alikuwa ameambatana pia na wakili Jason.Geti lilifunguliwa wakaingia ndani

“ Mathew una hakika watakubali kuongea nasi wakiniona nimeongozana nawe? Akauliza Jason kwa wasi wasi

“ Usijali Jason.Wataongea nasi tu” akasema Mathew huku akibonyeza kengele ya mlango wa sebuleni ambao ulifunguliwa na mwanadada mmoja mwembamba mrefu.Aliwakaribisha sebuleni na kuwahudumiwa vinywaji na baada ya dakika kama tatu hivi wazazi wa Edson wakatokea.Bi Hellen alikuwa anatembea kwa uchovu na ilionekana wazi kwamba hali yake haikuwa nzuri.Hii ilitokana na mstuko alioupata mchana baada ya kuongea na Mathew na kumkumbusha kuhusiana na kifo cha mwanae Edson .Jason na Mathew wakasimama na kuwasalimu wazee wale kwa heshima .Bado Bi Hellen aliendelea kumuangalia Jason kwa macho makali sana .Ilionyesha wazi kwamba hakupendezwa na uwepo wake pale

“ Karibuni vijana” akasema mzee Robinson Kobe

“Nimeambiwa kwamba mna jambo mnataka kuzungumza nasi”

“ Ndiyo mzee.Tulionana na mama mchana na tukaomba tukutane na kuonana nanyi.Tuna jambo tunataka kuzungumza nanyi wazee wetu” akasema Mathew

“ Ni kuhusu nini? Akauliza mzee Robinson

“ Ni kuhusu mwanetu Edson”

“ Kuna jambo gani kumuhusu Edson? Kesi yake imekwisha malizika na mtuhumiwa akaachiwa huru.Huyo mwenzako anafahamu kila kitu kwani yeye ndiye aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa” akasema mzee Robinson

“ Nalifahamu hilo mzee” akasema Mathew na kunyamaza kidogo kisha akaendelea

“ Wazee wangu naomba kwanza nijitambulishe kwenu kwa sababu huyu mwenzangu tayari mnamfahamu.Mimi naitwa Mathew Kwanga.Kazi yangu ni mchunguzi wa kimataifa.Ninapokea na kufanya kazi mbali mbali za kiuchunguzi toka sehemu mbali mbali duniani” akanyamaza kidogo na kuendelea

“ Nilifuatwa na ndugu zangu hawa wawili.Jason na mwingine ambaye tulitakiwa kuwa naye hapa lakini amepata udhuru .Yeye ni Jaji Elibariki ambaye alikuwa akiisikiliza kesi ya mauaji ya Edson.” Akasema Mathew.Wazazi wa Edson wakatazamana baada ya jina la Jaji Elibariki kutajwa

“ Ndugu zangu hawa “ akaendelea Mathew

“ Waliniomba niwasaidie kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo chenye utata cha kijana wenu Edson na kumfahamu nani muuaji”

Kabla hajaendelea mzee Robinson akaingilia kati

“ Kijana Uchunguzi ulikwisha fanyika na mtuhumiwa akapatikana japokuwa mahakama kwa sababu wanazozijua wao wakamuachia huru. Sioni haja ya kufanya tena uchunguzi kwa sababu jambo hili sisi tumekwisha muachia Mungu kwani yeye pekee ndiye mwenye kutenda haki.Duniani hapa hakuna haki” akasema mzee Robinson akionekana kukata tamaa

Jason aliyekuwa kimya toka wamefika akakohoa kidogo na kusema

“ Mzee naomba na mimi niongee kidogo” akasema huku akitazamana na mzee Robinson.Akaendelea

“ Naomba niwafahamishe wazee wangu kwamba Peniela siye muuaji wa Edson?

Kauli ile ilimfanya mzee Robinson amtazame kwa jicho kali na kusema

“ Kijana ,nafahamu kwamba wewe ni mwanasheria mahiri kabisa na umeifanya kazi yako vyema ya kuishawishi mahakama ikakubali kumuachia huru mteja wako.Najua hata siku moja hutakubali kwamba mteja wako alimuua mwanetu.Yote hii ni kwa sababu anakulipa pesa nyingi.Pesa inaweza kufanya jambo lolote hata kupindisha sheria na wenye hatia wakaachiwa huru.Ndiyo maana hapo awali nilisema kwamba haki inapatikana mbinguni tu.Huku duniani hakuna haki.” Akasema mzee Robnson

“Hapana mzee.Si hivyo unavyofikiri.Sheria na Mahakama vimewekwa ili kutoa haki.Mahakama haiko kwa ajili ya kupindisha sheria na kulipendelea kundi fulani la watu kwa sababu ya pesa zao au nafasi zao.Peniela aliachiwa huru baada ya mahakama kuridhika kwamba hakuwa na hatia.Hakutenda kosa.Hakumuua Edson.Baada ya kesi kumalizika na Peniela kuachiwa huru ,Jaji Elibariki ambaye ndiye aliyetoa hukumu ile alinifuata na kunieleza nia yake ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo cha Edson.Aliamua kufanya hivyo kutokana na sintofahamu nyingi alizozigundua katika mwenendo mzima wa kesi ile.” Jason akanyamaza kidogo na kusema

“ Kumekuwa na maneno mengi na hisia tofauti kuhusiana na hukumu ile kwa hiyo tunataka tufanye uchunguzi wa kina tuufahamu ukweli.Tumfahamu muuaji wa edson na kumfikisha sehemu husika apate adhabu stahili.Kwa kuwa sisi ni wanasheria na hatuna taaluma ya kiuchunguzi tumeamua kutumia gharama zetu kumkodisha huyu ndugu yetu Mathew aweze kuifanya kazi hiyo.Yeye amebobea katika masuala haya ya kiuchunguzi,amekwisha fanya kazi katika idara mbali mbali nyeti za kiusalama hapa nchini kabla ya kuamua kufanya kazi zake binafsi.Kabla ya kuanza kufanya uchunguzi wake Mathew ameona ni bora aje azungumze nanyi mambo kadhaa. “ akasema Jason.Kimya kikatawala pale sebuleni.Mzee Robinson aliinama akatafakari huku akikuna kichwa chake.Baada ya dakika mbili akainua kichwa na kusema

“Natamani niamini maneno uliyoniambia kijana wangu lakini nafsi yangu inakataa kabisa. Sidhani kama kuna kitu cha kunishawishi niamnini kwamba Penny siye aliyemua mwanangu” akasema mzee Robinson

“ Mzee wangu sina kitu cha kukushawishi kwa sasa lakini naomba unipe muda kidogo tu na nitakuwa na cha kukukushawishi uamini hivyo.Ninachohitaji toka kwenu sasa ni ushirikiano tu” akasema Mathew.Mzee Robinson akainama akafikiri na kusema

“ Unahitaji nini toka kwetu?

“ Mzee,mimi ni mzoefu katika masuala haya .Nimekwisha fanya chunguzi mbali mbali za vifo vyenye utata kama hiki cha mwanao.Mara nyingi kinapotokea kifo kama hiki kunakuwa na sababu Fulani nyuma yake.Sitaki kuongea sana lakini ninachotaka kukisema ni kwamba tutaifahamu sababu hiyo na kwa nini Edson aliuawa.Sahauni uchunguzi uliopita na tushirikiane katika uchunguzi huu tunaotaka kuufanya. Kitu cha kwanza ninachotaka kukifahamu toka kwenu japo kwa ufupi tu ni kuhusiana na mwanenu Edson alikuwa ni mtu wa namna gani?



Mzee Robinson akavuta pumzi ndefu na kusema

“ Edson alikuwa ni mtoto pekee wa kiume kati ya watoto wanne tulionao.Kimakuzi Edson tumemlea katika maadili mazuri.Alikuwa ni kijana mtaratibu sana na asiye na makuu.Alipohitimu shahada yake ya mawasiliano nchini marekani alirudi nchini na akapata kazi katika kampuni moja ya simu na baadae akapata kazi ikulu katika kitengo cha mawasiliano ambako alifanya kazi hadi mauti yalipomkuta.Kitabia Edson hakuwa na tabia ambayo naweza kusema kwamba ni mbaya,hakuwa mnywaji wa pombe ,wala mtumiaji wa kilevi chochote kile.Muda mwingi aliutumia kwa kusoma na kufanya kazi zake.Alipoanza kazi ikulu alianzisha mahusiano na kimapenzi na Anna binti wa rais.Urafiki wao ulianza toka wakiwa wadogo kwa sababu familia zetu mbili ni familia rafiki kwa muda mrefu sana.Baada ya kuingia katika mahusiano na Anna,tuliamua kumpatia moja ya nyumba zetu aishi ili aweze kuwa huru.Edson na Anna walipendana sana na sote tulikuwa na matarajio makubwa kwamba siku moja familia zetu mbili zingeweza kuunganishwa na hawa vijana lakini ghafla tukasikia kwamba wamefarakana na tayari Edson alikuwa katika mahusiano na msichana mwingine aitwaye Peniela.Hatukutaka kuingilia mambo yake ya kimahusiano tukamuacha aendelee na Peniela hadi pale mauti yalipomkuta.Kwa ufupi hivyo ndivyo ninavyoweza kumuelezea mwanangu Edson japokuwa kuna mambo mengi sana ambayo naweza kuyaeleza. Kuhusiana naye” akasema mzee Robinson

“ I see….He was a nice guy..” akasema Mathew

“ Yah ! ..” akajibu mzee Robinson

“ Siku chache kabla ya kifo chake ulifanikiwa kuonana naye? Alikuwa katika hali gani? Kuna kitu chochote ambacho hakikuwa cha kawaida kwa namna ulivyomuona? Akauliza Mathew.Mzee Robinson akafikiri kidogo na kusema

“ Nilionana naye wiki mbili kabla ya kifo chake.Alikuja ofisini kwangu tukaongea kidogo akaondoka.Alikuwa katika hali ya kawaida kabisa.Ninachokumbuka ni siku tatu kabla ya kifo chake alimpigia simu mama yake usiku na kuongea naye.Alikuwa anamsalimu tu.Hakuwa na kawaida ya kupiga simu usiku lakini hakusema kama ana tatizo lolote ” akasema mzee Robinson

“ Nilifika katika nyumba aliyokuwa akiishi Edson nikaambiwa kwamba umeiuza” akasema Mathew

“ Ndiyo niliamua kuiuza ile nyumba. Sikutaka kuendelea kuimiliki ile nyumba baada ya mwanangu kuuliwa ndani yake” akasema mzee Robinson

“ Vifaa vyake mmevihifadhi wapi? Akauliza Mathew

“ Tuna nyumba ndogo iko huko nyuma ndiko tumevihifadhi”

“ Nitahitaji kuvipitia baadhi ya vitu vyake kama vitabu vya kumbu kumbu ili tuonne kama kuna kumbu kumbu yoyote isiyo ya kawaida ambayo anaweza kuwa aliiweka vitabuni ,vile vile kompyuta yake pamoja na simu” akasema Mathew

“ Edson alikuwa na vitabu vingi sana kwani alikuwa msomaji mzuri.Nadhani tunaweza kuchukua siku kadhaa kuvipitia vyote kuchambua kimoja kimoja.Kuhusu kompyuta zake ni kwamba hazikuwahi kuonekana na hatujui ni nani aliyezichukua.Simu yake pia haikuwahi kuonekana.Hatuelewi ni kwa nini vitu hivi vilitoweka katika mazingira yenye utata mkubwa. Akasema mzee Robinson

“ Baba Eddy..! akaita Bi Hellen

“ Kuna kitu nimekikumbuka.Katika mojawapo ya chungu cha maua kilichokuwa chumbani kwake siku tunahamisha vyombo vyake ilianguka laini ya simu ambayo nimeihifadhi ndani.Nadhani inaweza ikawa ni ile laini ya simu ambayo aliitumia aliponipigia simu mara ya mwisho kwa sababu hakutumia namba zake ninazozifahamu.” akasema Bi Hellen

“ Ok,nitaomba unipatie laini hiyo ya simu ili tuifanyie uchunguzi.Inaweza ikawa na jambo la muhimu kwetu” akasema Mathew na Bi Hellen akainuka akaelekea chumbani kuchukua laini ile ya simu

“ Bado sijapata jibu ni kwa nini muuaji aliondoka na kompyuta na simu wakati Edson alikuwa na kiasi cha shilingi milioni ishirini ndani.” Akasema mzee Robinson

“ Shida yao haikuwa pesa.Kuna kitu walichokuwa wakikitafuta ambacho ni zaidi ya pesa” akasema Mathew

“ Kwa mbali hata mimi ninaanza kupata picha kwamba mauaji ya kijana wangu ni tofauti kabisa na tunavyofikiri.Yawezekana kuna mtu au kitundi cha watu waliofanya mauaji yale na si Yule msichana aliyekuwa akituhumiwa” akasema mzee Robinson.Mathew na Jason wakatazamana.

“ Ahsante sana mzee kwa kuliona hilo.Jukumu letu sasa ni kubaini mtu huyo au kikundi cha watu waliotekeleza mauaji hayo “ akasema Mathew .Bi Helen akarejea na kumpatia ile laini ya simu aliyoikuta katika vifaa vya Edson

“ Wazee wangu nashukuru kwa kutusikiliza .Mimi na wenzangu tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba tunaufahamu ukweli.Nitakuwa nikiwapa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na uchunguzi wetu unavyoendelea .Ninachoomba suala hili liwe ni la siri na asifahamu mtu mwingine yeyote kwamba kuna uchunguzi unaendelea .” akasema Mathew

“ Msijali vijana wangu,muda wowote mnakaribishwa.Hapa ni nyumbani kwenu na milango iko wazi muda wote.Chochote mnachokihitaji msisite kutueleza tuwasaidie.” Akasema mzee Robinson

“ Tunashukuru sana wazee wetu.Sisi tutajitahidi kwa kila tuwezavyo kuhakikisha tumelichimba suala hili hadi katika mzizi wake na tuufahamu ukweli.Endapo kuna chochote kile mnaachoona kinaweza kutusaidia katika uchunguzi wetu msisite kututaarifu” akasema Mathew. Wakaagana na kuondoka.

“ Tayari kuna mwanga umeanza kuonekana,” akasema Mathew

“ kuna sababu iliyowafanya watu watu waliofanya mauaji ya Edson waondoke na kompyuta zake na simu.Kuna kitu gani walikuwa wanakificha? Kwa kuwa Edson alikuwa katika masuala ya mawasiliano inawezekana kuna jambo alikuwa analifahamu ambalo hakupaswa kulifahamu na kusababaisha kifo chake.Tutajua tu ni jambo gani hilo” akasema Mathew.Jason akaitika kwa kichwa alikuwa kimya sana .Mawazo yake yote yalikuwa kwa Peniela.Alijiuliza maswali mengi mahala aliko na kwa nini ameizima siku yake

“ Baba Eddy !.. akaita Bi Hellen baada ya Mathew na Jason kuondoka

“ Niliwadharau wale vijana lakini wamenifumbua macho na kwa sasa hata mimi nimeanza kuamini kwamba kuna watu walimuua mwanangu kwa sababu maalum ingawa itanichukua muda mrefu kuamini kwamba Yule msichana Peniela hakuhusika na kifo cha Edson” akasema bi Hellen.Mzee Robinson akavuta pumzi ndefu na kusema

“ Peniela hakumuua Edson” akageuka na kujifunika shuka akalala mke wake akabaki akimshangaa

*********

Jason alimfikisha Mathew nyumbani kwake na kisha akaendelea na safari ya kuelekea kwake.Mathew akaingia ndani mwake na kitu cha kwanza alichokifanya ni kuelekea katika chumba chake kikubwa kilichokuwa na runinga kubwa nane zilizotundikwa ukutani.Akaziwasha runinga zote na zikaanza kuonyesha picha zikaanza kuonekana.

“ wow ! my birds are working” akasema na kukaa kitini akaanza kufuatilia picha zile zilizokuwa zikionekana katika runinga.Runinga namba sita ilikuwa ikionyesha makazi ya Peniela.Vifaa vile mithili ya vipepeo Mathew alivyoviweka katika nyumba ya Peniela mchana vilikuwa ni kamera ambazo zilikuwa zikionyesha kila kilichokuwa kikiendelea katika makazi yale.Alizipeleka mbele picha zile na hakukuonekana mtu yeyote akiingia katika makazi yale hadi ilipotimu saa mbili na dakika ishirini na mbili.Geti dogo lilifunguliwa na watu wawili wakaingia kwa kunyata huku wakiwa na bastora mikononi.

“ Who are these people? Akajiuliza Mathew huku akiisogelea karibu runinga yake.

TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO……

No comments

Featured post

MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI

 MAMBO NANE YANAYOWAVUTIA WATEJA WENGI 1.Kuhudumiwa na Mtu anaye SMILES. Humfanya mteja ajihisi yuko huru zaidi kuuliza na kuamini unaweza k...