PENIELA (Season 1 Ep 17)
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Tunachotakiwa kufahamu watu hawa ni akina nani na nini lengo lao la kumchunguza Penny.Tayari tuna sehemu nzuri sana ya kuanzia uchunguzi wetu.Sehemu nyingine ya kufanyia uchunguzi ni katika laini ya simu ya Edson. Wauaji waliondoka na simu na pamoja na kompyuta zake zote.Inaonekana wazi kwamba kuna kitu kilichokuwa kinafichwa na ndiyo maana wauaji wale hawakuwa na shida na pesa na wakaondoka na vitu hivyo tu.Wakati wa kuhamisha vifaa vyake,ilipatikana laini ya simu ikiwa imefichwa katika chungu cha maua.Sielewi ni kwa nini aliificha laini hii ya simu lakini nina imani hakutaka ionekane kwa sababu maalum.Inaweza ikawa na msaada kwetu.Tunatakiwa tuichunguze laini hii pia” akasema Mathew.Anitha hakujibu kitu aliendelea na kazi yake ya kuunganisha mitambo yake. Nusu saa baadae alimaliza kuunganisha mitambo yake akaiwasha na kujaribu
“ Everything is in position.We can start our job now” akasema Anitha
ENDELEA…………………………..
“ Kazi ya kwanza ambayo tunaweza kuifanya usiku wa leo ni kuichunguza laini hii ya simu ili tufahamu Edson alikuwa akiwasiliana na akina nani kwa siri.Tukiwafahamu watu ambao aliwasiliana nao kwa siri kuna jambo tunaweza tukalipata toka kwao.Nina hakika lazima kuna sababu iliyomfanya Edson akaificha laini hii isionekane na mtu yeyote” akasema Mathew na kumpa Anitha ile laini ya simu akaipachika katika kifaa fulani kidogo mithili ya mkebe na kuanza kuibonyeza kompyuta yake.Baada ya sekunde kadhaa Anitha akaguna
“ Vipi mbona unaguna Anitha? akauliza Mathew
“ Laini hii ya simu imewekewa uzio.” Akasema Anitha
“ Una maana gani unaposema uzio?
“ Nina maana kwamba mtumiaji aliiwekea program maalum ambayo inaiwezesha laini hii ya simu kutumika katika simu yake tu .Inaonekana huyu jamaa alikuwa ana ufahamu mkubwa sana wa kompyuta”
“ Unaweza kuiondoa hiyo program? Akauliza Mathew
“ Ndiyo.Ninaweza kuiondoa.Hivi ni vitu vidogo sana kwangu” akasema Anitha huku akiendelea kucheza na kompyuta yake.Baada ya dakika saba akaegemea kiti na kuvuta pumzi ndefu
“ Tayari”
“ Congraturations” akasema Mathew lakini mara Anitha akaguna tena
“ This is strange !..Anitha akashangaa
“ Nini Anitha?
“ Inaonekana Edson alitumia laini hii ya simu kuwasiliana na watu wawili pekee.”
“ watu wawili ?! Mathew naye akashangaa
“ Ndiyo.Ameitumia kwa watu wawili tu”
“ Unaweza ukatafuta ni akina nani hao?
Anitha akaendelea kubonyeza kompyuta yake na baada ya dakika nne akasema
“ Kwa mujibu wa taarifa toka kampuni ya simu ya Tanphone namba hizo ni za Hellen Francis Kobe na nyingine ni ya Brigita samini.Inaonyesha Edson na Brigita wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara na hata siku moja kabla ya kifo chake Edson aliongea na Brigita kupitia laini hii.” Akasema Anitha
“ Hellen francis Kobe ni mama yake mzazi Edson na alinieleza kwamba kuna siku mwanae alimpigia simu kwa kutumia namba ngeni nadhani ni hii.Huyu Brigita simfahamu ni nani.Inawezekana alikuwa ni mtu muhimu sana kwa Edson na ndiyo maana akawa akitumia laini ya pekee kuwasiliana naye.” Akasema Mathew na kuziandika namba zile za Brigita katika simu yake akajaribu kupiga lakini hazikuwa zikipatikana.
“ Inawezekana mawasiliano ya watu hawa wawili yalikuwa ni ya siri mno.Inawezekana hata huyu Brigita hii akawa na laini ya ya siri ambayo huitumia kuwasiliana na Edson” akasema Mathew na kuzitafuta namba za simu za mzee Robinson Kobe na kumpigia
“ Hallo Mathew” akasema mzee Roinson baada ya kupokea simu
“ Samahani mzee wangu kwa kukupigia simu mida hii” akasema Mathew
“ Bila samahani Mathew.Kuna kitu chochote ninachoweza kukusaidia?
“ Ndiyo mzee.Ninataka kujua kama unamfahamu mtu anayeitwa Brigita Samini”
Kimya cha sekunde kadhaa kikapita halafu mzee Robinson akasema
“ Ninamfahamu Brigita.Edson aliwahi kunitambulisha kwake kwamba ni marafiki wakubwa.Brigita anafanya kazi katika hoteli ya kitalii ya Potina palace.”
“ Ok ahsante sana mzee” akasema Mathew na kukata simu
“ Brigita na Edson ni marafiki wakubwa kwa mujibu wa mzee Robinson.” Mathew akamwambia Anitha
“ Kama walikuwa na urafiki mkubwa kwa nini basi wawasiliane kwa siri? Akauliza Anitha
“ Hicho ndicho tunachotakiwa kukifahamu. Haiingii akilini kama watu ni marafiki wakubwa halafu wawasiliane kwa siri.Lazima kuna sababu iliyowafanya wawe na mawasiliano ya siri ” akasema Mathew na kuchukua kitabu chenye namba za simu za makampuni mbali mbali akaitafuta Potina palace hoteli anayofanya kazi Brigita.Akaipata na kuchukua namba zao za simu akapiga.
“ Karibu Potina palace nikusaidie nini? Ikasema sauti nzuri ya mwanadada baada ya kupokea simu
“ Namtafuta dada mmoja anaitwa Bigita Samini ni mfanyakazi wa hapo hotelini kwenu” akasema Mathew
“ Wewe ni ndugu yake?
“ Hapana mimi ni rafiki yake “
“ Samahani ndugu yangu Brigita hatunaye tena hapa hotelini.Alikwisha fariki dunia.”
“ Amefariki dunia?
“ Ndiyo alifariki dunia “
“ Alifariki lini na nini kilimuua?
“ Alilipukiwa na gesi na kufariki yeye na familia yake yote yapata mwaka sasa” akasema Yule dada na kumtajia Mathew tarehe ambayo Brigita alifariki dunia.Mathew akashukuru na kukata simu.
“ Vipi wanasemaje? Akauliza Anitha
“ Mambo yanazidi kuibuka.Brigita alifariki dunia wiki moja tu baada ya Edson kufariki dunia.Alilipukiwa na gesi na wakafariki yeye na familia yake yote ” akasema Mathew na kimya kikapita
“ Walikuwa wakiwasiliana kwa siri na hata vifo vyao vimetokea kwa kufuatana.Mathew kuna kitu hapa si bure.Kama walikuwa ni marafiki kuna jambo lazima watakuwa wakilifahamu kwa pamoja au wakilificha na ndiyo maana hata mawasiliano yao yalikuwa ya siri kubwa na hawakutaka mtu mwingine yeyote Yule afahamu kama walikuwa wakiwasiliana.Siri hiyo waliyokuwa wakiificha ndiyo iliyowagharimu maisha yao.” Akasema Anitha
“ Anitha inatosha kwa leo.Tupumzike na kesho tuanze kazi rasmi.Tutaanza kazi kwa kutafuta taarifa za Brigita Samini .Anaonekana ni mtu muhimu sana katika suala hili” akasema Mathew.Anitha akamtazama na kutabasamu halafu akazima kompyuta zake
“ Uko sahihi Mathew.Leo imekuwa ni siku ndefu sana.Tupumzike ili kesho tuanze kazi “ akasema Anitha
TUKUTANE SEHEMU UNAYO…
No comments
Post a Comment